Tafuta

Baba Mtakatifu anasema yuko kati yao, kuwaonesha ukaribu na faraja ya Kanisa zima, umuhimu wa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini DRC. Baba Mtakatifu anasema yuko kati yao, kuwaonesha ukaribu na faraja ya Kanisa zima, umuhimu wa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini DRC.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hotuba ya Papa Francisko Kwa Viongozi Nchini DRC: Amani, Upatanisho Mafao ya Wengi

Papa amegusia kuhusu: Rasilimali, amana na utajiri wa DRC, lakini imeharibiwa na vita, kinzani, wimbi kubwa la wakimbizi na unyonyaji unaofanywa na makampuni makubwa ya madini, dhahabu inayonuka damu ya watu wasio na hatia. Yuko kati yao kama hujaji wa mchakato wa upatanisho na amani, ili kuwaonesha ukaribu na faraja ya Kanisa zima, ujenzi wa udugu na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na msafara wake baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa “Ndjili”, Jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, alikaribishwa kwa heshima zote kitaifa na baadaye akamtembelea Ikulu Rais Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo aliyeingia madarakani tarehe 24 Januari 2019. Baadaye, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi na mashirika ya Kimataifa nchini DRC. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amegusia kwa namna ya pekee kuhusu: rasilimali, amana na utajiri wa DRC, lakini imeharibiwa na vita, kinzani, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji pamoja na unyonyaji mkubwa unaofanywa na makampuni makubwa ya uchimbaji wa madini, dhahabu inayonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia. Yuko kati yao kama hujaji wa mchakato wa upatanisho na amani. Baba Mtakatifu anasema yuko kati yao, kuwaonesha ukaribu na faraja ya Kanisa zima, umuhimu wa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini DRC, mchango wa dini katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu, utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, madaraka yanapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu katika ukweli na uwazi; haki na amani sanjari na uwajibikaji wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Watu wa Mungu nchini DRC wanapaswa kujikita katika ujasiri ili kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya watu.

Papa Francisko: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Papa Francisko: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu nchini DRC, ambayo imebarikiwa kwa rasilimani, amana na utajiri mkubwa, lakini kutokana na vita, ghasia, kinzani na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, nchi imeharibika na kunyonywa sana, kinyume cha utu na kazi ya uumbaji. Baba Mtakatifu anasema, amekuja na yuko kati yao kama hujaji wa mchakato wa upatanisho na amani, kuonesha ukaribu na faraja ya Kanisa Katoliki. Almasi ni kati ya madini yanayopatikana kwa wingi nchini DRC. Umefika wakati kwa watu wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanajiamini na hivyo kutumia kikamilifu akili, busara na nguvu, kuleta mageuzi katika nchi yao kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kujikita katika amani na kwa nguvu, juhudi na maarifa waweze kuijenga nchi yao. Kwa msaada wa Mungu waanze kujikita katika msingi wa amani na maendeleo; kwa kujizatiti katika haki, msamaha, maridhiano na upatanisho, huku wakiendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao: Wakomeshe vita, chuki na uhasama kati yao, kwani ni vitendo vinavyokwenda kinyume cha Ukristo na utu wa binadamu katika ujumla wake; wazike vitendo hivi na kuanza kujielekeza kwa yale yajayo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hata leo hii licha ya nchi nyingi Barani Afrika kujipatia uhuru wa bendera, lakini bado zinaelemewa na ukoloni wa kiuchumi, unyonyaji pamoja na ukwapuaji mkubwa wa ardhi, kiasi kwamba, raia wanaonekana kuwa kama wageni katika nchi yao wenyewe. Baba Mtatakatifu anasema, umefika wakati wa kuondoa mirija ya unyonyaji nchini DRC., na Barani Afrika katika ujumla wake, ili Waafrika wenyewe waweze kuwa ni wadau wa ustawi, maendeleo na mafao yao wenyewe na kwamba, walimwengu watambue kwamba, kwa miaka mingi wamelinyonya Bara la Afrika, sasa tabia hii lazima ifikie ukomo wake. Diplomasia ya Kimataifa ijikite katika utu, heshima na haki msingi za binadamu, kwa kutoa fursa kwa watu wa Mungu Barani Afrika kujiendeleza kiuchumi na wala si diplomasia inayodhibiti amana na utajiri wa Bara la Afrika. Afrika inahitaji soko la bidhaa zake kwa ajili ya ustawi, maendeleo fungamani ya binadamu kwa ajili ya Bara la Afrika. Baba Mtakatifu anazipongeza nchi na Mashirika ya Kimataifa yanayochangia kwa hali na mali katika mapambano dhidi ya umaskini, magonjwa na ujinga; kwa kujikita katika utawala wa sheria na kwa kuheshimu utu wa binadamu.

Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote
Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote

Umefika wakati wa kuweka kando tofauti ndogo ndogo na kuanza kujikita katika ujenzi wa mtandao wa kijamii, utakaowaunganisha watu badala ya kuwatenganisha; mtandao utakao wakutanisha watu ili kwa pamoja waweze kusimama kidete na kujielekeza katika amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Dini zichangie katika kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya watu, uhuru wa kuabudu na kuondokana na wongofu wa shuruti, ili kuheshimu dhamiri nyofu ya watu, haki msingi za binadamu na elimu bora. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu kutoka DRC ambao wamesimama kidete kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, haya mambo msingi yanapatikana kwa ajili ya watu wengi. Madaraka na uongozi ni kwa ajili ya huduma kwa jamii, ili kukuza na kudumisha demokrasia, chaguzi huru, za kweli na za haki; zinazowashirikisha watu wengi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo, mafao na usalama wa raia na mali zao na hivyo kuondokana na uongozi unaowanyonya watu na kuwaacha wakiteseka na umaskini, ujinga na magonjwa. Viongozi wajenge utamaduni wa huduma na hivyo kuwa karibu na wananchi wao, ili kudumisha misingi ya haki, amani, usawa, utawala wa sheria na haki ya kupata habari.

Uongozi ni huduma katika haki, amani na ustawi wa wengi
Uongozi ni huduma katika haki, amani na ustawi wa wengi

Baba Mtakatifu anasema, elimu bora ni msingi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Afrika. Elimu itawajengea watu wa Mungu uwezo wa kujiamini. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu, ili kujenga jamii inayosimikwa katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; watu wanaotambua na kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza, huku wakiwajibika na kuendelea kuwa wadumifu. Kwa bahati mbaya, mfumo wa elimu umewafanya watu wengi kunyonywa na kudhalilishwa kwa kufanyishwa kazi za suluba migodini. Kuna watoto wengi wametumbukizwa katika kashfa hii, kiasi kwamba wamepokwa haki zao msingi, utu na heshima yao. Watoto na vijana wanapaswa kujengewa matumaini ya leo na Kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anawataka watu wa Mungu nchini DRC kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kujizatiti katika amani, ustawi na maendeleo ya wengi sanjari na kudumisha ushirikiano na mshikamano na Jumuiya ya Kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa iwe mstari wa mbele kulisaidia Bara la Afrika kupambana kikamilifu na madhara ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Bara la Afrika linapaswa kujenga mifumo inayopania kuboresha maisha ya watu katika elimu na afya; kwa kuwekeza zaidi katika uhakika na usalama wa chakula, ili kuondokana na baa la njaa pamoja na magonjwa yanayopekenyua nguvu kazi kama vile Malaria.

Haki, amani na upatanisho muhimu kwa maendeleo ya wengi
Haki, amani na upatanisho muhimu kwa maendeleo ya wengi

Baba Mtakatifu amehitimisha hotuba yake kwa kuwataka watu wa Mungu nchini DRC kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu na kuwa na matumaini; ili kulinda na kudumisha utu na heshima yao na wajasiri katika kupyaisha jamii. Hii ni dhamana inayoweza kutekelezwa miongoni mwa watoto na vijana. Baba Mtakatifu Francisko anasema, ataendelea kushikamana na wale wote wanaojikita katika mchakato wa amani, maridhiano, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini DRC.

Papa Hotuba kwa viongozi

 

31 January 2023, 17:36