Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amevishukuru na kuvipongeza vikosi vya ulinzi na usalama vinavyotekeleza dhamana na wajibu wake msingi. Baba Mtakatifu Francisko amevishukuru na kuvipongeza vikosi vya ulinzi na usalama vinavyotekeleza dhamana na wajibu wake msingi.  (ANSA)

Papa Francisko: Shukrani na Pongezi Kwa Vikosi Vya Ulinzi na Usalama Mjini Vatican

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican kuendelea kuwa makini katika utume wao, kwa kuzingatia mambo msingi ambayo ni chimbuko la maisha na utume wao katika vyombo vya ulinzi na usalama ambao unasimikwa katika sadaka na wakati mwingine hatari, kwa shauku kuu ya kutoa huduma katika ujumla wake. Huduma makini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amevishukuru na kuvipongeza vikosi vya ulinzi na usalama vinavyotekeleza dhamana na wajibu wake msingi kwa kuzingatia weledi na dhamana kwa maisha ya watu na mali zao mjini Vatican, bila kuwasahau viongozi wa maisha ya kiroho, wanaowasindikiza kila siku katika shughuli zao. Anatambua na kuthamini uwepo wao wakati wa anapokutana na mahujaji pamoja na wageni wanaomtembelea Khalifa wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, wale wanaofanya hija kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro na waandamizi wake waliolala usingizi wa amani kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican; wakati wa Ibada na mikutano mbalimbali bila kusahau hija zake za kichungaji nchini Italia. Baba Mtakatifu ameyasema hayo, Alhamisi tarehe 12 Januari 2023 wakati alipokutana na vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican ili kutakiana heri na baraka za mwaka mpya wa 2023. Baba Mtakatifu anasema, anawashukuru sana kutoka katika sakafu ya moyo wake na anathamini uwepo na huduma makini inayotekelezwa kwa weledi mkubwa kama watumishi wa Serikali ya Italia, hali inayonogesha mahusiano na mafungamano mema na Vatican katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anawataka wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican kuendelea kuwa makini katika utume wao, kwa kuzingatia mambo msingi ambayo ni chimbuko la maisha na utume wao, ambao unasimikwa katika sadaka na wakati mwingine hatari, kwa shauku kuu ya kutoa huduma katika ujumla wake.

Papa Francisko anavipongeza vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican
Papa Francisko anavipongeza vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Sherehe za Noeli yataendelea kupyaishwa ndani mwao, ili kukoleza na kudumisha udugu wa kibinadamu na mshikamano wa upendo. Huu ni mwaliko wa kuendelea kugundua uzuri na nguvu mpya ya Injili, ili iweze kupenyeza na kuzama katika dhamiri na maisha yao katika ujumla, tayari kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu katika medani mbalimbali za maisha, lakini zaidi sehemu ya kazi. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani tarehe 1 Januri 2023 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos” umenogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Kupambana na UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia za amani.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huu anagusia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa makini kwa kujikita katika haki na ukweli; anayaangalia madhara yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; changamoto na mambo mazuri yaliyoibuliwa na UVIKO-19 na kwamba, walimwengu waendelee kujifunza kutokana na historia ya maisha ya mwanadamu.

Vyombo vya ulinzi na usalama vitekeleze dhamana kwa vitendo
Vyombo vya ulinzi na usalama vitekeleze dhamana kwa vitendo

Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wathesalonike anasema “Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.” 1The 5:1-2. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mwaliko kwa waamini kuwa na matumaini pamoja na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu anayewaongoza kwa huruma na mapendo; wakianguka, anawainua na kuwaelekeza katika njia salama, licha ya matukio ya ukosefu wa haki, mateso na mahangaiko mbalimbali. Huu ni wakati wa kuamka kutoka usingizini, ili kuondokana na woga, majonzi na hali ya kujikatia tamaa na badala yake, wainue macho yao kwa mng’ao wa mwanga hata katika giza nene! Hii ni njia muafaka ya kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani duniani, si kwa maneno matupu, bali kwa njia ya matendo, hasa wanapotekeleza dhamana na wajibu wao wa ulinzi na usalama wa watu na mali zao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia wote heri na baraka tele kwa mwaka 2023 na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na Mtakatifu Mikaeli, Malaika mkuu, ili waweze kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kuwakarimu ustawi, amani sanjari na kuwakinga dhidi ya hatari zote za roho na za mwili.

Ulinzi na usalama
12 January 2023, 14:43