Tafuta

Wazazi na wasimamizi wa Ubatizo, wawe ni dira na mwongozo kwa watoto hawa waliozaliwa kwa Sakramenti ya Ubatizo. Wazazi na wasimamizi wa Ubatizo, wawe ni dira na mwongozo kwa watoto hawa waliozaliwa kwa Sakramenti ya Ubatizo.  

Ubatizo wa Watoto Wachanga: Wajibu wa Wazazi na Wasimamizi wa Ubatizo

Baba Mtakatifu Francisko katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Dominika tarehe 8 Januari 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Sistina na kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga 13. Katika mahubiri yake, amewapongeza wazazi na walezi kuwaleta watoto wao ili waweze kubatizwa na hivyo kuzaliwa upya katika maisha ya Kikristo: Sala na Ushuhuda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa Kristo Yesu kukubali kubatizwa Mtoni Yordani anafunua kwamba haki ya kweli ya Mungu ni huruma inayookoa, upendo unaoshiriki hali ya kibinadamu na ulio katika mshikamano na mateso ya binadamu katika giza lao ili kuwarudisha tena kwenye nuru angavu! Baba Mtakatifu Francisko katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Dominika tarehe 8 Januari 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Sistina na kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga 13. Katika mahubiri yake, amewapongeza wazazi na walezi kuwaleta watoto wao ili waweze kubatizwa na hivyo kuzaliwa upya katika maisha ya Kikristo. Iwe ni nafasi ya kukumbuka tarehe hii ya Ubatizo na kuiadhimisha kila mwaka kama siku ya kuzaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu. Wazazi na wasimamizi wa Ubatizo, wawe ni dira na mwongozo kwa watoto hawa waliozaliwa kwa Sakramenti ya Ubatizo. Wawe ni walimu na makatekista wa kwanza kwa sala ili iweze kuwa ni ngao madhubuti wakati wa raha na shida. Wazazi na walezi wawafunze watoto wao kusali Rozari, Bikira Maria aweze kuwasindikiza katika hija ya maisha yao hapa duniani, watambue kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa na kwamba, yuko karibu sana na Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Watoto waliobatizwa leo wameanza sherehe kubwa ya safari na maisha ya Kikristo, changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanawasindikiza watoto wao kwa sala na ushuhuda wa maisha.

Watoto wachanga wamezaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu
Watoto wachanga wamezaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu

Mama Kanisa ametumia fursa hii, kuwakumbuka na kuwaombea watoto wote waliobatizwa katika Kipindi cha Noeli, ili wauvae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu, katika haki na utakatifu wa kweli. Amewaombea viongozi mbalimbali ili wawe ni vyombo na wajenzi wa amani duniani. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuwakirimia watoto wote amani na utulivu; afya na hekima. Awaongoe wakatili na wadhambi. Mwenyezi Mungu awafariji watoto wanaoteseka na wale wote walioko kufani! Sakramenti ya Ubatizo ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika Roho “vitae spiritualis ianua” na kwa njia hii, mwamini anaweza kupata Sakramenti nyingine zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanafanywa huru toka dhambi na wanazaliwa upya kama watoto wa Mungu, viungo vya Kristo Yesu, wanaingizwa katika Kanisa na kufanywa washiriki katika utume wa Kristo. Kimsingi Mababa wa Kanisa wanasema, Ubatizo ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji na katika neno. Ni kutokana na umuhimu huu, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini kuhakikisha kwamba, wanaadhimisha kwa ari na moyo mkuu Sikukuu ya Ubatizo wao, alama ya kufa na kufufuka na Kristo Yesu, kwa njia ya Maji ya Ubatizo na Roho Mtakatifu na hivyo kuwa ni viumbe wapya, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, sanjari na ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. 

Wazazi na wasimamizi wa Ubatizo watekeleze vyema wajibu wao
Wazazi na wasimamizi wa Ubatizo watekeleze vyema wajibu wao

Sakramenti ya Ubatizo inachota utajiri wake kutoka katika Fumbo la Pasaka. Hii ni Sakramenti ya imani inayomwezesha mwamini kuingia katika maisha ya kiimani, kwa kuwekwa huru dhidi ya mitego ya Shetani. Kuhusu Ubatizo wa Watoto wachanga, Kanisa linapania kuwasaidia watoto hawa kuzaliwa upya kwa “Maji na Roho Mtakatifu” ili kuwaweka huru dhidi ya nguvu za giza na hatimaye, kuingizwa katika utawala wa uhuru wa watoto wa Mungu. Kutokana na utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, malezi na makuzi ya watoto na vijana yamekuwa ni changamoto kubwa kwa wazazi na walezi wengi. Kuna watoto wengi hawana tena fursa ya kupokea Sakramenti za Kanisa kutokana na shule wanakosoma na kuishi. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Barani Afrika wanasema kutokana na huruma na neema ya Mwenyezi Mungu, hakuna mtoto anayepaswa kunyimwa Sakramenti ya Ubatizo, kwani ni sehemu ya utekelezaji wa Agizo la Kristo Yesu aliyesema “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” Mt. 28:19. Rej Mk. 16:15-16.

