Tafuta

Viongozi wa Kanisa wawe tayari kutoka kimasomaso kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Viongozi wa Kanisa wawe tayari kutoka kimasomaso kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika.   (Vatican Media)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Viongozi wa Kanisa Sudan ya Kusini: Ushuhuda

Papa amegusia matukio muhimu katika maisha ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini, dhana ya maji katika Maandiko Matakatifu; Unyenyekevu na Sala. Viongozi wa Kanisa wajifunze Sanaa ya kutembea kati pamoja na watu wa Mungu, ili kushuhudia ukaribu wa Mungu, wawe tayari kutoka kimasomaso kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi Dominika tarehe 5 Februari 2023 wamekuwa wakitembelea Sudan ya Kusini, kielelezo cha hija ya uekumene wa amani na watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Hija imenogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21. Hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho, haki na amani na ujenzi wa umoja wa Kitaifa, ili hatimaye, mamilioni ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum waweze kurejea tena katika maisha yao ya kawaida, huku wakishiriki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 4 Februari 2023 amekutana na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi kutoka Sudan ya Kusini. Katika hotuba yake amegusia matukio muhimu katika maisha ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini, dhana ya maji katika Maandiko Matakatifu; dhamana ya Musa Mtumishi wa Mungu: Unyenyekevu na Sala kama kielelezo cha wokovu wa waja wake. Viongozi wa Kanisa wajifunze Sanaa ya kutembea kati pamoja na watu wa Mungu, kutangaza na kushuhudia ukaribu wa Mungu kwa waja wake kwa njia ya sala. Viongozi wa Kanisa wawe tayari kutoka kimasomaso kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika.

Viongozi wa Kanisa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili
Viongozi wa Kanisa wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili

Baba Mtakatifu Francisko anasema, moyoni mwake kuna chapa ya matukio muhimu katika maisha na utume wake kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini: Sala kwa ajili ya kuombea amani Sudan ya Kusini iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kunako mwaka 2017, Mafungo ya kiroho kwa ajili ya viongozi wa Sudan ya Kusini yaliyofanyika mwaka 2019 kama sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kutafuta na hatimaye, kuambata mchakato wa amani na udugu wa kibinadamu nchini Sudan ya Kusini kwa kumpokea Kristo Yesu amani na matumaini ya waja wake. Dhana ya maji katika Maandiko Matakatifu inatumika kama kielelezo cha huruma na utakaso wa watu wa Mungu waliotangatanga Jangwani kwa muda wa miaka 40. Maji katika Sakramenti ya Ubatizo yanatakasa na kupyaisha maisha; yanapokea kilio cha watu wanaoteseka, waliovunjika na kupondeka moyo. Dhana ya Maji inawakumbusha waamini mchango wa Musa Mtumishi wa Mungu katika mchakato wa kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri na kuwaongoza Jangwani kwa muda wa miaka 40. Mtumishi wa Mungu Musa ni mfano bora wa kuigwa na viongozi wa Kanisa ambao wanatembea na kuambatana na watu wao katika mapambano dhidi ya: chuki, uhasama na vita; magonjwa na umaskini. Musa katika maisha na utume wake alionesha unyenyekevu wa hali ya juu na kukita maisha yake katika sala.

Viongozi wa Kanisa wawe ni mashuhuda wa ukaribu wa Mungu
Viongozi wa Kanisa wawe ni mashuhuda wa ukaribu wa Mungu

Haya ni mambo muhimu sana kwa viongozi wa Kanisa wanaopaswa kuwa wanyenyekevu na watiifu katika kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao. Utambulisho wao kama watumishi wa Mungu uwasaidie kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu wa Mungu, ili hatimaye, kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za bonadamu. Jangwa na mateso ya moyoni, yaliyosukumwa na dhamiri nyofu yalimwachia Musa mateso makali kiasi cha kukimbia kutoka Jumba la Farao na kukimbilia Midiani, kwani alibaki kuwa mtumwa kwa kutaka kulipiza kisasi! Hii ndiyo “falsafa ya jino kwa jino na matokeo yake wengi wangebaki kuwa vibogoyo.” Huu ni mwaliko na changamoto kwa viongozi wa Kanisa kutafuta suluhu ya matatizo ya watu wao kwa mwanga wa Injili. Kinyume cha mpango huu, viongozi wa Kanisa wanaweza kujikuta wakimezwa na uchu wa mali, fedha na madaraka kwa kudhani kwamba, “fedha ni sabuni ya roho.”. Viongozi wa Kanisa wajifunze kumsogelea Mungu kwa unyenyekevu katika kusoma, kulitafakari na hatimaye kumwilishwa kwa njia ya unyenyekevu, kwani Mwenyezi Mungu ndiye mhusika mkuu wa sera, mbinu na mkakati wa maisha ya mtu binafsi na utume wa Kanisa katika ujumla wake. Watu wa Mungu wajifunze kuwa wanyenyekevu mbele ya Fumbo la Mungu katika maisha na utume wao, ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya wokovu kwa watu wa Mungu.

