Mbiu ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana 9 Aprili 2023: Mateso, Kifo na Ufufuko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2013 alisema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliongozwa na nyota angavu hadi wakafanikiwa kumwona Mtoto Yesu, Nuru halisi amtiaye nuru kila mtu. Rej. Yn 1:9. Kama mahujaji wa imani, Mamajusi wamegeuka wenyewe na kuwa ni nuru inayong'ara angani na hivyo kuwaonesha watu dira na njia. Watakatifu ni mwanga wa Mungu unaofukuzia mbali giza la usiku wa ulimwengu huu na kuwaongoza waamini katika Nuru ya kweli, Kristo Yesu, Bwana na Mkombozi. Baba Mtakatifu Francisko, katika Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2023 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika mahubiri yake, amekazia kuhusu Kristo Yesu nuru angavu anayekuja kuwaangazia watu wa Mataifa hija ya maisha ya kiroho, ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha pasi na kukata tamaa. Ni safari ya matumaini inayorutubishwa kwa: Neno la Mungu, Sala, Sakramenti za Kanisa, tayari kumwabudu na kumsujudu Kristo Yesu, Nuru angavu ya Mataifa na wala si kuabudu vitu!
Tokeo la Bwana, yaani Epifania ni kati ya Sherehe kubwa zinazoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria anajifunua kwa mataifa kama Mwana wa Mungu, Masiha na Mwanga wa Mataifa. Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, anatangaza pia Fumbo la Pasaka, linaloonesha kwa namna ya pekee, utukufu wa Kristo kati ya watu wake hadi pale atakapokuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Katika hija ya maisha ya kila siku, waamini wanajitahidi kumwilisha Fumbo la Ukombozi, kiini cha maadhimisho haya ni Liturujia ya Mwaka wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, Sikukuu tatu zinazoonesha: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, yaani Sherehe ya Pasaka ambayo kwa Mwaka huu itaadhimishwa hapo tarehe 9 Aprili 2023. Kila Dominika, Mama Kanisa anaadhimisha Pasaka ya Bwana na kuwawezesha waamini kuendelea kuadhimisha tukio hili kuu katika maisha na imani yao; kwani Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti. Sherehe ya Pasaka ni chemchemi ya Sikukuu nyingine zote zinazoadhimishwa na Mama Kanisa.
Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu, kitaanza rasmi tarehe 22 Mwezi Februari 2023 kwa kupakwa majivu, mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Mama Kanisa ataadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni hapo tarehe 21 Mei 2023 na Pentekoste, Sherehe ya kuzaliwa kwa Kanisa na Siku ya Waamini Walei kutangaza na kushuhudia Injili itaadhimishwa hapo tarehe 28 Mei 2023. Jumapili ya kwanza ya Majilio ambayo kimsingi ni mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kanisa, na maandalizi ya ujio wa Kristo itaadhimishwa hapo tarehe 3 Desemba 2023. Mama Kanisa anayeendelea kufanya hija yake hapa duniani anatangaza pia Pasaka ya Bwana, anapoadhimisha Sherehe na Sikukuu za Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa; Sikukuu za Mitume na Watakatifu mbali mbali; anapowakumbuka watoto wake waliotangulia katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini katika ufufuko wa wafu. Sifa na utukufu kwa Kristo aliyekuwepo, aliyepo na atakayekuja. Yeye ni Bwana wa Historia na nyakati zote ni zake, ni Alfa na Omega. Amina.