Mkataba wa Lateran Miaka 94: Jubilei ya Mwaka 2025: Ushirikiano
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican tarehe 11 Oktoba 1962, katika mahubiri yake, alikazia kuhusu: Upendo ambao Kristo Yesu ameuonesha kwa Kanisa lake, licha ya dhambi, udhaifu na mapungufu ya kibinadamu na hata wakati mwingine, kumezwa na malimwengu. Hii ni changamoto na mwaliko kwa Kanisa kurejea tena katika chemchemi ya upendo ule wa awali ulioneshwa na Kristo Yesu kwa Kanisa lake: Moja, takatifu, katoliki na la mitume. Hili ni Kanisa linalotumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayomwilishwa katika imani tendaji. Kanisa katika upendo, unyenyekevu na sadaka, linakabidhiwa utume wa kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Kristo na wa Mungu; kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na utamadunisho, ili kushiriki: furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya walimwengu kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu amekazia ushiriki mkamilifu wa ukuhani wa waamini wote unaowawezesha kushiriki sadaka ya Ekaristi Takatifu, kwa kupokea Sakramenti za Kanisa, kwa kusali na kwa njia ya ushuhuda wa maisha matakatifu, toba, wongofu wa ndani, kwa kujikana na kwa upendo wenye utendaji; Umoja wa watu wa Mungu ukipewa kipaumbele cha kwanza. Kanisa litambue kwamba, maskini wanao upendeleo wa pekee mbele ya Mwenyezi Mungu. Kanisa ni Sakramenti ya umoja inayowaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na hivyo kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Ni jukumu la Mama Kanisa kuendelea kujikita katika Mapokeo, sera na mikakati ya shughuli za kiuchungaji. Mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha ushirika wa Kanisa, ili wote wawe na umoja kama Kristo Yesu alivyojisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican imekuwa ni fursa ya maandalizi ya Mwaka wa kwanza wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Hiki ni kipindi cha Kanisa kujikita zaidi katika tafakari ya kina ya Nyaraka Kuu 4 za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican yaani: “Dei verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu”, “Sacrosanctum concilium” yaani “Juu ya Liturujia”; “Lumen gentium” yaani “Fumbo la Kanisa” pamoja na “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika ulimwengu mamboleo.” Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 94 ya Mkataba wa Lateran uliofanyiwa marekebisho tarehe 18 Februari 1984 Jumanne tarehe 14 Februari 2023 ameongoza ujumbe wa Vatican uliokutana na ujumbe wa Italia uliongozwa na Rais Sergio Mattarella wa Italia. Pande zote mbili zimetia nia ya kushirikiana kwa karibu zaidi katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Mada nyingine zilizojadiliwa katika hali ya utulivu ni kuhusu: Vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi; Sera na mikakati ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na sera na mikakati yake. Kardinali Parolin anasema, kuna haja ya kuongeza mwendo katika maandalizi ya Jubilei ya Miaka 2025, kwani inaonekana kwamba, maandalizi haya yamechelewa kidogo. Sera na mbinu mkakati wa maisha ya ndoa na familia ni kati ya tema tete inayovaliwa njuga na Kanisa Katoliki nchini Italia. Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna ongezeko kubwa la umaskini wa hali na kipato kwenye familia nyingi nchini Italia, kiasi cha kutishia, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, Kanisa na Serikali ya Italia zishirikiane na kushikamana, ili dhamana na utume wa familia uweze kujipambanua bayana, licha ya changamoto ya idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa nchini Italia.