Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 10 Januari 2023 amekutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni pamoja na ujumbe wake. Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 10 Januari 2023 amekutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni pamoja na ujumbe wake.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni Akutana na Papa Francisko

Viongozi wamejikita katika masuala yanayohusu ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hususan mapambano dhidi ya ongezeko la kiwango cha umaskini nchini Italia, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na changamoto zake; idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa nchini Italia pamoja na umuhimu wa kuendelea kujikita katika mchakato wa malezi na makuzi ya vijana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumanne, tarehe 10 Januari 2023 amekutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni pamoja na ujumbe wake, ambaye, baadaye amepata bahati pia ya kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu na Waziri mkuu wa Italia katika mazungumzo yao, wameridhishwa na uhusiano mwema wa kidiplomasia kati ya Italia na Vatican. Baadaye, wameendelea kujikita katika masuala yanayohusu ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Italia, hususan mapambano dhidi ya ongezeko la kiwango cha umaskini nchini Italia, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na changamoto zake; idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa nchini Italia pamoja na umuhimu wa kuendelea kujikita katika mchakato wa malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya.

Waziri mkuu wa Italia alikutana pia na viongozi wakuu wa Vatican
Waziri mkuu wa Italia alikutana pia na viongozi wakuu wa Vatican

Baba Mtakatifu Francisko na Waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni, baadaye wamejielekeza zaidi katika masuala ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU hususan kuhusu vita kati ya Ukraine na Urusi. Itakumbukwa kwamba Giorgia Meloni, Waziri mkuu mpya wa Italia, Dominika tarehe 23 Oktoba 2022 alianza kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Waziri mkuu wa Italia, baada ya chama chake cha siasa “Fratelli d'Italia” kilichoanzishwa kunako mwaka 2012 na Mheshimiwa: Ignazio La Russa, Guido Crosetto na Giorgia Meloni, ambaye amekuwa Rais wa chama hiki tangu mwaka 2014 kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni nchini Italia. Giorgia Meloni alizaliwa tarehe 15 Januari 1977 mjini Roma na alianza harakati za kisiasa kunako mwaka 1996. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 23 Oktoba 2022, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea umoja wa Kitaifa na amani nchini Italia.

Umaskini, malezi na majiundo makini ya vijana ni muhimu
Umaskini, malezi na majiundo makini ya vijana ni muhimu

Kwa upande wake, Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika salam na matashi mema kwa Giorgia Meloni, Waziri mkuu mpya wa Italia, amemtakia pongezi za dhati anapoufungua ukurasa mpya wa historia ya uongozi wa Italia, kwa mara ya kwanza kuongozwa na mwanamke katika nafasi ya Waziri mkuu. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kabla ya mchakato wa uchaguzi mkuu, lilibainisha vipaumbele kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Italia, kwa kuwakumbusha wanasiasa kuhusu wajibu wao kwa watu wa Mungu nchini Italia mintarafu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.” Huu ni udugu unaopaswa kumwilishwa katika matendo kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni udugu unaofumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Baba Mtakatifu anapenda pia kukazia msamaha na upatanisho wa kweli; kumbukumbu hai pamoja na haki. Kila mtu anao wajibu na haki ya kulinda utu na heshima yake, kwa sababu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu sanjari na kukazia mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa ajili ya mafungamano ya kijamii, ustawi na mafao ya wengi.

Papa alikutana na kuzungumza na ujumbe wa Waziri mkuu wa Italia
Papa alikutana na kuzungumza na ujumbe wa Waziri mkuu wa Italia

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI linasema, kati ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele kwa sasa na Serikali ya Italia ni pamoja na mapambano dhidi ya baa la umaskini wa hali na kipato; idadi ndogo ya watoto watoto wanaozaliwa; ulinzi na usalama wa wazee; ukosefu wa usawa wa maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Italia. Maaskofu wanazungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi na kiikolojia; changamoto ya kupanda kwa gharama ya nishati; ukosefu wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya na umuhimu wa kuondoa ukiritimba na kuboresha huduma zinazotolewa na Serikali ya Italia katika ngazi mbalimbali. Wananchi wa Italia wanapenda kuona mabadiliko katika masuala sheria ya uchaguzi. Changamoto kubwa kwa sasa inayotishia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni Vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine, ambayo imepelekea kupanda kwa gharama ya maisha na kushuka kwa hali ya maisha. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kujikita katika mchakato wa kusitisha vita, ili hatimaye, kupata amani ya kudumu. Kanisa Katoliki nchini Italia, linamtakia heri na baraka Waziri mkuu Giorgia Meloni na Serikali yake na kwamba, Kanisa daima lipo kuendeleza mchakato wa majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa limetia nia ya kuchangia kutafuta mafao ya wengi; ulinzi, usalama pamoja na kudumisha misingi ya haki na amani kwa watu wote wa Mungu. Kati ya Mawaziri 24 wanaounda Serikali ya Waziri mkuu Giorgia Meloni kati yao kuna wanawake 6.

Waziri mkuu wa Italia
12 January 2023, 12:30