Tafuta

Ibada ya Jina Takatifu la Yesu inapata chimbuko na asili yake kwenye Maandiko Matakatifu na hatimaye kuingia kwenye Mapokeo ya Kanisa Ibada ya Jina Takatifu la Yesu inapata chimbuko na asili yake kwenye Maandiko Matakatifu na hatimaye kuingia kwenye Mapokeo ya Kanisa 

Sikukuu ya Jina Takatifu la Yesu 2023: Fadhila Na Shuhuda za Kikristo

Jina Takatifu la Yesu lilifafanua ndani mwake: Fumbo la Umwilisho linalopata hatima yake katika Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Hili ni jina linalofumbata na kuambata tunu msingi za maisha ya Kikristo: Ufukara, maisha, utume na kazi alizotenda Kristo Yesu kwa ajili ya kufunua na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada ya Jina Takatifu la Yesu inapata chimbuko na asili yake kwenye Maandiko Matakatifu. Lakini zilikuwa ni juhudi za Mtakatifu Bernardino wa Siena (8 Septemba 1380 - 20 Mei 1444), na Yohane wa Capistrano) Watawa wa Shirika la Ndugu Wadogo kuineza sehemu mbalimbali za dunia. Mtakatifu Bernardino wa Siena ndiye anayesadikiwa kutunga herufi IHS, yaani “Iesus Hominum Salvator.” Na kwa lugha ya Kigiriki “ΙΗΣΟΥΣ, Iesûs” “Yesu.” Kwa kuwa Jina Takatifu la Yesu ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Wakristo, Papa Innocent XIII akaieneza ulimwenguni kote. Na Mtakatifu Yohane Paulo II akatamka iandikwe kwenye Kalenda ya Liturujia ya Kiroma na kuadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Januari. Lengo la Sikukuu ya Jina Takatifu la Yesu ni kukuza na kudumisha fadhila za kikristo na kuboresha maisha ya Kikristo. Kwa namna ya pekee kabisa Mtakatifu Bernardino wa Siena alitaka kulipyaisha Jina Takatifu la Yesu kama lilivyojulikana kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Jina Takatifu la Yesu lilifafanua ndani mwake: Fumbo la Umwilisho linalopata hatima yake katika Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Hili ni jina linalofumbata na kuambata tunu msingi za maisha ya Kikristo: Ufukara, maisha, utume na kazi alizotenda Kristo Yesu kwa ajili ya kufunua na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake. Maandiko Matakatifu yanakaza kusema “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” Mt 1:21.

Mt. Bernardino wa Siena: Iesus Hominum Salvator
Mt. Bernardino wa Siena: Iesus Hominum Salvator

Kumbe, hili ni jina kadiri ya Maandiko Matakatifu linalofafanua utume wa Yesu, yaani “Mungu anaokoa." Katika maisha na utume wao, Mitume pamoja na wafuasi mbalimbali wameendelea kutenda miujiza na maajabu mengi kwa jina la Yesu kama Maandiko Matakatifu yanavyofafanua “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.” Yn 14:13-14. Mwinjili Luka katika Kitabu chake cha Matendo ya Mitume anakaza kusema, “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Mdo 4:12. Jina la Kristo Yesu ni chemchemi ya umoja na unyenyekevu “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya Msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.” Flp 2: 5-11.

Jina la Yesu 2023
03 January 2023, 15:27