Papa Francisko Asikitishwa na Maafa ya Watu 40 Nchini Senegal
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika salam za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, kwenda kwa Rais Macky Sall wa Senegal, anapenda kuungana na wale wote wanaoomboleza vifo vya ndugu, jamaa na wajuani wao 40 waliopoteza maisha kutokana na ajali iliyotokea huko Cheikh Deing, Kati kati ya mkoa wa Kaffrine nchini Senegal mapema Dominika tarehe 8 Januari 2023. Ajali hii imesababisha watu zaidi ya 78 kujeruhiwa vibaya.
Rais Mack Sall ametangaza kwamba, kuanzia tarehe 9 Januari, kwa muda wa Siku tatu, Senegal itapandisha bendera nusu mlingoti kama alama ya maombolezo kwa watoto wake waliopoteza maisha katika ajali hii mbaya. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wale wote waliofikwa na msiba huu mzito kwa sala na sadaka yake na kwamba, wale waliojeruhiwa waweze kupona haraka na hatimaye, kurejea katika maisha na shughuli zao za kila siku. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuwapokea na kuwaangazia mwanga wa maisha na uzima wa milele wote waliopoteza maisha; awafariji wale wote wanaoomboleza msiba huu mzito!