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha. Kumbe, kimsingi Vatican na Italia zimekubaliana kusimamia na kuratibu mchakato wa wakimbizi na wahamiaji nchini Italia. Kuhusu vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine, kwa sasa changamoto kubwa ni kukosekana na utashi wa kisiasa wa kutaka kusitisha vita na hivyo amani na utulivu kuanza kurejea tena. Mwishoni ni kuhusu uchaguzi wa marudio uliofanyika hivi karibuni kwa ajili ya mikoa ya Lazio na Lombardia, kumekuwepo na mahudhurio hafifu sana, kiasi cha kutoridhisha hata kidogo, changamoto kwa wanasiasa katika shughuli zao za kila siku. Itakumbukwa kwamba, Vatican ni kati ya nchi ndogo kabisa duniani, tarehe 11 Februari, 2023 imeadhimisha miaka 94 tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana saini Mkataba na Serikali ya Italia “Inter Sanctam Sedem e Italiae Regnum Conventiones” kwa kifupi “Patti Lateranensi” yaani “Mkataba wa Lateran” unaoratibiwa na kusimamiwa na Sheria za Kimataifa na hivyo kuhitimisha kile kilichojulikana “Masuala ya Roma, Questione Roman.” Hii ni Italia iliyokuwa inaibuka baada ya kutenganisha shughuli za Kanisa na Serikali ya Italia. Kardinali Pietro Gasparri, Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati huo kwa niaba ya Kanisa pamoja na Bwana Benito Mussolini, Waziri Mkuu wa Italia kwa niaba ya Serikali ya Italia, walitiliana saini Mkataba wa Lateran maarufu kama “Patti Lateranensi.”
Mkataba huu ulikuwa na sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuhitimisha kinzani na mpasuko uliokuwa umejitokeza baada ya Serikali ya Italia kuvamia mji wa Roma kunako mwaka 1870. Mkataba huu ulitoa uhuru kwa Kanisa Katoliki nchini Italia kuweza kujiamria mambo yake bila kuingiliwa na Serikali. Huu ni msingi wa uhuru wa kuabudu. Vatican ikapewa mamlaka kamili ya kujisimamia yenyewe katika shughuli zake na Serikali ya Italia, tangu wakati huo ikatambua uhuru na mamlaka ya mji wa Vatican hata katika udogo wake. Mkataba huu, uliiwezesha Vatican “Kiti Kitakatifu-Holy See” kuwa na uhuru kamili kuhusiana na masuala ya dini na imani. Sehemu ya Pili ya Mkataba huu, uliitaka Serikali ya Italia kulipa fidia kwa Vatican kutokana na uharibifu mkubwa uliofanywa na Serikali wakati wa kuvamia mji wa Roma ambao ulikuwa ni ngome ya Kanisa Katoliki, kunako mwaka 1870. Serikali ikailipa Vatican fidia. Sehemu ya tatu ya Mkataba huu ni kuhusu “Makubaliano ya Kifedha” “Convenzionale Finanzarie.” Huu ni utaratibu na kanuni zinazoratibu mchakato wa mahusiano ya ndani kati ya Serikali ya Italia na Kanisa Katoliki nchini Italia. Katika sehemu hii, Maaskofu walipaswa kula kiapo cha utii kwa Serikali. Na Serikali kwa upande wake, ikalipatia Kanisa upendeleo wa kufundisha dini na kumwilisha Mafundisho tanzu ya Kanisa katika maisha ya hadhara. Serikali ya Italia ikatambua Sakramenti ya Ndoa na utenguzi wake kufanyika kwenye Mahakama za Kanisa. Mkataba wa Lateran uliifanya Vatican kutambuliwa rasmi kama nchi huru yenye uwezo wa kujiamria mambo yake yenyewe katika medani za kimataifa bila kuingiliwa na Serikali ya Italia. Papa Pio XI alilitaka Kanisa kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Italia: kiroho na kimwili; kwa kutumia amana na utajiri wake wa kihistoria, kitamaduni na kisanaa; mambo yanayofumbatwa katika Ukristo. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuihakikishia Italia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili kweli nchi ya Italia, iendelee kuwa aminifu kwa Mapokeo pamoja kupyaisha mshikamano wa udugu wa kibinadamu ambao umeipambanua Italia kwa miaka mingi.