Hija ya Kitume ya Papa Francisko Sudan ya Kusini: Hotuba ya Dr Ian Greenshield
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo anapenda kujikita zaidi katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaokita mizizi yake katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kulinda, kudumisha na kuendeleza misingi ya haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Hii ni sehemu ya mchakato wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya 40 ya Kitume akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023 wanatembelea Sudan ya Kusini, kielelezo cha hija ya uekumene wa amani na watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Hija inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21.
Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland katika hotuba aliyotoa Ijumaa tarehe 3 Februari 2023 kwa viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa nchini Sudan ya Kusini amejielekeza zaidi ujenzi wa Sudan ya Kusini unaosimikwa katika umoja wa Kitaifa; viongozi wanaothamini tunu msingi za Maisha katika ujenzi wa upatanisho, amani na maendeleo tayari kutekeleza mpango wa Mungu katika Maisha ya wananchi wa Sudan ya Kusini. Amesema, katika hali ya unyenyekevu, umoja na upendo kama viongozi wa Makanisa wako mbele yao kuwatia shime watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini, ili waweze kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Heri za Mlimani ni Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Rej. Mt 59-12. Mheshimiwa Dr Iain Greenshields anakaza kusema, ujenzi huu wa amani ni shirikishi na unawakirimia watu wote amani.
Hii ni amani inayokita mizizi yake katika familia, makabila na mataifa yote ya dunia. Ulimwengu una kiu ya amani na kuna haja ya kuwa na viongozi wanaojali na kuheshimu: hali na tunu msingi za maisha ya watu wao, huku wakijitahidi kuboresha maisha ya watu wao, mambo msingi katika ujenzi wa amani ya kudumu. Umoja na mafungamano ya kijamii ni muhimu ili kuwawezesha watu wote wa Mungu kuishi utimilifu wa amani, kumbe, viongozi wa Sudan ya Kusini hawana budi kujielekeza katika mchakato wa ujenzi wa amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopania kuleta mabadiliko katika maisha ya watu. “Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.” Isa 65: 21-22. Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland amehitimisha hotuba yake kwa kuwataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia kumwilisha ujumbe huu wa matumaini kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini.