Vipaumbele vya Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katika Ujumla Wake: Utu wa Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Diplomasia ya Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, inatoa kipaumbele cha pekee kwa uhuru wa kidini, utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Vatican katika medani mbalimbali za Kimataifa. Kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu ni hatua muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu, kwani mizizi ya haki za binadamu inafumbatwa katika hadhi, heshima na utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hizi ni haki za wote zisizoweza kukiukwa wala kutenguliwa. Ni za binadamu wote bila kujali: wakati, mahali au mhusika. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Haki ya kwanza kabisa ni uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi pale anapofariki dunia kadiri ya mpango wa Mungu. Mkazo umewekwa katika haki ya uhuru wa kidini inayofafanuliwa katika uhuru wa kuabudu. Hiki ni kiini cha haki msingi kinachofumbata haki nyingine zote. Kuheshimu na kuthamini haki hii ni alama ya maendeleo halisi ya binadamu katika medani mbalimbali za maisha. Haki inakwenda sanjari na wajibu!
Mama Kanisa anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuheshimu haki msingi za binadamu, kichocheo muhimu sana cha amani na utulivu miongoni mwa binadamu. Kanisa linapenda kusimama kidete: kulinda na kudumisha haki na amani sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya mwanga na chachu ya tunu msingi za Kiinjili! Hii ni amani inayofumbatwa katika: ukweli, haki, mshikamano na uhuru wa kweli. Uhuru wa kidini ni sehemu muhimu sana ya Tamko la Haki Msingi za Binadamu lililopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1948. Mwamini anapaswa kukiri na kushuhudia imani yake inayomwilishwa katika matendo. Uhuru wa kidini ni kati ya mambo ambayo hayapewi tena kipaumbele cha pekee katika vyombo vya utekelezaji wa sheria na hata wakati mwingine kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kuna haja ya kuwajulisha walimwengu kwamba, kuna nyanyaso na dhuluma za kidini zinazoendelea kutendeka sehemu mbalimbali za dunia, kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko Jumatatu, tarehe 9 Januari 2023 amekutana na kuzungumza na wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kama sehemu ya mapokeo na utaratibu wa kutakiana heri na baraka kwa mwaka mpya wa 2023. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Msiba mkubwa wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, wajibu wa kidiplomasia, Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia, Kumbukizi ya Miaka 60 ya Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa tarehe 11 Aprili 1963, Hija ya Kitume nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 3 Februari 2023 na Sudan ya Kusini ni kuanzia tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023. Amani duniani inapaswa kusimikwa katika: ukweli, haki, mshikamano na uhuru wa kweli.
Kwa upande wake, Balozi Georgios F. Poulides, Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican yapatayo 183 kutoka Cyprus katika hotuba kwa Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya salam na matashi mema kwa Mwaka mpya wa 2023 amewasilisha salam rambirambi kwa Baba Mtakatifu Francisko kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Benedikto XVI kilichotokea tarehe 31 Desemba 2022 na kuzikwa tarehe 5 Januari 2023. Madhara makubwa ya UVIKO-19, Sala ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili tarehe 8 Desemba 2022; umuhimu wa kutafuta na kudumisha amani duniani pamoja na changamoto zake; Hija za Kitume zilizofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2022 huko Malta na Canada pamoja na umuhimu wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni pamoja na matashi mema kwa Baba Mtakatifu katika hija yake ya kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini.
Itakumbukwa kwamba, kuna nchi 183 zenye uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Pia kuna Mashirika ya Kimataifa kama: Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU inayoundwa na nchi 27, Chama Cha Kitume Cha Kijeshi cha Malta “Sovrano Militare Ordine di Malta” ambayo kwa pamoja yanafikisha idadi ya Mashirika 91. Umoja wa Falme za Kiarabu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (United Nations High Commission for Refugees, UNHCR) na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji “International Organization For Migration (IOM) yana makazi yao mjini Roma. Hatimaye, tarehe 4 Oktoba 2022, Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris wa mwaka 2015 umeanza kutekelezwa mjini Vatican. Makubaliano kati ya Vatican na Kazakhstan ya 24 September 1998 yameboreshwa zaidi mintarafu hati za kuingia nchini humo zinazotolewa kwa viongozi wa Kanisa na watawa kutoka nchi za nje.