Mkataba wa Ushirikiano wa Matumizi ya Akili Bandia: Maadili, Utu wema na Ushirikiano
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ilikuwa ni tarehe 28 Februari 2020, Mkataba wa Ushirikiano unaojulikana kama “Rome Call For Artificial Intelligence” unaozingatia kanuni maadili uliowekwa saini kati ya Taasisi ya Kipapa ya Maisha, Kampuni ya Microsoft, Kampuni ya IBM pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Food and Agriculture Organzation of the United Nations"; kifupi: FAO). Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali, yamesaidia kuleta maboresho makubwa katika matumizi ya “akili bandia”: “artificial intelligence” katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu, iwe kwa mtu binafsi au jamii katika ujumla wake. Mapinduzi makubwa ya teknolojia yanawawezesha watu kujifahamu sanjari na kuufahamu ulimwengu unaowazunguka, kiasi hata cha kuathiri maamuzi, uwezo wa kufiki na kutenda katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Leo hii utashi wa mwanadamu unaathiriwa kwa namna ya pekee na matumizi ya “akili bandia” kutokana na mchango wake mkubwa! Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya maisha iliyoanzishwa tarehe 11 Februari 1994, anasema, kuanzia mwaka 2020, Taasisi yake imekuwa ikifanya upembuzi yakinifu kuhusu matumizi ya “artificial intelligence” yaani “akili bandia” kwa ajili ya huduma ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hususan katika sekta ya afya.
Upembuzi huu pamoja na mambo mengine umekuwa ukichambua: kanuni maadili, haki msingi za binadamu na afya kwa kuwahusisha wasomi pamoja na viongozi wa ngazi ya juu kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa, akiwemo Bwana Dongyu Qu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO pamoja na Bwana Brad Smith, Rais wa Kampuni ya Microsoft. Tafiti hizi zimekuwa zikiendeshwa kwa kuzingatia Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; tunu msingi za maisha ya Kiinjili kuhusu zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Haya ni mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Taasisi ya Kipapa ya Maisha, ili kuibua na kuendeleza mang’amuzi na uzoefu wa maisha ya binadamu, ili kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Habari Njema ya Wokovu kuhusu maisha ya binadamu inawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi na wasomi pamoja na wanazuoni; wanasiasa na watetezi wa haki msingi za binadamu bila kuwasahau wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kudumisha kanuni maadili na utu wema.
Ni katika muktadha huu, tarehe 10 Januari 2023 Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na wajumbe waliotia saini Mkataba wa Ushirikiano unaojulikana kama “Rome Call For Artificial Intelligence” unaozingatia kanuni maadili na utu wema, tukio ambalo limeandaliwa na “Mfuko wa Renaissance.” Wajumbe ni kutoka katika dini ya Kiislam, Kiyahudi na Wakristo, wanaotaka kujielekeza zaidi katika maisha ya kiroho, utu, heshima na haki msingi za binadamu mintarafu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii.” Papa Francisko anasema, lengo ni kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii, bila kumwacha mtu awaye yote nyuma. Mwezi Julai 2023, huko nchini Japan, kutakuwa na Mkutano Maalum wa kutiwa saini kwa Mkataba wa Ushirikiano unaojulikana kama “Rome Call For Artificial Intelligence” unaozingatia kanuni maadili kwa kuwahusisha waamini kutoka katika dini kuu huko Mashariki.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wajumbe, amekazia umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili, utu wema na haki msingi za binadamu. Maendeleo makubwa ya sayansi yawe ni kwa ajili ya huduma, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Teknolojia isaidie kukuza na kudumisha huduma ya haki na amani duniani. Inapendeza kuona kwamba, mkataba huu, unawashirikisha pia viongozi wa kidini, waamini na watu wenye mapenzi mema, kielelezo makini cha mshikamano na mafungamano ya kijamii, kwa kutoa kipaumbele kwa maskini na wahitaji zaidi, huku haki msingi za binadamu zikipewa msukumo wa kwanza. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mambo msingi ya kuzingatia ni kanuni maadili, elimu na haki msingi za binadamu. Mkataba wa Ushirikiano unaojulikana kama “Rome Call For Artificial Intelligence” ni chombo madhubuti cha majadiliano ya kidini na kiekumene; mahali pa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu katika ulimwengu wa kidigitali.