Tafuta

Mt. Yohane Paulo II alisema, hija yake ya Kitume nchini Cuba kuanzia tarehe 21- 26 Januari 1998 ilipania pamoja na mambo mengine: Kuwaimarisha na kuwatia shime watu wateule wa Mungu nchini Cuba katika imani, matumaini na mapendo. Mt. Yohane Paulo II alisema, hija yake ya Kitume nchini Cuba kuanzia tarehe 21- 26 Januari 1998 ilipania pamoja na mambo mengine: Kuwaimarisha na kuwatia shime watu wateule wa Mungu nchini Cuba katika imani, matumaini na mapendo. 

Miaka 25 ya Hija ya Kitume ya Papa Yohane Paulo II Cuba: Ujenzi wa Upatanisho na Udugu

Huu ni wakati wa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.Misingi ya imani, iwe ni chachu ya mabadiliko katika jamii inayojikita katika ukweli, mafao ya wengi, haki, upendo na maridhiano mambo haya msingi yakiratibiwa kwa mwanga wa tunu msingi za Kiinjili na kushuhudiwa kikamilifu na watu wa Mungu nchini Cuba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kumbukizi ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II afanye hija yake ya kitume nchini Cuba kuanzia tarehe 21 hadi 26 Januari 1998, imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu Francisko, kuwaandikia barua ya kichungaji watu waaminifu wa Mungu, kuwashukuru, pamoja na kuwahimiza kuendeleza ujenzi wa matumaini unaojikita katika mizizi ya watu wa Cuba na ile ya Kikristo kwa kuwa wazi, wakarimu na watu wenye mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kwamba, barua hii ni kielelezo cha uwepo wake wa karibu na ushirika kwa watu wa Mungu nchini Cuba. Katika kumbukizi ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipofanya hija yake ya kitume nchini Cuba, Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba, lilimwalika Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, kuhudhuria tukio hili adhimu ambalo limeacha alama za kudumu katika maisha ya watu waminifu wa Mungu nchini Cuba. Imekuwa pia ni fursa ya kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Cuba kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa matumaini kwa taifa lao kwa kujikita zaidi katika uvumilivu, haki na busara kwa kukabiliana na changamoto mamboleo kwa ari na moyo mkuu, kwa kuendelea kuzama zaidi katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na zile za watu wa Cuba, ili kujenga jamii bora zaidi inayosimikwa katika uhuru kwa kutambua kwamba, uhuru unakwenda sanjari na wajibu kwa jirani na katika historia ya watu wa Mungu nchini Cuba.

Mshikamano wa Kimataifa na Cuba kwa ajili ya mafao ya wengi
Mshikamano wa Kimataifa na Cuba kwa ajili ya mafao ya wengi

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutumia fursa hii ya kumbukizi ya Miaka 25 ya Hija ya Kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Cuba, kuwahimiza kujikita zaidi katika tunu msingi za maisha ya Kikristo na zile za watu wa Cuba, ili kukuza na kuimarisha ushuhuda wa sadaka ya upendo na mshikamano kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Cuba, hususan maskini na wahitaji zaidi. Hizi ni tunu msingi zinazotoa utambulisho wa watu wa Mungu nchini Cuba yaani: Ukweli na uwazi, Ukarimu na Mshimamano wa upendo. Hii ni changamoto ya kuendelea kufanya hija ya pamoja, katika shida na mahangaiko yao, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu pamoja na Bikira Maria, Mama yake, wako pamoja na watu waaminifu wa Mungu nchini Cuba. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu na ushirika. Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.” Yer. 17:7-8. Mwishoni mwa barua yake ya kichungaji kwa watu wa Mungu nchini Cuba, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wateule wa Mungu nchini Cuba kuendelea kujiaminisha mbele ya Mungu, huku wakijitahidi kuzamisha mizizi katika maisha yao kwa ujasiri na uwajibikaji ili waendelee kuzaa matunda katika imani, matumaini na mapendo.

Vijana wasikilizwe, wapewe uhuru na kuwajibika vyema
Vijana wasikilizwe, wapewe uhuru na kuwajibika vyema

Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba, kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II atembelee nchini Cuba, limewaandikia watu wateule wa Mungu nchini Cuba ujumbe wa shukrani, kwa matukio yote yaliyofanyika kama sehemu ya kumbukumbu hii muhimu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Cuba. Maaskofu wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe wake, ambao umewapatia hamasa ya kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kujikita katika tunu msingi za Kiinjili na maisha ya watu wa Mungu nchini Cuba. Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Wakleri, amebahatika kutembelea majimbo yote ya Cuba na hivyo kuwaachia urithi mkubwa, unaoonesha ukaribu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu nchini Cuba.

