Tafuta

Papa Francisko: Jumuiya ya Papa Yohane XXIII: Kilio cha watoto wengi ni haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Papa Francisko: Jumuiya ya Papa Yohane XXIII: Kilio cha watoto wengi ni haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. 

Jumuiya ya Papa Yohane XXIII: Kilio Cha Watoto ni Amani Duniani

Familia ni mahali panapotoa hifadhi kwa wote, mahali muhimu pa kukuza na kudumisha mafungamano ya kifamilia kwa watu wote. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulipatia Kanisa zawadi ya Mtumishi wa Mungu Don Oreste Benzi, leo watoto wote hawa wanatambulikana kwa majina na sura zao halisi na wala si kivuli “Photocopy.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtumishi wa Mungu Don Oreste Benzi alizaliwa tarehe 7 Septemba 1925 huko Rimini nchini Italia. Baada ya masom na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 29 Juni 1949 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Katika maisha na utume wake, akajipambanua kuwa ni Padre, Mwalimu na kunako Mwaka 1968 akawa ni Muasisi wa Jumuiya Papa Yohane XXIII, inayojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Akafariki dunia tarehe 2 Novemba 2007. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 14 Januari 2023 alikutana na kuzungumza na Watoto wa Jumuiya ya Papa Yohane XXIII kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewaambia watoto hawa kwamba, Mwenyezi Mungu anasikiliza sala za watoto wanaolilia haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinatangazwa, zinashuhudiwa na zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kushikamana kama ndugu wamoja. Familia ni mahali panapotoa hifadhi kwa wote na kwamba, hapa ni mahali muhimu pa kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kifamilia kwa watu wote.

Kilio cha watoto wengi duniani ni haki, amani na maridhiano
Kilio cha watoto wengi duniani ni haki, amani na maridhiano

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kulipatia Kanisa zawadi ya Mtumishi wa Mungu Don Oreste Benzi, leo watoto wote hawa wanatambulikana kwa majina na sura zao halisi na wala si kivuli “Photocopy.” Wote watambue kwamba, ni watoto wateule wa Mungu, ndugu zake Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi wa Ulimwengu, wanaopendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo. Huyu ni Mwenyezi Mungu anayetambua amana, utajiri na udhaifu wa kila kiumbe chake, na hivyo kuwasaidia kukabiliana nao, ili hatimaye, waweze kufikia utimilifu wa maisha. Kristo Yesu ni utimilifu wa utu wa binadamu na upendo wa Mungu, unaopaswa kulindwa, kukuzwa na kupaliliwa ili uweze kutoa matunda yanayokusudiwa, yaani furaha ya kweli, licha ya matatizo na changamoto za maisha zinazowaandama kila kukicha! Baba Mtakatifu anawapongeza wazazi na walezi wote wanaojitahidi kuunda mazingira ya nyumba ya kifamilia, wazo na dhana iliyovaliwa njuga na Mtumishi wa Mungu Don Oreste Benzi, aliyebahatika kuwazamisha watoto na vijana katika malezi na makuzi ya kiutu, kwa jicho na upendo wa Kristo Yesu; akawa karibu sana kwa watoto watukufu, waliokuwa wamekosa kuonja huruma na upendo wa baba na mama zao kutokana na sababu mbalimbali za maisha.

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Don Oreste Benzi kwa msaada na nguvu ya Roho Mtakatifu, akafanikiwa kuwashirikisha watu wenye mapenzi mema malezi na makuzi ya watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuanzisha nyumba za kifamilia, ili kutoa fursa kwa watoto ambao hawakubahatika kuzaliwa na kulelewa katika mazingira ya kifamilia, huu ukawa ni uamuzi wa maisha, ili kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, mahali pa ukarimu na upendo. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea watoto wagonjwa pamoja na mama zao pamoja na kukazia umuhimu wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, ili kamwe watoto wasipokwe amana na utajiri wa maisha yao ya utoto kutokana na vita. Hii ni sala na kilio cha watoto wengi duniani, ipo siku Mwenyezi Mungu atajibu kilio hiki. Kwa wale watoto wanaotaabika kuhudhuria na hatimaye, kushiriki Ibada ya Misa Takatifu, watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anasikiliza kilio na matamanio yao halali. Waendelee kuwakumbuka na kuwaombea ndugu na jamaa zao waliofariki dunia na sasa wametangulia mbele ya haki, wakiwa na tumaini la maisha na uzima wa milele. Watoto hawa wamewakumbuka na kuwaombea watoto ambao wamefyekelewa mbali kutokana na utamaduni wa kifo unaokumbatia sera na mikakati ya utoaji mimba. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza watoto hawa ambao kila Dominika wanaungana pamoja na watoto wenzao sehemu mbalimbali za dunia kwa ajili ya kusali Rozari Takatifu. Wakumbuke kwamba, iko siku Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anayesikiliza sala zao, atawajibu kwa wakati muafaka. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa anawasaidie kuwalinda na kuwatunza katika imani, matumaini na mapendo.

Jumuiya Yohane XXIII
16 Januari 2023, 14:11