Papa Mstaafu Benedikto XVI: Wosia wa Kiroho na Ratiba Elekezi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliyefariki dunia tarehe 31 Desemba 2022, katika wosia wa maisha yake ya kiroho, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake wa ajabu, ambao umemwongoza vyema katika maisha na utume wake. Anawashukuru wazazi wake kwa zawadi ya imani ambayo imemwongoza katika safari ya majiundo yake ya kisayansi. Anawashukuru ndugu zake wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yake, hadi akafanikiwa kuona njia ya kweli. Anawakumbuka wale wote waliochangia katika hatua mbalimbali za maisha, wito na utume wake, ambao alibahatika kuwatangazia na kuwashuhudia uzuri wa imani na ana matumaini makubwa kwamba, imani hii itaendelea kubaki imara na thabiti.
Anawashukuru kwa namna ya pekee kabisa watu wa Mungu mjini Roma na Italia katika ujumla wake, mahali ambako pamekuwa makazi yake kwa muda mrefu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika wosia wake wa maisha ya kiroho, anawataka watu wote aliokabidhiwa katika maisha na utume wake, waendelee kubaki imara na thabiti na kamwe wasipokwe imani kutokana na upembuzi yakinifu wa Maandiko Matakatifu. Wawe imara na kamwe wasikengeuke kwa tafsiri za kifalsafa zinazoweza kutolewa mintarafu Maandiko Matakatifu. Anaomba msamaha kwa wale wote waliokwazika katika maisha na utume wake. Anawataka wajitahidi kuwa wanyenyekevu wanapofanya majadiliano katika medani mbalimbali za maisha kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima na Kanisa licha ya udhaifu wake ni Fumbo la Mwili wa Kristo.
Mwishoni mwa wosia wake wa kiroho, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumkumbuka na kumwombea, licha ya dhambi na udhaifu wake, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo aweze kumpokea katika maisha ya uzima wa milele. Huu ni wosia aliouandika tarehe 29 Agosti 2006. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, kuanzia Jumatatu tarehe 2 Januari 2023 Saa 3:00 za Asubuhi kwa Saa za Ulaya, Mwili wa Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI utawekwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kutoa nafasi kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoa heshima zao za mwisho. Jumanne hadi Jumatano, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican litafunguliwa kuanzia saa 1: 00 za Asubuhi hadi Saa 1: 00 za Jioni kwa Saa za Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 5 Januari 2023, kuanzia Saa 3:30 Asubuhi kwa Saa za Ulaya ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye Sala ya Mwisho na Ibada ya Buriani “Ultima Commendatio & Valedictio” na mazishi kufanyika kwenye Makaburi yaliyoko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.