Tafuta

Viongozi wakuu wa Makanisa Jumamosi tarehe 4 Februari 2023 walikutana na kuzungumza na watu wasiokuwa na makazi maalum nchini Sudan ya Kusini. Viongozi wakuu wa Makanisa Jumamosi tarehe 4 Februari 2023 walikutana na kuzungumza na watu wasiokuwa na makazi maalum nchini Sudan ya Kusini.   (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Sudan ya Kusini: Watu Wasiokuwa na Makazi Maalum

Taarifa ya UNHCR inabainisha kwamba, hadi tarehe 31 Desemba 2022 kulikuwa na watu wasiokuwa na makazi maalum zaidi ya 2,229,657, wakimbizi 308,374 na wale waliokuwa wakiomba hifadhi ya kisiasa ni zaidi ya watu 2,146. Wote hawa ni matokeo ya vita, ghasia, athari za mabadiliko ya tabianchi, kinzani na migogoro ya kikabila. Ni muhimu kujikita katika mchakato wa upatanisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija ya 40 ya Kitume amekuwa akiambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi Dominika tarehe 5 Februari 2023 wamekuwa wakitembelea kwa pamoja Sudan ya Kusini. Huu ni shuhuda wa hija ya uekumene wa amani na matumaini kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Viongozi hawa Jumamosi tarehe 4 Februari 2023 walikutana na kuzungumza na watu wasiokuwa na makazi maalum nchini Sudan ya Kusini. Kadiri ya takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulika na Wakimbizi, UNHCR hadi tarehe 31 Desemba 2022 kulikuwa na watu wasiokuwa na makazi maalum zaidi ya 2,229,657, wakimbizi 308,374 na wale waliokuwa wakiomba hifadhi ya kisiasa ni zaidi ya watu 2,146. Wote hawa ni matokeo ya vita, ghasia, athari za mabadiliko ya tabianchi, kinzani na migogoro ya kikabila.

Watoto wanataka fursa za elimu, afya, michezo na kusali
Watoto wanataka fursa za elimu, afya, michezo na kusali

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, alikazia umuhimu kumaliza vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini na kuanza kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho; kwa kutambua na kuthamini utu, heshima na haki msingi za wasichana na wanawake ambao wana mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Umoja wa Kitaifa na udugu wa kibinadamu ni muhimu kwa mustakabali wa Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wadau wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wasiokuwa na makazi maalum, wakimbizi na wahamiaji pamoja na wale wote wanaotafuta hifadhi ya kisiasa nchini humo. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ambayo iligusa kiini cha hija yake ya kitume nchini Sudan ya Kusini, baada ya kuelezea sababu zinazopelekea watu wengi kuyakimbia makazi na nchi zao, amewataka watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini kujielekeza zaidi katika ujenzi wa haki na amani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuwapatia watu wasiokuwa na makazi maalum fursa ya kuweza kurejea tena katika makazi yao na kuendelea kushiriki katika ujenzi wa nchi yao.

Viongozi wa Makanisa wamekazia mchakato wa haki na amani
Viongozi wa Makanisa wamekazia mchakato wa haki na amani

Kuna haja ya kuwa na amani ya kweli inayowashirikisha watu wote bila ubaguzi. Sudan ya Kusini ni kati ya nchi zenye idadi kubwa ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum Barani Afrika. Matokeo yake kuna idadi kubwa ya watoto wanaopekenywa kwa baa la njaa na utapiamko wa kutisha, lakini licha ya matatizo na changamoto zote hizi, lakini bado wanawake wana matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi. Wanawake ni muhimu sana katika mchakato wa haki, amani na upatanisho sanjari na maendeleo fungamani ya binadamu. Wanawake wanapaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa, kulindwa na kutunzwa kwani hawa ni kielelezo cha matumaini ya Sudan kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwatia shime kuendelea kuwa na matumaini kwa leo na kesho bora zaidi. Ili kuweza kuifikia hali hii, kuna haja ya kujenga na kudumisha mtandao na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, tayari kujikita katika mchakato wa haki, amani, msamaha na maridhiano, tayari kujenga ujirani mwema.

