Papa,Marekani:wito wa kulinda uhai katika hatua zake zote!
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Papa Francisko anashukuru sana kwa ushuhuda mwaminifu uliooneshwa hadharani kwa miaka mingi na wale wote wanaohamasisha na kutetea haki ya kuishi ya watu wasio na hatia na walio hatarini zaidi wa familia yetu ya kibinadamu. Hayo ndiyo yaliyo andikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican katika ujumbe aliotuma kwa Askofu Michael Burbidge wa Arlington, na Rais wa Tume ya Maaskofu wa Marekani kwa ajili ya shughuli za kuhamasisha utetezi wa maisha, katika tukio la mkesha wa kitaifa wa kuombea uhai uliofanyika tarehe 19 Januari 2023 kwenye Kanisa Kuu la Madhabahu ya Kitaifa ya Mama Bikira Mkingiwa dhambi ya Asili huko Washington, Marekani.
Mkesha, Washington
Mkesha huo unatangulia na maandamano ya kila mwaka ya mwezi Machi kwa ajili ya utetezi wa Maisha, jijini Washington. Ni katika kumbukumbu ya miaka 50, tangu kuanza kwake ikiongozwa na kauli mbiu: “Hatua zinazofuata:maandamano kuelekea Amerika ya baada ya Roe”. Tukio hilo lilifunguliwa kwa kutafakari za hatua zitakazo chukuliwa baada ya Mahakama ya Juu kubatilisha kesi ya Roe vs. Wade na kuamua kuwa wanawake hawana haki ya kikatiba ya utoaji mimba".
Linda maisha ya mwanadamu
"Ujenzi wa jamii yenye haki ya kweli unategemea heshima kwa hadhi takatifu ya kila mtu na kukaribisha kila mtu kama kaka au dada," unasomeka ujumbe wa Papa, uliotiwa saini na Kardinali Parolin, uliochapishwa kwenye tovuti ya Baraza la Maaskofu wa Amerika (Usccb). “Katika suala hili, Baba Mtakatifu anaamini kuwa Mwenyezi Mungu ataimarisha dhamira ya wote, hasa vijana, kudumu katika juhudi za kulinda maisha ya binadamu katika hatua zake zote, hasa kwa hatua za kisheria za kutosha zinazotungwa katika kila ngazi ya jamii". Kwa wale wote ambao wameshiriki Maandamano ya kuhamasisha Maisha, na kwa wale wote wanaowaunga mkono kwa sala na sadaka zao", Baba Mtakatifu kwa hiari ametoa baraka zake kama ahadi ya nguvu na furaha katika Bwana.”