Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anamkumbuka kwa moyo wa shukrani Kardinali George Pell kwa sadaka, majitoleo na ushuhuda wake thabiti. Baba Mtakatifu Francisko anamkumbuka kwa moyo wa shukrani Kardinali George Pell kwa sadaka, majitoleo na ushuhuda wake thabiti. 

Kardinali George Pell Nguzo ya Mageuzi ya Kiuchumi Vatican: Jela Siku 404: Msamaha! Imani

Papa Francisko anamkumbuka kwa moyo wa shukrani Kardinali George Pell kwa sadaka na ushuhuda wake uliomwezesha kuweka msingi thabiti wa mageuzi katika uchumi wa Vatican. Akashutumiwa kwa nyanyaso za kijinsia na kufungwa jela siku 404, akakata rufaa na kushinda kesi, akiwa gerezani akawasamehe watesi wake kutokana na nguvu ya imani iliyokuwa ndani mwake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa halina budi kuendelea kujikita katika misingi ya ukweli, uwazi, uadilifu, weledi na maadili katika matumizi ya fedha na mali ya Kanisa ambayo kimsingi ni kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa kuzingatia kanuni hizi Kanisa, litaweza kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Hizi pia ni kanuni msingi zinazoweza kusaidia mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya Kanisa na umma katika ujumla wake, unaoweza kufanywa na “wajanja wachache.” Sekretarieti kuu ya Vatican, inapaswa kusoma alama za nyakati pamoja na kuyasaidia Makanisa yale ambayo bado "yanachechemea" katika masuala mbalimbali, ili kuweza kutekeleza utume wake barabara. Kwa upande wake, Sekretarieti ya Uchumi Mjini Vatican tangu kuanzishwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki ilikazia zaidi kuhusu: huduma makini, ukweli, uwazi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali fedha za Kanisa ambazo kimsingi ni kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Tangu wakati huo, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa kuandaa bejeti ya Vatican na taasisi zake. Udhibiti wa matumizi ya fedha za Kanisa utaendelea kufanyika ili kuhakikisha kwamba, kiwango cha bajeti kilichotengwa kinaheshimiwa kama sehemu ya maboresho ya huduma kwa watu wa Mungu kwa kuzingatia nidhamu, tija, weledi na ufanisi bora.

Kardinali Pell alisimamia ukweli dhidi ya shutuma nzito juu yake
Kardinali Pell alisimamia ukweli dhidi ya shutuma nzito juu yake

Huu ndio msingi, kanuni, sera na mikakati iliyopewa kipaumbele cha kwanza na Kardinali George Pell aliyefariki dunia, Jumanne, tarehe 10 Januari 2023 akiwa na umri wa miaka 81 hapa mjini Roma, baada ya kukabiliana na changamoto za kiafya kutokana na upasuaji mkubwa kwenye nyonga. Huduma hii ilikuwa imepangwa kwa muda, kiasi kwamba, tarehe 5 Januari 2023 aliweza kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko amepokea taarifa ya kifo cha Kardinali George Pell, Mwenyekiti mstaafu wa Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican kwa masikitiko na majonzi mazito. Baba Mtakatifu ametuma salam zake za rambirambi kwa Baraza la Makardinali, lakini kwa namna ya pekee kabisa kwa Bwana David pamoja na ndugu na jamaa, kama kielelezo chake cha ukaribu katika kipindi hiki cha majonzi. Baba Mtakatifu anasema, anamkumbuka kwa moyo wa shukrani Kardinali George Pell kwa sadaka, majitoleo na ushuhuda wake uliomwezesha kuweka msingi thabiti wa mageuzi katika uchumi wa Vatican.

Alimsindikiza Papa Benedikto XVI kwa sala na sadaka yake
Alimsindikiza Papa Benedikto XVI kwa sala na sadaka yake

Huu ni utume ambao aliutekeleza kwa ari, moyo mkuu, hekima na busara. Baba Mtakatifu anasema, anapenda kumwinulia Mwenyezi Mungu sala na kilio chake, kwa ajili ya mtumishi wake mwaminifu Kardinali George Pell, Mwenyekiti mstaafu wa Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican, bila kuteteleka ameifuata ile “Njia ya Msalaba” kwa uvumilivu mkubwa, sasa ampokee miongoni mwa wateule wake mbinguni na hatimaye amvike taji ya amani na maisha ya uzima wa milele. Itakumbukwa kwamba, Hayati Kardinali George Pell alizaliwa tarehe 8 Juni 1941 huko Ballarat, Australia na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 16 Desemba 1966. Tarehe 30 Machi 1987 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Melbourne, Australia na kuwekwa wakfu 21 Mei 1987. Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 16 Julai 1996 akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Melbourne na kusimikwa rasmi tarehe 16 Agosti 1996. Tarehe 26 Machi 2001 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa tena kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Sydney, nchini Australia na kusimikwa rasmi tarehe 10 Mei 2001.

Alituhumiwa, akakamatwa na kufungwa kwa siku 404, lakini akashinda kesi.
Alituhumiwa, akakamatwa na kufungwa kwa siku 404, lakini akashinda kesi.

Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 21 Oktoba 2003 akamteuwa na kumsimika kuwa Kardinali. Tarehe 13 Aprili 2013, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni mjumbe wa Baraza la Makardinali Washauri mjini Vatican. Tarehe 24 Februari 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Mwenyekiti wa Sekretariet ya Uchumi mjini Vatican. Mwaka 2017 akashutumiwa kwa kosa la kuwanyanyasa watoto wadogo kijinsia na mwaka 2019, Mahakama kuu nchini Australia ikamtia hatiani na kumhukumu kifungo cha miaka 6 jela. Kardinali George Pell kupitia kwa wakili wake, akakata rufaa na kushinda kesi mwezi Aprili 2020, taarifa iliyopokelewa kwa furaha na moyo wa shukrani na Vatican baada ya kutumikia adhabu ya kifungo kwa muda wa siku 404. Alipofunguliwa na kuachiliwa huru, akasema, amewasamehe wale waliomshutumu na kumnenea mabaya. Imani thabiti imekuwa ni nguzo yake wakati wote alipokuwa kifungoni.

Kifo Kardinali Pell
12 January 2023, 15:01