Papa anawataka watu wa Mungu Sudan ya Kusini kuwa na matumaini
Papa anawataka watu wa Mungu Sudan ya Kusini kuwa na matumaini

Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini kuwa ni mbegu ya matumaini, itakayozaa matunda kwa wakati wake kwa kujenga udugu wa kibinadamu kwani wote ni watoto wa Mungu na tofauti zao msingi ni amana na utajiri wa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini katika ujumla wake. Huu ni wakati wa kufungua na kuandika ukurasa mpya wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana katika ukweli na uwazi; kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa udugu na amani; upendo na mshikamano wa kweli ili kuondokana na vita, chuki na uhasama. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wadau wote wanaoendelea kuwasaidia wakimbizi, wahamiaji, watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Sudan ya Kusini ni nchi ambayo ingeweza kujitegemea kwa mambo mengi, lakini kwa wakati huu, msaada wa kiutu unahitajika kutoka kwa Wasamaria wema. Ni vyema misaada ikaelekezwa katika mchakato wa kuwajengea watu wa Mungu uwezo wa kuleta mageuzi ya uzalishaji katika sekta ya kilimo, ili kujitosheleza kwa mahitaji msingi ya chakula. Watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini bado wanahitaji kuonjeshwa umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, wasiachwe peke yao, bado wanahitaji misaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Mwishoni, Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwaalika watu wa Mungu kutoka Sudan ya Kusini wanaoishi nje ya nchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa nchi yao kwa hali na mali.

Viongozi wa Makanisa wamesikiliza shuhuda zao
Viongozi wa Makanisa wamesikiliza shuhuda zao

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na ujumbe wake, wamepata fursa ya kusikiliza shuhuda za watu wanaoishi katika kambi za wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Watoto wamesema wazazi wao hawana fursa za ajira, kumbe wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Wanataka amani na utulivu ili waweze kurejea tena katika makazi yao, wapate nafasi ya kucheza na kwenda shule, kwani mahali ambapo kuna amani, watoto wanaweza kwenda shule na kupata matibabu bora zaidi pamoja na kusali. Mashuhuda wamewashukuru ndugu na jamaa wanaowapatia mahitaji yao msingi pale inapowezekana. Watu wanataka amani ili waweze kujipatia mahitaji yao msingi. Wanaushukuru Umoja wa Mataifa kwa misaada yake ya hali na mali kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Watu wanaendelea kusali ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia amani, ustawi na maendeleo ya kweli. Watu wanataka amani ili kutekeleza ndoto zao, ili kuboresha maisha kwa njia ya elimu na maisha bora zaidi na kuendelea kufurahia maisha ya utoto wao. Watoto wanawataka viongozi wa kisiasa nchini Sudan kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanarejesha amani, upendo na umoja na hivyo kuanza kujielekeza katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wao: kiroho na kimwili.

Watu wanataka haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu
Watu wanataka haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu

Viongozi wa kidini wasiache kusali na kuimbea Sudan ya Kusini ili amani ya kweli iweze kupatikana na hivyo kutawala katika akili na nyoyo za watu. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi zimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Amani ya kudumu ni msaada mkubwa kwa mahangaiko ya watu. Wanamshukuru Baba Mtakatifu pamoja na Makanisa mbalimbali nchini Sudan ya Kusini, mwaliko ni kuendelea kuwafundisha jinsi ya kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii na udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wa Mungu Sudan ya Kusini tangu wajipatie uhuru wao wa bendera wamekuwa wakiteseka kwa vita, kinzani na migogoro ya kikabila, njaa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuna idadi kubwa ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, jambo linalohatarisha pia uhakika na usalama wa chakulal. Hawa ni watu wanaoteseka kwa kukosa elimu na huduma bora za afya; utekaji nyara na vitendo vinavyodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kiasi cha Dola bilioni 1:7 kinahitajika katika kipindi cha mwaka 2023 kwa ajili ya kuwahudumia watu wasiokuwa na makazi maalum. Amani ya kudumu ni jibu kwa changamoto na mahangaiko Sudan ya Kusini. Tangu mwaka 2022 zaidi ya wafanyakazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya kujitolea wameshambuliwa na wengine kupoteza maisha yao. Amani ya kudumu ni jibu muafaka kwa changamoto za kivita.

Papa Watu Wasio na Makazi
07 February 2023, 15:11