Juma la 56 la Kuombea Umoja wa Wakristo: Jengeni Ushirika Na Watu Wote
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Juma la 56 la Kuombea Umoja wa Wakristo kuanzia tarehe 18-25, Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa, Januari 2023 linanogeshwa na kauli mbiu: “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema Wakristo wote wanawajibika kushiriki katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kufikia umoja kamili na tilimifu mintarafu fadhila za Kimungu katika Biblia na Liturujia, Mahubiri ya Neno la Mungu na Katekesi, Utume wa waamini walei, mtindo wa maisha ya kitawa na maisha ya kiroho katika ndoa; mambo yote haya ni muhimu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hakuna uekumene wa kweli pasi na toba na wongofu wa ndani; sadaka na upendo kwa Mungu na jirani na hatimaye, ni fadhila ya unyenyekevu. Dhambi dhidi ya umoja wa Wakristo inaendelea kuwapekenya na kuwatafuna taratibu Wakristo. Waamini wakumbuke kwamba, kadiri watakavyo jitahidi kuishi matakatifu, kufuatana na tunu za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile, watahamasishwa na watatekeleza umoja wa Wakristo, ikiwa kama wameungana na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ushirikiano huu ujengeke katika: sala, huku Wakristo wenyewe wakijitahidi kufahamiana; kufundisha kwa kuzingatia mchakato kiekumene na kwamba, majadiliano ya kiekumene hayana budi kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha. Rej. Lumen gentium 5-11.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema kuwa wakristo chini ya ishara ya Msalaba kunawachochea waamini wote katika Kristo Yesu kusitawisha ushirika katika kila ngazi, katika jina la Mwenyezi Mungu anayewakumbatia wote kwa njia ya huruma yake. Wito wa Sauli: “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kwenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda. Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu. Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.” Mdo 9:1-19.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 25 Januari 2023 Mama Kanisa anaadhimisha, kilele cha Juma la 56 la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17. Waamini wanahimizwa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema, ili hatimaye, waweze kuvikwa nuru ya Kristo Mfufuka, ili na wao weze hatimaye, kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Neno la Mungu kwa wale wote wenye shida na mahangaiko mbalimbali; watu wanaohitaji kukombolewa, kugangwa na kuponywa kutoka katika undani wa maisha yao. Kutubu na hatimaye, kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa, ni kutokana na neema aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwa ni chombo kiteule cha kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama Mtume wa Mataifa. Msaada wa sala na maombi yake, uwawezeshe waamini kumwilisha upendo wa Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha yao, tayari kuwashirikisha pia na jirani zao.
Baba Mtakatifu anawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa na ujasiri wa kuondokana na tabia pamoja na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Waondokane na tabia ya kuchanganyikiwa, chuki, hasira na upinzani usiokuwa na mvuto wala mashiko na badala yake, wawe tayari kushirikiana na kushikamana na wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika kifungo cha upendo. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kiekumene cha Bossey kilichoko nchini Uswis. Amewataka vijana, wazee, wagonjwa na wanandoa wapya, kila mtu kadiri ya wito na hali yake ya maisha kujibidiisha kumwilisha ndani mwake dhana ya umoja wa Wakristo inayopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Kwa kutambua umuhimu wa zawadi hii, kila kukicha Wakristo wamtolee Mungu sala na sadaka kwa ajili ya umoja wa Wakristo.