Tafuta

Watu wa Mungu Sudan ya Kusini wawe ni nuru ya ukarimu, na sadaka kwa ajili ya matumaini na ujenzi wa jamii iliyojipatanisha, kwa ajili ya leo na kesho yenye matumaini. Watu wa Mungu Sudan ya Kusini wawe ni nuru ya ukarimu, na sadaka kwa ajili ya matumaini na ujenzi wa jamii iliyojipatanisha, kwa ajili ya leo na kesho yenye matumaini.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko Mahubiri Ibada ya Misa Takatifu: Injili ya Amani na Matumaini Sudan ya Kusini

Muhimu: Injili ya matumaini inayofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Waamini ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, mwaliko wa kuwa ni mashuhuda wa tunu hizi ili watu waweze kuangaziwa: Amani, upendo wa Mungu, matumaini na hivyo kuendelea kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho; Ushuhuda wa Mungu ambaye ni chemchemi ya amani na faraja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi Dominika tarehe 5 Februari 2023 amekuwa akifanya Hija ya Kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini. Lengo ni kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu, Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; amani na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika nchi hizi mbili ambazo kwa hakika zimepekenywa sana kwa: vita, umaskini, magonjwa na ujinga. Baba Mtakatifu Francisko katika hija ya 40 ya Kitume amekuwa akiambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala, kuanzia Ijumaa tarehe 3 Februari hadi Dominika tarehe 5 Februari 2023 wamekuwa wakitembelea kwa pamoja Sudan ya Kusini. Huu ni shuhuda wa hija ya uekumene wa amani na matumaini kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 5 Februari 2023 amehitimisha hija ya uekumene wa amani na matumani nchini Sudan ya Kusini kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya “John Garang.”

Watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini wawe ni chumvi na nuru ya Mataifa
Watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini wawe ni chumvi na nuru ya Mataifa

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia kuhusu Injili ya matumaini inayofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Amewakumbusha waamini kwamba wao ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda wa tunu hizi katika maisha na utume nchini Sudan ya Kusini, ili watu waweze kuangaziwa na: amani, wema na upendo wa Mungu, matumaini na hivyo kuendelea kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho; Ushuhuda wa Mungu ambaye ni chemchemi ya amani na faraja. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amechambua kwa kina na mapana hekima ya Mungu ambayo imehubiriwa na Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa kuhusu Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha imani ya Kikristo na kwamba, yuko kati ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini kuwatangazia, kuwashuhudia na hatimaye, kuwaimarisha katika Injili ya matumaini, ili waweze hatimaye, kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Wageuze hali ya masikitiko katika matumaini na malalamiko yote katika furaha na kicheko. Watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini watambue kwamba, wao ni chumvi ya dunia, alama ya hekima na busara na Kristo Yesu ametumia Heri za Mlimani kuwa ni dira, mwongozo na katiba inayokoleza ladha ya utakatifu wa maisha, kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu, katika hali ya unyenyekevu, upole na huruma.

Heri za Mlimani zimwilishwe katika upole na unyenyekevu wa moyo
Heri za Mlimani zimwilishwe katika upole na unyenyekevu wa moyo

Heri za Mlimani zinapaswa kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha ya Kikristo na mahali wanapoishi. Chumvi katika mapokeo ya kale ilitumika kwa ajili ya kuhifadhia chakula na katika Maandiko Matakatifu chumvi ilitumika kutengeneza mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, huku akiendelea kuwa mwaminifu kwa ahadi zake. Hii ni changamoto kwa wafuasi wa Kristo Yesu kuwa waamini kwa Agano lao na kwamba, Mwenyezi Mungu atabaki kuwa mwaminifu, hata kama binadamu atayumba na kukengeuka. Wakristo wanahimizwa kuwa ni mashuhuda wa Agano na Mungu kwa furaha, moyo wa ushukrani na maisha ya kidugu; kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano mema ya kirafiki ili kupambana na rushwa na ufisadi, vita, chuki, uhasama, utengano, biashara za kidanganyifu pamoja na mambo yote yanayosababisha ukosefu wa haki ndani ya jamii. Baba Mtakatifu anawalika waamini nchini Sudan ya Kusini kuwa ni chumvi ya dunia tayari kuganga na kuponya sumu ya chuki na uhasama, ukosefu wa haki msingi za binadamu; umaskini wa hali na kipato. Hata katika udogo na uchache wao wajitahidi kunogesha Injili ya matumaini, licha ya vita, kinzani na migawanyiko kuonekana kana kwamba ni nguvu zinazopita uwezo wao, lakini kama Wakristo wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa nchi yao kama historia inavyo onesha.

Wakristo wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya S. Sudan.
Wakristo wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya S. Sudan.

Huu ni wakati uliokubalika wa kuweka chini silaha, kuachana na tabia ya kutaka kulipiza kisasi, ili kuzama zaidi katika sala na matendo ya huruma; kielelezo cha imani tendaji. Ni wakati wa kuondokana na ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko na badala yake, wazame zaidi katika mchakato wa msamaha, upatanisho na uponyaji; kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kuonesha upendo kwa jirani na kuendelea kuboresha mema na mazuri ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha na wajitahidi wasitumbukie katika ubaya wa moyo. Baba Mtakatifu Francisko amewaambia watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini kwamba, wanapaswa kuwa nuru ya Mataifa kama utabiri huu kutoka kwa Nabii Isaya unavyotimia katika maisha na utume wa Kristo Yesu, aliyetumwa na Baba wa milele kuwa ni Nuru ya Ulimwengu, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Kristo Yesu, hata waamini katika ulimwengu mamboleo wanaitwa na kutumwa kuwa ni nuru angavu ya Mungu kwa watu wa Mataifa na mashuhuda wa matendo makuu ya Mungu katika maisha yao na kamwe wasielemewe na giza la maisha! Waamini wawe ni nuru ya matumaini katika medani mbalimbali za maisha. Wakimtumainia Kristo Yesu atawakirimia nguvu na uwezo wa kutekeleza dhamana na nyajibu zao mbalimbali kwa ari na moyo mkuu na furaha ili kumtukuza Mwenyezi Mungu.

Ni wakati wa kutangaza Injili ya amani na matumaini
Ni wakati wa kutangaza Injili ya amani na matumaini

Kama watoto wa Baba wa milele, waamini wanatakiwa kuwaka moto wa mapendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Sudan ya Kusini ni nchi nzuri na yenye rasilimali na utajiri mkubwa, lakini imeharibiwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; kumbe, kunahitajika sasa mwanga angavu ili kuondokana na matendo yote haya yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, nchi ya Sudan ya Kusini itakuwa ni nuru angavu inayojikita katika ushuhuda wa Injili ya udugu wa kibinadamu. Wawe ni nuru ya ukarimu, na sadaka kwa ajili ya matumaini na ujenzi wa jamii iliyojipatanisha, kwa ajili ya leo na kesho yenye matumaini. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewahakikishia watu wa Mungu Sudan ya Kusini kwamba, daima ataendelea kuwa pamoja nao katika sala, ili waweze kupata uzoefu wa furaha na mwanga wa Mungu wa amani na faraja katika maisha yao.

Papa Ibada ya Misa
05 February 2023, 16:59