Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika Nia Zake za Jumla kwa Mwezi Januari 2023, anawaalika watu wote kuwaombea walimu ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa kufundisha udugu wa kibinadamu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia Zake za Jumla kwa Mwezi Januari 2023, anawaalika watu wote kuwaombea walimu ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa kufundisha udugu wa kibinadamu, 

Nia za Papa Francisko Kwa Mwezi Januari 2023: Walimu na Malezi ya Udugu wa Kibinadamu

Papa Francisko katika Nia Zake za Jumla kwa Mwezi Januari 2023, katika ujumbe wake kwa njia ya video, inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika watu wote wenye mapenzi mema kuwaombea walimu ili waweze kuwa ni mashuhuda wa kufundisha udugu wa kibinadamu, kulikokuwa ni vikwazo kwa vijana wa kizazi kipya na zaidi kwa vijana ambao ni dhaifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ni mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa mfumo wa elimu unaojikita katika msingi wa elimu fungamanishi. Lengo ni kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kujizatiti zaidi katika elimu fungamanishi inayowataka vijana hawa kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa! Baba Mtakatifu anakazia mfumo wa elimu itakayosaidia pia kuleta Mfumo Mpya wa Uchumi Duniani unaojikita katika wongofu wa kiikolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika mfumo wa elimu duniani unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu” mahali ambapo watu wote, kadiri ya dhamana zao, wanashiriki wajibu wa kuunda mtandao ambao ni wazi katika ujenzi wa mafungamano ya kibinadamu, kwani kila mtu anakuwa na wajibu wa kuchangia katika mchakato wa maboresho ya elimu! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia Zake za Jumla kwa Mwezi Januari 2023, katika ujumbe wake kwa njia ya video, inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea walimu ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa kufundisha udugu wa kibinadamu, kulikokuwa ni vikwazo kwa vijana wa kizazi kipya na zaidi kwa vijana ambao ni dhaifu.

Walimu wawasaidie kuelimisha udugu wa kibinadamu
Walimu wawasaidie kuelimisha udugu wa kibinadamu

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuangalia changamoto zinazomsibu mwanadamu sanjari na utume wa Kanisa. Kimsingi walimu hawawezi kutoa kile ambacho hawana wenyewe. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya walimu milioni 100 waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni wale wanaofundisha shule za: awali, msingi na sekondari; vyuo, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, kuna kundi kubwa la walimu wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika medani mbalimbali za maisha hata kama hawatambuliki rasmi. Hawa ni viongozi wa kijamii na kidini; ni watu wa kujitolea bila ya kujibakiza; wazazi; wachungaji na makatekista; walezi na wafanyakazi katika sekta ya elimu: washauri wa mambo ya biashara na uchumi na baadhi yao ni walimu wa michezo. Baba Mtakatifu anawataka wadau katika sekta ya elimu katika Mwezi huu wa Januari 2023 kuboresha huduma ya elimu kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu; kwa kuwathamini, kuwajali na kuwaendeleza wadhaifu zaidi. Walimu wawe na ujasiri wa kushuhudia kile wanachoamini na kukitenda kwa furaha. Walimu waendelee kuelimisha na kufundisha kwa ukamilifu kwa kutumia vyema viungo vyao vyote yaani: kichwa, mikono, roho na nyoyo zao. Wawe ni wadau makini katika ujenzi wa jumuiya yenye uwezo wa kufanya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuendelea kusoma alama za nyakati na kuwa ni sehemu ya wajenzi wa jumuiya.

Watoto wajenge utamaduni wa udugu wa kibinadamu
Watoto wajenge utamaduni wa udugu wa kibinadamu

Baba Mtakatifu Francisko anawataka walimu wawe ni wajenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu, kwa kuonesha njia ya amani na maridhiano na kamwe wasigeuke kuwa ni wapinzani wa mchakato wa ujenzi wa jamii shirikishi. Itakumbukwa kwamba, ellimu inaisaidia jamii kuwapokea wengine jinsi walivyo na si kama wanavyotaka wao, bila ya kuwahukumu wala kuwalaani. Kwa upande wake Padre Frédéric Fornos Mkurugenzi mkuu wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watenda kazi katika sekta ya elimu kutumia Waraka wa Kitume wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazomsibu mwanadamu, kwa kukazia elimu makini na wadau kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao. Walimu wawe ni wajenzi wa udugu wa kibinadamu na kamwe wasiwe ni sehemu ya migogoro ya kijamii. Wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha zilizoko ndani mwao. Na jambo hili linawezekana kwa njia ya sala.

Nia Januari 2023
10 January 2023, 16:00