Jumatano ya Majivu, Mwanzo wa Safari ya Siku 40 za Kipindi cha Kwaresima
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu: “Kujinyima kwa ajili ya Kwaresima, Mchakato wa Kisinodi.” Baba Mtakatifu anatarajia kuzindua maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima, Jumatano ya Majivu, tarehe 22 Februari 2023 kwa kuongoza maandamano ya toba na wongofu wa ndani kutoka katika Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmi kuelekea katika Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina, ambamo, ataongoza Ibada ya Misa Takatifu, Ibada ya Kubariki na Kupakwa Majivu, kuanzia saa 10:30 kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 12:30 kwa Saa za Afrika Mashariki. Makanisa haya yako kwenye Kilima cha Aventine, Jimbo kuu la Roma. Mwanzo huu wa Kipindi cha Kwaresima, tunapenda kumwomba Mwenyezi Mungu apende kulijalia Kanisa lake kujiandaa kikamilifu kiroho, kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, ili jitahada za kufunga, kusali, kutafakari na matendo ya huruma yawasaidie waamini kupata toba na wongofu wa ndani katika maisha yao, hasa ya kiroho.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake wa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2023 linasema, Kwaresima ni kipindi cha kutafakari zaidi mateso ya Kristo aliye kielelezo cha utu wema. Katika Kwaresima ya mwaka 2023 tunaalikwa kutafakari sala ya Mtakatifu Paulo anapoiandikia jumuiya ya Waefeso, ambayo ilikuwa changa kiimani. Ni jumuiya iliyohitaji kuwa na elimu ya Mungu na ya Kanisa (rej. Efe 1:15-18; 3:14-19), iliyohitaji umoja hasa kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi (rej. Efe 2:11-22) na iliyohitaji kutiwa nguvu ili kuweza kushinda kila aina ya udhaifu (rej. Efe 4:17-5:18). Katika sala hii, ''[Mungu] awajalieni kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani" (Efe 3:16), Mt. Paulo anawaombea watu wa Efeso ili Mungu awajalie utu ambao kwa huo Kristo Yesu ataweza kuingia katika mioyo yao.
Jina hili la Jumatano ya majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbano II. Mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”. Majivu yanayotumika siku hii ya Jumatano ya majivu ni ya matawi ya mitende yaliyotumika Jumapili ya Matawi ya mwaka uliopita ambayo yanaashiria ushindi dhidi ya dhambi na mauti kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Majivu ni alama au ishara tu ya nje inayoashiria toba ya ndani ya mioyo yetu kama ilivyo rangi ya kijivu ambayo ni rangi ya toba na matumaini. Kupakwa majivu ni ishara ya toba yetu ya ndani ya nafsi zetu tunayoifanya ambayo inatutakasa na kutusafisha na uovu wote, kama Majivu yanavyotumika kusafisha vyombo. Kumbe kupakwa majivu ni kukubali kwetu kuwa tu wachafu, tu wadhambi, tunahitaji kusafishwa, tunahitaji kutakaswa.
Majivu haya yanapakwa kwenye paji la uso, kama vile siku ya ubatizo tulipopakwa Mafuta ya Krisma Takatifu, tukaondolewa dhambi ya asili na adhabu zake zote, kwa ishara ya msalaba, alama ya ushindi tuliyokombolewa nayo. Kumbe majivu yanatukumbusha kufanya toba na kuungama dhambi tulizotenda baada ya ubatizo. Kupakwa majivu katika paji la uso ni kukiri hadharani bila kujificha kuwa tu wadhambi na tunahitaji huruma ya Mungu Baba, tunahitaji msamaha, tunahitaji kutakaswa na kufanywa upya watoto wa Mungu na wa Kanisa. Asili ya kujipaka majivu kama alama ya toba: Tendo hili la kiroho la kupakwa majivu katika paji la uso ni ishara ya toba ya kweli, ishara ambayo imekuwa ikitumika kwa maelfu ya miaka iliyopita hata kabla ya kuja Kristo. Katika ulimwengu wa wayahudi majivu yalikuwa ni alama ya huzuni, masumbuko, uchungu au uduni (Ayubu 2:8, 30:19; Zab 102:10). Baadaye utamaduni huu wa kupakwa majivu ulitumiwa na wakristo wa kwanza kama alama ya toba. Mwaka 600 hivi, Gregory Mkuu aliifanya siku ya Jumatano ya majivu kuwa siku ya kwanza ya Kwaresma na kufanya kipindi hiki cha toba kuwa ni cha siku arobaini.