Nia za sala kwa mwezi Februari:kila parokia iwe mlango wazi kwa wote!
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Parokia sio klabu iliyotengwa kwa ajili ya wachache, bali ni mahali ambapo hakuna mahitaji maalum yanayotakiwa katika kuingia na ambayo mlango wake wa kuingilia unapaswa kusoma neno lililoandkwa: “kuingia bure.” Ni kwa nia hiyo ambayo Papa Francisko ametoa mwaliko kwa njia ya Video ili Kanisa zima kusali ambayo imetolewa na Mtandao wa Sala ya Papa Ulimwenguni kote kwa ajili ya mwezi Februari 2023. Njia moja ya kuomba kwamba "parokia kweli ziwe jumuiya, vituo vya kusikiliza na kukaribisha na milango yao wazi daima."
Ujumbe wa Papa: Parokia iwe wazi
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe huo kwa njia ya video amebainisha kuwa“Wakati mwingine nadhani tunapaswa kubandika bangomlangoni katika parokia lenye maneno yanayosomeka: 'Kiingilio bila malipo'”. Parokia lazima ziwe jumuiya za karibu, zisizo na urasimu, zinazojikita kwa ajili ya watu na ambamo ndani yake wanaweza kupata karama ya sakramenti. Lazima zirudi kuwa shule za huduma na ukarimu na milango iliyo wazi kila wakati kwa waliotengwa, kwa waliojumuishwa na kwa kila mtu”. Ujumbe wa Papa Francisko ni kwamba “parokia si klabu kwa ajili ya wachache, ambayo inahakikisha mali fulani ya kijamii”. Kwa hiyo anaendelea kutoa himizo kuwa: “Tafadhali, tuwe na ujasiri! Hebu sote tufikirie kwa upya mtindo wa jumuiya zetu za parokia”. Kwa hiyo nia ya Papa kwa ajili ya mwezi wa Februari “ili kwamba parokia, katika kujikita na umoja, ushirika wa watu na ushirika wa kikanisa katikati, zizidi kuwa jumuiya za imani, udugu na kukaribisha kwa wahitaji zaidi”.
Utajiri wa Kanisa ni watu
Sehemu ya nje ya parokia nzuri lakini ni tupu. Na baadaye parokia yenyewe, inajaa watu, ambayo kwa hiyo inakuwa nzuri zaidi. Ndivyo kwa njia ya Video ya Papa ya mwezi Februari inafunguka kama ilivyoletwa kwenye vyombo vya habari kwa kukumbuka kuwa utajiri wa Kanisa sio majengo, bali ni watu wanaoishi humo. Picha hizo zinazotoka parokiani za ulimwenguni, zikielezea mikutano ya kufurahisha, makongamano, usambazaji wa misaada kwa wahitaji zaidi, ziara za wazee na wagonjwa na maonesho. Kwa hiyo ni video iliyojaa maisha, kwamba maisha hutiririka katika parokia na bado huwafanya kuwa vituo (pointi) vya kumbukumbu kwa wengi, ambapo sanaa ya kujifunza kukutana inatokea hapo.
Parokia ni uwepo wa Kanisa kati ya nyumba
Katika taarifa hiyo kwa vyombo vya habari imekumbusha kwamba tayari katika Waraka wa Kitume Evangelii Gaudium, Papa Francisko alikuwa ameweka wazi, akinukuu usemi wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Christifideles laici, kuwa umuhimu wa parokia “ingawa sio taasisi pekee ya uinjilishaji, lakini parokia ina sifa maalum ya kuwa “Kanisa lenyewe linaloishi katikati ya nyumba za wana na binti zake”. Kwa sababu hiyo lazima iwe katika mawasiliano na familia na maisha ya watu na sio kuwa muundo wa muda mrefu uliotengwa na watu au kikundi cha viongozi waliochaguliwa wanaojiangalia wenyewe. Lakini katika wito huo wa marekebisho na upya wa parokia bado haujazaa matunda ya kutosha kwao kuwa karibu zaidi na watu”. Kwa hivyo, Papa Francisko amesisitiza juu ya wazo kwamba parokia lazima ziendeleze njia hiyo ya mageuzi ili daima kuwa wazi na kupatikana kwa wote bila kutengwa au kubagua, ndiyo maana anazungumzia uthubutu na kutafakari kwa upya juu ya mtindo wa sasa wa kuwa jumuiya.
Watu walio katikati ya maisha ya parokia
Akizungumzia juu ya nia ya maombi ya mwezi Februari, Padre Frédéric Fornos S.J., Mkurugenzi wa Kimataifa wa Mtandao wa Maombi ya Papa Ulimwenguni kote alikumbuka kwamba: “miaka michache iliyopita, Papa Fransisko aliiambia Jimbo la Isernia-Venafro kuwa “Kila jumuiya ya parokia inaitwa kuwa mahali pa pekee pa kusikiliza, kwa na kutangaza Injili; nyumba ya sala iliyokusanyika karibu na Ekaristi; shule ya kweli ya ushirika'. Kusikiliza, sala na ushirika kwa mujibu wa Padre Fornos ni ishara muhimu za sinodi kwa maisha ya parokia. Ili kufanya hivyo, hata hivyo, lazima wawe jumuiya, na watu katikati, kwa sababu sisi ni jumuiya wakati tunafahamiana, tunajua majina yao, mahitaji yao, sauti zao.”
Kutafakari kwa upya mtindo wa jumuiya zetu
Ni changamoto kubwa sana, alisisitiza mkurugenzi wa Mtandao huo, kiukweli kwani ni mara ngapi hutokea kwamba parokia inabadilishwa kuwa kundi la watu wasiojulikana zaidi au wasiojulikana ambao hukutana katika Misa za Dominika lakini bila maisha ya jumuiya? Kuwa jumuiya ya Kikristo ni neema, ambayo imezaliwa na imani ya pamoja, ya udugu unaoishi na wa kukaribisha walio na mahitaji zaidi; inatokana na uzoefu wa kawaida wa kiroho, kutoka katika kukutana na Kristo Mfufuka. Kama Papa Francisko asemavyo katika Video ya Papa kuwa lazima tuwe na 'ujasiri' katika kumsikiliza Roho Mtakatifu na sote tufikirie upya 'mtindo wa jumuiya zetu za parokia' alihitimisha Padre Fornos.