Sikukuu ya Kuongoka Kwa Mtakatifu Paulo Mwalimu na Mtume wa Mataifa: Wema na Haki
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa anakiri kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye alimtenga tangu tumboni mwa mama yake, akamwita kwa neema yake, Rej. Gal 1:15, akakutana uso kwa uso na Kristo Yesu Mfufuka wakati akiwa njiani kuelekea Dameski, akienda kuwadhulumu Wakristo. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinaelezea kwa kina wito wa Sauli, jinsi alivyoitwa na Kristo Yesu, akamwongokea Mungu, toka katika upofu mwili, akabahatika kuuona Mwanga wa kweli, Kristo Yesu Mfufuka, akawa kweli ni chombo kiteule cha Mungu, ili kutangaza na kushuhudia Jina la Mungu kwa watu wa Mataifa. Rej. Mdo 9:15. Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Januari sanjari na kilele cha Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo unafumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayotangazwa, kushuhudiwa na hatimaye, kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu. Juma la 56 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25 Januari 2023 linaongozwa na kauli mbiu: “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema Wakristo wote wanawajibika kushiriki katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kufikia umoja kamili na timilifu mintarafu fadhila za Kimungu katika Biblia na Liturujia, Mahubiri ya Neno la Mungu na Katekesi, Utume wa waamini walei, mtindo wa maisha ya kitawa na maisha ya kiroho katika ndoa; mambo yote haya ni muhimu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.
Hakuna uekumene wa kweli pasi na toba na wongofu wa kweli; sadala na upendo kwa jirani na hatimaye, ni fadhila ya unyenyekevu. Dhambi dhidi ya umoja wa Wakristo inaendelea kuwatafuna taratibu. Waamini wakumbuke kwamba, kadiri watakavyo jitahidi kuishi matakatifu, kufiatana na tunu za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile, watahamasishwa na watatekeleza umoja wa Wakristo, ikiwa kama wameungana na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ushirikiano huu ujengeke katika: sala, huku Wakristo wenyewe wakijitahidi kufahamiana; kufundisha kwa kuzingatia mchakato kiekumene na kwamba, majadiliano ya kiekumene hayana budi kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha. Rej. Lumen gentium 5-11. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa kiinjili kati yao na kati ya watu wa Mataifa, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadam alama yenye mvuto na mashiko kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake, na kama sehemu muhimu sana ya mapambano dhidi ya changamoto mamboleo. Wakristo kama ilivyokuwa kwa nyakati za Mtakatifu Paulo, Mtume wanapaswa kujitahidi kuungana pamoja kwa mawazo na maneno na kwamba, umoja wa Wakristo si mkakati wa kibinadamu bali ni changamoto kutoka kwa Kristo Yesu mwenyewe, anayewavuta wafuasi wake kuungana sanjari na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kutenda kadiri ya mapenzi yake yanayojikita katika upendo kwa mwanadamu. Mwenyezi Mungu ndiye kiini, sababu na kikolezo cha umoja miongoni mwa Wakristo.
Utengano miongoni mwa Wakristo si jambo la kawaida anasema Baba Mtakatifu Francisko, linahitaji kufanyiwa marekebisho ya kina, kwani utengano kati ya Wakristo una madhara makubwa katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Unahatarisha ushuhuda unaopaswa kutolewa na Wakristo duniani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu ndiye msingi wa Kanisa na urithi wa wakristo wote. Lakini inasikitisha kuona kwamba, bado Wakristo wenyewe wamegawanyika kinyume kabisa cha utashi wa Kristo mwenyewe na utengano huu unaendelea kuwa ni kielelezo cha kashfa ya ushuhuda wa utangazaji wa Injili duniani. Baba Mtakatifu anawatia shime Wakristo kufanya hija pamoja na kutegemezana ili kujenga na kuimarisha umoja miongoni mwa Wakristo. Katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, dhana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro imejidhihirisha wazi, mwaliko wa kuendelea kufahamiana zaidi kwa ajili ya majadiliano ya Kiekumene kwa kutambua utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hata kwa siku za usoni. Changamoto na vikwazo vinavyoendelea kujitokeza katika majadiliano ya Kiekumene ni mambo ambayo hayawezi kufichika, lakini kuna haja kwa Wakristo kupiga moyo konde na kuanza kujivika utashi wa Kristo kwa ajili ya umoja miongoni mwa Wakristo. Wawe tayari kuvuka vikwazo vyote vinavyosababisha utengano na hivyo kujivika nguvu ya upendo inayotolewa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa.