Hija ya Kitume ya Papa Francisko Sudan ya Kusini: Uekumene wa Amani na Umoja wa Kitaifa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anasema, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapobaki wanyenyekevu mikononi mwa Mwenyezi Mungu, Yeye huwatengeneza na kuwafanya kuwa ni watu wa upatanisho, wenye uwezo na ambao wako wazi kushiriki katika majadiliano, kwa kuridhiana na kusameheana, ili kufanya mito ya amani iweze kutiririka katika nyanda kame za vurugu na vita. Huu ni ujumbe mahususi kabisa kwa watu wa Mungu nchini DRC, wakati akiwa anahitimisha hija yake ya 40 ya Kitume nchini DRC na kuanza kuelekea nchini Sudan ya Kusini ambako pamoja na mambo mengine, baada ya kuwasili wamepokelewa kwa heshima za kitaifa, wakakutana na kuzungumza na Makamu wawili wa Rais nchini Sudan ya Kusini na Baba Mtakatifu Francisko baadaye kidogo amewahutubia viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na Mashirika ya Kimataifa nchini Sudan ya Kusini. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Jumamosi asubuhi, tarehe 4 Februari 2023 anakutana na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi kutoka nchini Sudan ya Kusini. Mchana, Baba Mtakatifu Francisko anafanya mazungumzo ya faragha na Wayesuit wanaoishi na kufanya utume wao nchini Sudan ya Kusini. Jioni atakutana na kuzungumza na watu wasiokuwa na makazi maalum na hatimaye, kuhitimisha siku kwa Sala ya Kiekumene, itakayowashirikisha viongozi wakuu wa Makanisa.
Dominika, tarehe 5 Februari 2023, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya “John Garang.” Na baada ya hapo, atakuwa anahitimisha hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika, tayari kurejea mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake. Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023 wanatembelea Sudan ya Kusini, kielelezo cha uekumene wa amani na watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Hija inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho na ujenzi wa umoja wa Kitaifa, ili hatimaye, mamilioni ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum waweze kurejea tena katika maisha yao ya kawaida, huku wakishiriki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko anasema hii ni hija ya uekumene wa amani kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Hizi ni jitihada za kutaka kurejesha amani na kuachana na vita, kinzani, migogoro na mipasuko ya kikabila, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja, tofauti zao msingi ni amana na utajiri kwa wote. Akiwa njiani kuelekea Juba, Sudan ya Kusini, Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam na matashi mema Rais Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo wa DRC., akimwonesha shukrani za dhati kabisa kutoka katika sakafu ya moyo wake kwa ajili ya watu wa Mungu nchini DRC, kwa moyo wa ukarimu na upendo waliomwonesha wakati wa hija yake ya kitume nchini mwao. Anaendelea kuwahakikishia uwepo wake wa daima kwa njia ya sala na amewaombea amani, furaha, ustawi na maendeleo. Baba Mtakatifu na msafara wake, alipowasili kwenye anga za Uganda, amemtumia salam na matashi mema Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, akimwambia kwamba, yuko njiani kuelekea nchini Sudan ya Kusini, ili kushiriki hija ya amani ya kiekumene nchini Sudan ya Kusini. Anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Uganda sala, ustawi na maendeleo.