Hija ya Kitume ya Papa Francisko DRC: Ibada ya Misa Takatifu: Kuombea Haki na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya 40 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu Jumatano tarehe 1 Februari 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Ndege wa Ndolo, ili kuombea haki na amani nchini DRC. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Kila mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu. Hii ni haki ya kuishi na kuwa na maisha na haki za tunu za kimaadili na kiutamaduni. Hizi ni nguzo kuu zinazosimika mchakato wa amani ya kweli, mahusiano na mafungamano ya watu wa Mungu katika ujumla wao wanaounda jumuiya ya Kisiasa. Amani katika ukweli inafumbatwa katika mchakato wa kuheshimu utu na haki msingi za binadamu; kutafuta na kuuambata ukweli; uhuru wa kujieleza pamoja na uwepo wa mazingira bora ya kila mtu kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amekazia pamoja na mambo mengine: amani ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, baada ya kukumbana uso kwa uso na Kashfa ya Msalaba. Kristo Yesu ni chemchemi ya amani, msamaha wa moyo; hii ni chemchemi ya ujenzi wa jumuiya inayosimikwa katika udugu. Amani ni chemchemi ya utume unaowataka kuwa ni wamisionari wa amani duniani.
Baba Mtakatifu Francisko ameonesha furaha yake ya ndani kwa kukutana na kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya DRC. Imekuwa ni fursa ya kutafakari tena amani kutoka kwa Kristo Yesu Mfufuka kwa wafuasi wake baada ya kufufuka kwa wafu. Ni amani iliyotangazwa na Malaika kule mjini Bethlehemu, amani inayotolewa kwa waamini wakati wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kwa Fumbo la Msalaba, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, ameshinda mauti, dhambi na kifo na hivyo kuwapatanisha wanadamu na Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, mwanadamu aweze kukumbatia na kuambata maisha na matumaini, baada ya kukutana uso kwa uso na Kashfa ya Fumbo la Msalaba. Mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, wanafunzi wengi walimkimbia na kumwacha peke yake, kumbe, ndani mwao kukabaki dhamiri nyofu iliyokuwa ikiwasuta kwa kumkimbia Kristo Yesu wakati wa mateso, kiasi hata cha kuchanganyikiwa, kuhuzunika na kuwa na huzuni moyoni. Kristo Yesu anawatangazia na kuwakirimia amani na maisha mapya, lakini Mitume bado wamelala “usingizi mzito makaburini kwa sababu bado wanahisi kifo mwilini mwao.” Hii ni amani inayochipusha na kupyaisha matumaini mapya, kiasi hata cha kuwashangaza wafuasi wake, ambao walidhani kwamba, kila kitu kimekwisha. Hii inaonesha kwamba, kifo hakina sauti ya mwisho na kwamba, Kristo Yesu ni amani ya watu wake, na wala hawana sababu msingi ya kukata wala kujikatia tamaa hata kwa sababu ya: vita na ghasia.
Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, wanaitwa na kutumwa kutangaza amani ya kinabii inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya amani, msamaha wa moyo; maisha ya kijumuiya yanayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, kwa kutambua kwamba, wanaitwa na kutumwa kuwa ni wamisionari wa amani duniani. Msamaha wa Kristo Yesu unabubujika kutoka katika Madonda yake Matakatifu, yanayowakirimia waamini msamaha na maondoleo ya dhambi. Dhambi na udhaifu wa maisha ya mwanadamu inageuzwa kuwa ni chemchemi ya msamaha na maisha yanakuwa ni chemchemi ya amani, upendo na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kukimbilia na kujipatia hifadhi katika Madona Matakatifu ya Kristo Yesu, chemchemi ya msamaha na upendo usiokuwa na kifani. Watu wa Mungu watambue kwamba, Kristo Yesu anafahamu madonda ya nchi na watu wao yanayoendelea kuvuja damu kutokana na chuki na uhasama, kiasi cha kuonekana kana kwamba, dawa ya haki na matumaini inakawia kuwafikia. Lakini watambue kwamba, Kristo Yesu anateseka pamoja nao na anatamani kuwafariji, kuwaponya, kuwaongoza na kuwarejeshea tena faraja zake, wale wanaomlilia. Rej Isa 57:18. Kristo Yesu anataka kuganya na kuponya majeraha ya moyo, mwaliko kwa waamini ni kupokea wito huu na kuufanyia kazi, kwa kuweka chini silaha na kuanza kukumbatia msamaha unaobubujika kutoka katika Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu.
Ni wakati wa kuachana na yale mambo ya kale, ili kumpatia Kristo Yesu nafasi ya kuwakirimia amani, na wao wenyewe kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani ya Kristo. Kristo Yesu ni chemchemi ya amani inayojenga jumuiya ya waamini inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, ili kufyekelea mbali hatari ya kumezwa na malimwengu. Mitume wa Yesu walikuwa wamehifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, lakini Kristo Yesu alipowavuvia na kuwaambia “Pokeeni Roho Mtakatifu” wakapata mwelekeo mpya wa maisha unaosimikwa katika ushirika ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kiasi hata cha kujisadaka maisha yao kwa ajili ya furaha ya Injili ya matumaini kwa jirani zao. Baba Mtakatifu amewaonya watu wa Mungu nchini DRC kuondokana na imani za kishirikina, chuki, uhasama, magomvi na utengano. Waamini wajikite katika fadhila ya unyenyekevu, toba na utakatifu wa maisha; kwa kushikamana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kuwafungulia wengine nyoyo zao. Kimsingi anasema Baba Mtakatifu Francisko, Jumuiya ya waamini kwa msaada wa Mungu inapaswa kulijenga Kanisa kwa kutumia amana na utajiri wake kwa ajili ya kukuza upendo wa kidugu, unaowawezesha kuwa ni wamisionari wa amani wanaotumwa kutangaza na hata kutoa maisha yao kwa ajili ya kuwafunulia watu huruma na upendo wa Mungu kwa watu wote.
Wamisionari wa amani wanahimizwa kushirikiana na kushikamana na watu wote, kama mashuhuda wa upendo mintarafu tunu msingi za Kiinjili yaani: Udugu wa kibinadamu, upendo na msamaha kwa kutafuta na kuambata upendo wa dhati kutoka kwa Mwenyezi. Hata leo hii, Kristo Yesu anaendelea kusema, amani kwenu. Hii ni amani kwa watu wote, changamoto ni kuchagua kuwa ni wamisionari wa msamaha, wadau wa ujenzi wa jumuiya yenye utume wa kutangaza amani duniani. Wakati huo huo, Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, OFM Cap. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwatembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, alama na ushuhuda wa upendo kwa watu wa Mungu, nchi yao ya DRC na utamaduni wao, lakini zaidi kwa uwepo wake wa karibu kiroho. Watu wa Mungu nchini DRC wanamshukuru kwa kuwatembelea, kuwaimarisha na kuwafariji, kielelezo makini cha ushirika na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi ni chemchemi ya baraka na wakfu kwa Kristo Yesu, atakayewakirimia watu wa Mungu nchini DRC amani ya kudumu kwa wakati wake. Kwa hakika hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC imekuwa ni chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu. Mwishoni, watu wa Mungu nchini DRC wamemweka Baba Mtakatifu Francisko chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama Yetu wa DRC.