Tafuta

Itakumbukwa kwamba, Sudan ya Kusini ilijipatia uhuru wake wa bendera 9 Julai 2011 lakini tangu wakati huo imetumbukia katika vita, magonjwa, ujinga, umaskini na majanga asilia. Itakumbukwa kwamba, Sudan ya Kusini ilijipatia uhuru wake wa bendera 9 Julai 2011 lakini tangu wakati huo imetumbukia katika vita, magonjwa, ujinga, umaskini na majanga asilia.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Viongozi Nchini Sudan ya Kusini

Papa amegusia: Hija ya uekumene wa amani; rasilimali za nchi ziwe ni kwa ajili ya maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati wa kutambua kwamba, vita inaendelea kusababisha madhara makubwa. Viongozi wawe ni wajenzi wa amani, demokrasia, ili kupyaisha matumaini ya wananchi Sudan ya Kusini. Vijana na wanawake wanao mchango mkubwa kwa mustakabali wa nchi yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya 40 ya Kitume, akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023 wanatembelea Sudan ya Kusini, kielelezo cha hija ya uekumene wa amani na watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Hija inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho, haki na amani pamoja na ujenzi wa umoja wa Kitaifa, ili hatimaye, mamilioni ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum waweze kurejea tena katika maisha yao ya kawaida, huku wakishiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tangu Sudan ya Kusini ijipatie uhuru wake tarehe 11 Julai 2011 imejikuta ikitumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe inayojikita katika ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko. Ni wakati wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa Kitaifa.

Hija ya uekumene wa amani udumishe haki, amani na upatanisho
Hija ya uekumene wa amani udumishe haki, amani na upatanisho

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia na wanadiplomasia baada ya kuwasili nchini Sudan ya Kusini, Ijumaa tarehe 3 Februari 2023 amegusia hija ya uekumene wa amani; amana, utajiri na rasilimali za nchi ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati kwa viongozi kujikita katika maendeleo ya wananchi kwa kutambua kwamba, vita inaendelea kusababisha madhara makubwa. Viongozi wawe ni wahudumu na wajenzi wa amani, demokrasia, ili kupyaisha matumaini ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Vijana na wanawake wanao mchango mkubwa kwa mustakabali wa nchi yao. Ni wakati wa kujizatiti katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, kwa kujielekeza zaidi katika maendeleo fungamano ya binadamu, haki, amani na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu amesema, viongozi wa Makanisa wanafanya hija ya uekumene wa amani ili kulinda, kudumisha na kuendeleza: utu, heshima, haki msingi za binadamu, upatanisho na amani ya kudumu. Mateso, uvulivu na sadaka ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini viwalete amani ya kudumu. Hii ni nchi ambayo imebarikiwa kuwa na amana, utajiri na rasilimali nyingi na baraka ya Mto Nile, kati ya mito mirefu duniani. Utajiri wote huu, usaidie kuboresha Injili ya uhai nchini Sudan ya Kusini. Viongozi wajikite katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, wamechaguliwa na kuteuliwa ili kuwaongoza watu wa Mungu. Ni wakati wa kujizatiti katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano.

Ni wakati wa kupambana dhidi ya rushwa, ukosefu wa haki na amani
Ni wakati wa kupambana dhidi ya rushwa, ukosefu wa haki na amani

Baba Mtakatifu amekazia ujenzi wa amani mintarafu Maandiko Matakatifu kwa kuweka silaha zao chini bila masharti; kwa kuondokana na utamaduni wa kifo na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia, si wakati wa kunyoosheana kidole, bali wote katika ujumla wao waweze kuwajibika, kulinda na kudumisha amani. Wananchi wa Sudan ya Kusini wana kiu ya amani ya kudumu. Sudan ya Kusini ilijipatia uhuru wake wa bendera 9 Julai 2011. Kumbe, viongozi wanayo dhamana na wajibu wa kuwaongoza watu wao huku wakijikita katika huduma ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuanzia na mahitaji msingi na hivyo kuendeleza juhudi za ufufuaji wa uchumi unaosimikwa katika mgawanyo sawa wa rasilimali za nchi na ukuzaji wa demokrasia inayoheshimu na kulinda: utu, heshima na haki msingi za binadamu; Utawala wa sheria pamoja na uhuru wa kujieleza pamoja na kujipatia mahitaji yake msingi. Huu ni wakati uliokubalika wa kujizatiti katika kupyaisha matumaini na hivyo kuondokana na: chuki na uhasama; ukabila na ukanda, kwani wote wameumbwa sawa na ndugu wamoja. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili kujenga utamaduni wa kukutana na watu, kuna haja ya kuheshimiana, kupokeana jinsi walivyo, kufahamiana na hatimaye, kujenga moyo wa udugu wa kibinadamu tayari kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na haki. Vijana na wanawake wanayo dhamana kubwa ya ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana ili kuendeleza Injili ya uhai duniani sanjari na kulinda, utu, heshima na haki msingi za wanawake na wasichana.

Papa Francisko amewakumbuka wamisionari waliouwawa nchini Sudan ya Kusini
Papa Francisko amewakumbuka wamisionari waliouwawa nchini Sudan ya Kusini

Baba Mtakatifu amewagusia pia wamisionari waliokuwa wamejisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, wakakutana na mauti, changamoto na mwaliko wa kudumisha ulinzi na usalama kwa watu wa kujitolea na kwa wafanyakazi wa mashirika ya misaada, ili watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini waendelee kupata huduma. Baba Mtakatifu anawahamasisha watu wa Mungu kujizatiti zaidi katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, ili kudhibiti majanga asilia, hasa kwa ukataji ovyo wa miti ili kujitajirisha. Ni wakati wa kupambana dhidi ya rushwa na ufisadi na hivyo kujikita katika misingi ya ukweli na uwazi. Sudan ya Kusini itoke kimasomaso kupambana na umaskini unaosambabishwa na vita, kinzani, chuki na uhasama na hivyo kusababisha mamilioni ya watu wasiokuwa na makazi maalum kuishi katika mazingira magumu na hatarishi. Ni wakati wa kudhibiti silaha zinazoingia nchini Sudan ya Kusini kutokana na biashara haramu ya silaha duniani inayoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo.

Watu wana matumaini katika hija ya uekumene wa amani
Watu wana matumaini katika hija ya uekumene wa amani

Serikali ijikite zaidi katika maboresho ya huduma ya elimu, afya na maendeleo fungamani ya binadamu, urithi mkubwa kwa watoto na vijana wa kizazi kipya. Watoto wapewe fursa ya kwenda shule na wala si kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha mapigano. Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza na kuwashukuru wadau wote ambao wameendelea kusimama kidete katika mchakato wa upatanisho na maendeleo nchini Sudan ya Kusini, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati ili kukidhi mahitaji msingi ya watu mahalia kama alivyo wahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II yaani: suluhu ya matatizo na changamoto za Kiafrika hazina budi kupata ufumbuzi wake kutoka ndani ya Bara la Afrika. Baba Mtakatifu Francisko na viongozi wenzake kama mahujaji wa uekumene wa amani amehitimisha hotuba yake kwa kuwataka watu wa Mungu Sudan ya Kusini kuondokana na mafuriko ya vita na kinzani; rushwa, ufisadi na umaskini.

Papa Hotuba Viongozi

 

04 February 2023, 17:08