Viongozi wa Kanisa wajifunze kuishi na kuhudumia kwa unyenyekevu
Viongozi wa Kanisa wajifunze kuishi na kuhudumia kwa unyenyekevu

Ni kwa njia ya unyenyekevu Mwenyezi Mungu anawakirimia nguvu na uwezo wa kuwa ni waombezi wa watoto wa Mungu kwa kutembea na kuambatana na watu wa Mungu kama alivyofanya Musa Mtumishi wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa viongozi wote wa Kanisa kujenga mshikamano na mafungamano na watu wa Mungu. Inasikitisha kuona viongozi wa Kanisa wakiwa wameelemewa na migawanyiko, utengano na kinzani. Kumbe kuna haja ya kujenga na kudumisha ukaribu wa Mungu, ushirikiano, mshikamano na mafungamano na watu wa Mungu. Kama Manabii wa Mungu watende miujiza, kwa kuwaombea watu wao; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki zao msingi. Wafanye yote haya kwa niaba ya Kristo Yesu na Kanisa lake kama anavyoshuhudia Padre Luka katika maisha na utume wake. Viongozi wa Kanisa wakijikita kutafuta fursa na upendeleo, watapoteza dira na mwongozo kwa ajili ya watu wa Mungu. Musa mtumishi wa Mungu kwa muda wa miaka arobaini aliwaongoza Waisraeli jangwani! Hawa ni watu waliokuwa na shingo ngumu, watu waliojikatia tamaa ya maisha; wakachoka kusafiri jangwani, wakashikwa na kiu na njaa ya “kufa mtu”; watu walalamishi na wakati mwingine wavivu. Musa alielemewa sana na uzito wa mahangaiko ya Waisraeli lakini hakukata tamaa, akatangaza na kushuhudia umainifu wa Mungu katika kutekeleza ahadi zake.

Watawa wametoa shuhuda za wenzao waliouwawa nchini Sudan ya Kusini
Watawa wametoa shuhuda za wenzao waliouwawa nchini Sudan ya Kusini

Mungu huyu ni mwingi wa huruma na upendo ndiyo maana, Musa daima alipenda kujitambulisha na Waisraeli waliokuwa amana na utajiri wake, ili awapatie kutoka kwa Mungu: msamaha wa dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu; aweze kuwazamisha katika mchakato wa upatanisho ili waonje na kuzama katika huruma ya Mungu anayewasamehe na kuwatakasa dhambi zao. Viongozi wa Kanisa wanayo dhamana na wajibu wa kuwaombea watu wao na kuendelea kuwa ni Manabii wa Mungu, ili kuwasindikiza, kuwaombea na kushuhudia kwa vitendo Fumbo la ukaribu wa Mungu kwa waja wake, chemchemi ya maisha. Sudan ya Kusini inayo mifano hai ya viongozi wa Kanisa waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, ushuhuda wa mbegu ya imani na matumaini kwa watu wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo kuendeleza utume waliouanzisha katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili, tayari hata kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Viongozi wa Kanisa wajifunze kutoka na kwenda Barani Afrika, huku wakiwa tayari hata kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa tafakari yake, amewapongeza na kuwashukuru kwa: Ujasiri, sadaka na majitoleo yao. Waendelee kuwa ni wachungaji na mashuhuda wakarimu, wanaokita maisha yao katika sala na huduma ya Injili ya upendo, tayari kutumiwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya neema yake, vyombo vya ukombozi; Wachungaji na Manabii wa ukaribu wa Mungu anayewasindikiza na kuwaombea waja wake. Baba Mtakatifu na viongozi wote wa Kanisa katika hali ya ukimya wamewakumbuka na kuwaombea wale wote waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.

Papa Francisko apongezwa kwa kukuza diplomasia ya amani
Papa Francisko apongezwa kwa kukuza diplomasia ya amani

Kwa upande wake, Askofu Yunana Tombe Trille Kuku Andali, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan, katika hotuba yake elekezi kwa Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru kwa kuhakikisha kwamba, Majimbo ya Sudan yanapata wachungaji kwa wakati. Kanisa litaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kufuata mafundisho na mifano ya Kristo Yesu katika maisha, utume na mafundisho yake. Kanisa litaendelea kusimama kidete kulinda na kutunza na kudumisha mazingira bora, nyumba ya wote sanjari na kusimama kidete kulinda haki jamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan linampongeza Baba Mtakatifu kwa kujielekeza zaidi katika diplomasia ya haki na amani katika kutatua migogoro na kizani mbalimbali. Mafundisho yake kuhusu huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ni mfano bora wa kuigwa na Jumuiya ya Mataifa. Kanisa litaendelea kujielekeza katika Injili ya huduma ya upendo. Maaskofu wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa mfano wa maisha na utume wake kwa Kanisa la Kristo!

Viongozi wa Kanisa wawe ni mfabo bora wa kuigwa
Viongozi wa Kanisa wawe ni mfabo bora wa kuigwa

Watawa kwa upande wao, wametoa shuhuda za watawa ambao wamepoteza maisha nchini Sudan ya Kusini kama mashuhuda wa Injili ya upendo na kwamba, damu yao, itakuwa ni mbegu ya mchakato wa upatanisho, haki na amani nchini Sudan ya Kusini. Wakati huo huo Mapadre wamesema, wataendelea kumwimbia Mwenyezi utenzi wa sifa na shukrani kwa wema na ukarimu wake kwa watu wa Sudan ya Kusini, licha ya madhara ya vita, Kanisa bado liko mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kadiri ya uwezo na fursa zilizopo! Changamoto kubwa nchini Sudan ya Kusini ni madhara ya vita, ukabila, matumizi mabaya rasilimali za nchi kwa ajili ya mafao ya watu wachache; ujinga, umaskini na magonjwa; ukosefu wafursa za ajira pamoja na wafanyakazi kupata mishahara ambayo haikidhi mahitaji msingi ya watu wa Mungu. Mbaya zaidi, ni kukosekana kwa utashi wa kisiasa wa kujikita katika mchakato wa upatanisho, haki na amani ya kudumu.

Kanisa Sudan ya Kusini
05 February 2023, 15:19