Mama JKanisa amesali pia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto
Mama JKanisa amesali pia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto

Hii ni sehemu ya utume wa Kanisa na mlango wa wokovu kwa watoto wa Mungu, ambao hata kama hawawezi kukiri imani kwa vinywa vyao wenyewe, lakini wazazi na wasimamizi wao, wanakiri imani ya Kanisa kwa niaba yao. Ni kwa njia hii, watoto hawa wanapata neema na uhuru wao unakuzwa na kudumishwa. Wazazi na walezi wajitahidi kuwa ni mashuhuda wa imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kutambua kwamba, Sakramenti ya Ubatizo ni muhimu kwa wokovu wa mtu binafsi na ni njia ya huruma na upendo wa Mungu unaomwokoa mwanadamu kutoka katika dhambi ya asili na hivyo kuwashirikisha watoto maisha ya uzima wa Kimungu. Kumbe, ushiriki mkamilifu wa wazazi na walezi ni muhimu sana kwa Ubatizo wa watoto wachanga. Maandalizi ya kina yanapaswa kufanyika ili wazazi na walezi watambue tangu mwanzo dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya watoto wao. Jumuiya ya waamini inahamasishwa kushiriki kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto katika imani. Haya ni baadhi ya mambo muhimu yaliyopewa uzito wa pekee na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kuhusu Mwongozo wa Ubatizo kwa Watoto Wachanga wa tarehe 20 Oktoba 1980 ujulikanao kama “Sacred Congregation for the Doctrine of the Faith. INSTRUCTION ON INFANT BAPTISM. Pastoralis action.”

Ubatizo ni alama ya kufa na kufufuka na Kristo Yesu
Ubatizo ni alama ya kufa na kufufuka na Kristo Yesu

Katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, kumekuwepo na Mapokeo ya kuwabatiza watoto wachanga kwenye Kikanisa cha Sistina kilichoko mjini Vatican. Ikumbukwe kwamba, imani ni kipaji cha bure kinachotolewa na Mwenyezi Mungu, hali inayodhihirishwa kwa namna ya pekee, katika ubatizo wa watoto wachanga. Baba Mtakatifu Francisko daima anawataka wazazi, walezi na wasimamizi wa Ubatizo kushiriki kikamilifu katika kuwarithisha vyema watoto wao imani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwa njia ya ushuhuda wa maisha, yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Lengo kuu la Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” ni kuendeleaq kumwilisha furaha ya Injili katika uhalisia wa maisha ya waamini, tayari kujitoa na kujisadaka kuwa ni chemchemi ya furaha kwa ndugu, jamaa na jirani; zawadi kubwa kwa Mama Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hii ni nafasi ya kutangaza na kushuhudia umuhimu wa Sakramenti Takatifu ya Ndoa, tayari kushiriki ujenzi wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani, shule ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu.

Wazazi na wasimamizi wa Ubatizo wawe ni mifano bora ya kuigwa
Wazazi na wasimamizi wa Ubatizo wawe ni mifano bora ya kuigwa

Ndoa Takatifu inapyaisha upendo wa kibinadamu. Baba Mtakatifu analitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linatoa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake kwa: familia na vijana, kwa kukazia malezi, katekesi na majiundo awali na endelevu, kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani inayoweza kutolewa ushuhuda wa maisha. Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” liwe ni tukio shirikishi, litakalowagusa wana familia wote, kadiri ya wito na wajibu wao ndani ya familia, Kanisa na jamii katika ujumla wake. Maadhimisho haya yakoleze ari na mwamko wa maandalizi kwa wanandoa, kwa kuwasindikiza wanandoa wapya katika maisha na utume wao. Wazazi wapewe katekesi kuhusu dhamana na wajibu wao wa malezi: kiroho, kiutu na kitamaduni, ili waweze kutekeleza wajibu huu kwa umakini zaidi. Wazazi wafundwe na wapewe nafasi ya kushirikisha: matatizo, changamoto, uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, ili kutambua na hatimaye, kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kutangaza, kushiriki na kushuhudia mambo msingi katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anasema, ni kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanaitwa kuwa Wakristo, kwa kushirikishwa katika maisha na utume wa Kristo yaani: Ufalme, Unabii na Ukuhani wake, tayari kujenga na kudumisha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa! Baba Mtakatifu anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani na anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu nguvu ya kuweza kuwa kweli ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Ubatizo Watoto Wachanga

 

08 Januari 2023, 15:06