Tunu msingi za maisha ya kiroho zilete mageuzi ya ndani
Tunu msingi za maisha ya kiroho zilete mageuzi ya ndani

Kardinali Beniamino Stella,ambaye alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Cuba kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka 1999 amekutana, ameadhimisha Ibada za Misa Takatifu pamoja na kuzungumza na watu wa Mungu. Kwa ufupi kabisa amekaza kusema, upendo unahitaji ujasiri wa kuweza kukabiliana na changamoto za kila siku kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kwa hakika, maadhimisho haya yamekuwa ni chemchemi ya shukrani, neema na baraka. Changamoto kwa sasa ni kuendelea kusonga mbele kwa ari na mwamko mpya, ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu, na chemchemi ya furaha na matumaini ya kweli! Katika hotuba zake, Kardinali Stella amegusia kuhusu umuhimu wa Serikali ya Cuba kutoa msamaha kwa vijana waliotiwa mbaroni kwa kufanya maandamano haramu mwezi Julai, 2021. Viongozi wa Serikali wajenge utamaduni wa kutoa uhuru kwa vijana ili waweze kujieleza na wao wawasikilize na kuwatimizia matamanio yao halali, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Hayati Papa Benedikto XVI alitembelea pia nchini Cuba
Hayati Papa Benedikto XVI alitembelea pia nchini Cuba

Uhuru wa kujieleza ni muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya, kama chachu ya mabadiliko katika medani mbalimbali za maisha ya watu wa Mungu nchini Cuba. Lakini, ikumbukwe kwamba, hata uhuru una mipaka na unawajibisha pia. Ili kupata uhuru wa kweli, kuna haja ya Cuba kujikita katika mchakato wa upatanisho na ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kutambua na kuthamini umoja na tofauti msingi zilizopo kati yao. Ni kwa njia hii, watu wa Mungu nchini Cuba katika ujumla wao, wanapaswa kujielekeza katika ujenzi wa tunu msingi za kijamii zinazosimikwa katika urafiki wa kijamii kwa ajli ya mafao ya wengi. Chuki, uhasama na mipasuko ya kijamii ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni wakati wa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.Misingi ya imani, iwe ni chachu ya mabadiliko katika jamii inayojikita katika ukweli, mafao ya wengi, haki, upendo na maridhiano. Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, Cuba imetembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, Hayati Papa Benedikto XVI na hatimaye, Papa Francisko.

Ni wakati wa upatanisho, mshikamano na udugu
Ni wakati wa upatanisho, mshikamano na udugu

Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II alisema, hija yake ya Kitume nchini Cuba kuanzia tarehe 21 hadi 26 Januari 1998 ilipania pamoja na mambo mengine: Kuwaimarisha na kuwatia shime watu wateule wa Mungu nchini Cuba katika imani, matumaini na mapendo pamoja na kushiriki katika maisha yao ya kiroho; katika mapambano, furaha na mateso, kusherehekea, kama washiriki wa familia kubwa ya Mungu fumbo la upendo wa kimungu na kuufanya uwepo zaidi katika maisha na historia ya wananchi wa Cuba wenye kiu ya Mungu na maadili ya kiroho. Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Cuba alikuwa ni hujaji wa upendo, ukweli na matumaini, akiwa na shauku ya kunogesha mchakato wa Uinjilishaji mpya kuhusu maisha na utume wa Kristo Yesu ulimwenguni na Mama Kanisa kuendelea kujikita katika huduma makini kwa binadamu. Ujumbe wa Injili anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II unawaongoza watu wa Mungu katika upendo, sadaka, maisha ya kujitoa, dhabihu na msamaha, ili kama mahujaji wawe ni watu wenye matumaini kwa maisha yajayo. Jambo la msingi kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanamfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao, kuyapyaisha tena kadiri ya kweli za Kiinjili, ili waweze kumfuasa Kristo Yesu kwa uaminifu, wapate maana ya maisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Maaskofu wa Cuba wanawashukuru watu wa Mungu wote
Maaskofu wa Cuba wanawashukuru watu wa Mungu wote

Hii ni hija iliyomwezesha Mtakatifu Yohane Paulo II kukutana na kuzungumza na familia na vijana, ambao kimsingi wanapaswa kuwa ni wadau katika mageuzi ya maisha ya kiroho, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi yanayosimikwa katika upendo, ukweli na matumaini kwa watu wa Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni shuhuda wa kinabii, uliogusa undani wa watu wa Mungu, dhamiri nyofu, uhuru wa kuabudu; ujasiri wa kufikiri na kutenda mintarafu mwanga wa Injili. Hija ya kitume ya Mtakatifu Yohane Paulo II iligusia umuhimu wa Cuba kujifunua kwa Jumuiya ya Kimataifa na Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na Cuba kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, vikwazo vya kiuchumi, waathirika wakuu ni watu wa kawaida.

JPII Cuba 25
14 February 2023, 14:17