Hija ya Papa Francisko DRC:Kitovu cha maisha ya watawa ni Yesu!
Na Angella Rwezaula;- Vatican.
Katika Ziara ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko akiwa Congo DRC katika siku ya tatu tangu afikia tarehe 31 Januari, ambayo ilijaa matukio mengi ya mikutano na hatimaye alikuwa mkutano wa sala katika siku maalum ya ulimwengu. Na hii ni kwamba kila tarehe 2 Februari ya kila mwaka ni Sikukuu ya Kutolewa kwa Bwana Hekaluni, sambamba na Siku ya Watawa Duniani kote ambapo kwa mwaka huu, Papa akiwa katika ziara yake ya 40 ya kitume katika bara la Afrika, katika siku yake ya Pili imekuwa fursa kubwa kukutana na mapadre,mashemasi, watawa wa kike na kiume na waseminari katika Kanisa Kuu la Mama Yetu la Congo huko jijini Kinshasa.
Katika tafakari yake Baada ya kusomwa kwa Injili ambayo ilijikita juu ya kukutana kati ya Simeoni na Mtoto Yesu, Baba Mtakatifu alisema kuwa “Tunapomweka Yesu katikati ya maisha yetu, mtazamo wetu hubadilika, na licha ya juhudi na matatizo yetu yote, lakini tunahisi kufunikwa na nuru Yake, tukifarijiwa na Roho Wake, tukitiwa moyo na Neno lake na kutegemezwa na upendo Wake".
Baba Mtakatifu Francisko aliwakumbusha watawa wote kwamba, licha ya changamoto nyingi, hata hivyo kuna furaha kuu katika huduma ya Injili. Kwa hiyo alioneza kusema kwamba wakleri na wa watawa wameitwa kuwa mashuhuda wa upendo wa Mungu, kwa kuwapaka watu wake leo hii mafuta ya faraja na matumaini.
Baba Mtakatifu Francisko vile vile amesisitiza kuwa mapadre, masista, wamisionari na wengine walioitwa katika huduma ya kidini wanaitwa kuwa watumishi wa watu, kufanya kama ishara za uwepo wa Kristo, upendo wake usio na masharti, upatanisho na msamaha wake na huruma yake kwa ajili ya watu wenye mahitaji na maskini. Lakini huduma hiyo alisema, zitakaa daima katika kukabiliana na changamoto na matatizo, ikiwa ni pamoja na hali ya kiroho, faraja ya kidunia, na ujuu juu.
Hata hivyo Papa pia alisema kuwa "Changamoto hizi zinaweza kutatuliwa, kwa njia ya maombi, hadharani na faraghani; kwa kujisahau na kujitolea maisha yote kwa wengine; na kwa kuwa walioelimika, waliofunzwa vyema, na wenye shauku mashuhuda wa Injili. Changamoto hizi lazima zikabiliwe ikiwa tunataka kuwatumikia watu tukiwa mashuhuda wa upendo wa Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua wazi juu ya matatizo wanayokumbana nayo wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amewakumbusha makleri na watawa juu ya Msamaria Mwema, kusimama kwa ajili ya kuuguza majeraha ya wanyonge. “Kaka na dada huduma ambayo mmeitiwa ndiyo hii hasa, ya kutoa ukaribu na faraja, kama nuru inayoendelea kuangaza katikati ya giza linalozingira”
Hata hivyo Papa kwa kutoa shukrani zake za dhati kwa mapadre, mashemasi, watawa wa kike na kiume na waseminari, aliwahimiza wasivunjike moyo kwa sababu wanahitajika na akaongeza kusema kuwa katika jina la Kanisa zima, wao ni wa thamani na muhimu. Kwa maana hiyo aliwaalika ili daima wawe kama mkondo wa uwepo wa Bwana wenye kufariji, mashuhuda wenye furaha ya Injili, manabii wa amani katikati ya dhoruba za vurugu, wanafunzi wa upendo, walio tayari kutunza majeraha ya maskini na wanaoteseka.