Papa Francisko Dominika ya Neno la Mungu: Ni Kwa Wote, Toba na Ushuhuda Amini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Barua Binafsi, Motu Proprio “Aperuit illis” yaani: “Aliwafunulia akili zao” iliyochapishwa tarehe 30 Septemba 2019, kumbukumbu ya kiliturujia ya Mtakatifu Hieronimo, katika uzinduzi wa mwaka wa 1600 tangu alipofariki dunia, alianzisha maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu inayoadhimishwa Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa na kwa Mwaka huu inaadhimishwa Dominika tarehe 22 Januari 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.” 1Yn 1:3. Baba Mtakatifu anasema hii ni Dominika kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari, kulieneza na kulishuhudia Neno la Mungu. Ni dira na mwongozo wa maisha. Maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Dominika hii inaadhimishwa wakati wa Juma la kuombea Umoja wa Wakristo na maadhimisho haya kwa mwaka 2023 yanaongozwa na kauli mbiu “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu, tarehe 22 Januari 2023, ametoa daraja dogo kwa wasomaji watatu na kuwasimika Makatekista saba na amekazia kwamba: Neno la Mungu ni kwa ajili ya watu wote, ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu kwani ufalme wa Mungu umekaribia. Neno la Mungu linawawezesha watu wote kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekaza kusema, Injili inamwonesha Kristo Yesu, Mwalimu na Hujaji, daima akitembea huku na kule kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayofumbatwa katika huruma, msamaha na upendo, ili watu wote wa Mungu waweze kuona na hatimaye, kutembea katika nuru ya huruma ya Mungu kama ilivyokuwa kwa wale waliokuwa wanaishi ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya Mataifa, ili watu wapate kuyaona matendo yao mema na hivyo wamtukuze Mwenyezi Mungu aliye juu. Rej. Mt 4:15-16. Neno la Mungu linaganga, linatibu na kuwainua wale walioteleza na kuanguka. Neno la Mungu ni kwa ajili ya watu wote, ili kuwaganga na kuwaponya wagonjwa, kuwaokoa wadhambi; kuwatafuta na kuwaokoa Kondoo waliopotea; kuwasaidia wale wote waliovunjika na kupondeka moyo; wanaoelemewa na matatizo pamoja na changamoto za maisha.
Kristo Yesu anakaza kusema, huruma na upendo wa Mungu ni kwa ajili ya watu wote. Huu ni ujumbe kwa watu wa nyakati zote na kwamba, Neno la Mungu ni zawadi kwa watu wote na kila mmoja atajipatia zawadi hii kadiri ya Roho Mtakatifu atakavyomuwezesha, hii ni kwa sababu hata wokovu ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wote. Kumbe, changamoto ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu inapaswa kuwa ni kati ya vipaumbele vya Mama Kanisa, ili hatimaye, watu wa Mungu waweze kulipokea, ili hatimaye, hata wao waweze kushiriki katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Neno la Mungu linapaswa kuwa ni kiini na hatima maisha na utume wa Kanisa, ili watu wa Mungu waweze kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Neno la Mungu linamwilishwa katika maisha ya watu, maneno, maendeleo na vipaumbele katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Neno la Mungu ni mwaliko kwa kufanya toba na wongofu wa ndani, kwa kuamsha dhamiri mfu. “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.” Ebr 4: 12.
Neno la Mungu linapenya katika uhalisia wa maisha ya mtu na hivyo kumsaidia kufanya mang’amuzi ya kutambua mema na mabaya; kuona giza na mizizi ya dhambi, tayari kujivika silaha za mwanga kwa ajili ya mapambano, ili hatimaye, mwamini kuweza kumwelekea Mwenyezi Mungu katika maisha yake. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu ameamua kuwa jirani sana na waja wake. Baba Mtakatifu anawaalika watu wote wa Mungu kuweka maisha yao yote chini ya maongozi ya Neno la Mungu na kwamba, hata viongozi wa Kanisa wako chini ya maongozi ya Neno la Mungu, changamoto na mwaliko ni kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani, sanjari na kuendelea kuunganika na Kanisa la Kristo Yesu. Waamini wanapaswa kutoa nafasi kwa Neno la Mungu ili liweze kuwaongoza, kuwasafisha na kuwatakasa. Waamini wachunguze dhamiri zao na kuangalia wapi ambapo kimsingi wanahitaji toba na wongofu wa ndani. Neno la Mungu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili hatimaye, liweze kuwasaidia kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Neno la Mungu kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu: “Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.” Mt 4:19.
Mitume wakaacha yote na kumfuata, nao pia baada ya kukutana na Kristo Yesu, wakawashirikisha pia ndugu zao, tayari kuendeleza mchakato wa uvuvi wa watu, kwa kuwatangazia na kuwashuhudia ile furaha ya Injili. Neno la Mungu ni kama sumaku inayowavuta watu wa Mungu kutengeneza mtandao wa Injili ya upendo, ili waweze kuwa wavuvi wa Ufalme wa Mungu kwa watu wanaokutana nao katika hija ya maisha. Hata waamini katika ulimwengu mamboleo wanaitwa na kutumwa kuwa ni wavuvi wa watu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kila kukicha. Huu ni mwaliko wa kumwilisha Injili katika: Ukweli, haki na upendo, tayari kuwatafuta na kuwaganga wale wote waliopotea; wale waliovunjika na kupondeka moyo, ili wote hawa waweze kufarijika kwa Neno la Mungu. Hii ni kwa sababu, Mwenyezi Mungu ameamua kuwa ni jirani mwema, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu ni kumsikiliza kwa njia ya Neno lake, na humo, wataweza kupata mshangao wa ajabu.
Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake, Dominika ya Neno la Mungu kwa mwaka 2023 kwa kuwashukuru wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza, usiku na mchana kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linakuwa ni kiini cha maisha na utume wao, kwa kuwashirikisha wengine, kwa kulitangaza na kulishuhudia. Baba Mtakatifu anawashukuru wale wote wanaojitolea muda na nafasi yao, ili kusikiliza Neno la Mungu. Shukrani kwa wasomi na wanazuoni, wanaochakarika usiku na mchana, kwa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu; Kwa kulipembua na kulinyambulisha. Shukrani zinaiendea mihimili yote ya Uinjilishaji, inayojisadaka kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Shukrani za pekee zinawaendea Wasomaji wa Neno la Mungu na Makatekista, ambao katika maadhimisho ya Dominika ya Neno la Mungu, baadhi yao wamepewa daraja ya usomaji na wengine kuimarishwa katika huduma ya Ukatekista.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote ambao wamepokea mwaliko wake wa kujitahidi kutembea na Injili mifukoni mwao, ili waweze kuisoma na kuitafakari, kila siku ya maisha yao. Shukrani za dhati zinawaendea kwa namna ya pekee kabisa Mashemasi na Mapadre, wanaojitaabisha ili kuhakikisha kwamba, watu wateule wa Mungu wanalishwa kwa Neno la Mungu, ambalo wamelitafakari, wanajitahidi kuliishi na kulitangaza. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa huduma na sadaka yao. Neno la Mungu lilete faraja kwa watu wote wa Mungu na furaha ya kweli kwa wale wanaotangaza Neno la Wokovu!