Tafuta

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC na Sudan ya Kusini ni kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi 5 Februari 2023. Hujaji wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC na Sudan ya Kusini ni kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi 5 Februari 2023. Hujaji wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa.  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko: DRC na Sudan ya Kusini: Amani na Upatanisho wa Kitaifa

Papa anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu na mshikamano na watu wa Mungu katika nchi hizi mbili ambao kwa muda mrefu wameteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, ili hatimaye, sasa kuanza kukoleza mchakato wa haki, amani na maridhiano. Papa anatembelea nchi hizi kama kiongozi wa dini na mchungaji wa watu wa Mungu; hujaji wa amani na upatanisho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 5 Februari 2023 anafanya Hija ya Kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini. Lengo ni kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu, Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; amani na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika nchi hizi mbili. Hija ya Baba Mtakatifu nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala wanatembelea Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023. Hija hii inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho na umoja wa Kitaifa, ili hatimaye, mamilioni ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum waweze kurejea tena katika maisha yao ya kawaida, huku wakishiriki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hizi ni jitihada za kutaka kurejesha amani na kuachana na kinzani, migogoro na mipasuko ya kikabila, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja, tofauti zao msingi ni amana na utajiri kwa wote. Haya ni kati ya mawazo makuu yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati huu wa maandalizi ya Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini DRC na Sudan ya Kusini.

Papa Francisko anataka kuonesha ukaribu na mshikamano wake
Papa Francisko anataka kuonesha ukaribu na mshikamano wake

Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu, mshikamano wa udugu wa upendo na watu wa Mungu katika nchi hizi mbili ambao kwa muda mrefu wameteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, ili hatimaye, sasa kuanza kukoleza mchakato wa haki, amani na maridhiano. Baba Mtakatifu anatembelea nchi hizi kama kiongozi wa dini na mchungaji wa watu wa Mungu; hujaji wa amani na upatanisho. Baba Mtakatifu ataka kuwachangamotisha watu wa Mungu nchini DRC kupyaisha tena imani, matumaini na mapendo, kwa kuondokana na vita, ili kuimarisha mchakato wa amani na upatanisho wa Kitaifa unaoendelea nchini humo. Mikoa ya Mashariki mwa DRC imeathirika sana na vita na Baba Mtakatifu anapenda kukutana na waathirika, ili apate kuwafariji kwa Neno na uwepo wake; kwa kuwatia shime kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo na kamwe wasitumbukie katika mtego wa kutaka kulipiza kisasi, kuendeleza mipasuko ya kijamii, kisiasa na kidini. Lengo kuu ni amani ya kudumu, itakayowawezesha kujenga na kudumisha umoja wa Kitaifa na udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Itakumbukwa kwamba, baada ya kipindi cha sala, tafakari na upatanisho kwa ajili ya amani kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, Alhamisi, tarehe 11 Aprili 2019, Baba Mtakatifu Francisko alipiga magoti kwa unyenyekevu na heshima kubwa na kuanza kubusu miguu ya viongozi wa Sudan ya Kusini, waliokuwa wanatarajia kuanza utekelezaji wa muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Serikali ya mpito, hapo tarehe 12 Mei 2019.

Ushuhuda wa upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu ni muhimu.
Ushuhuda wa upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu ni muhimu.

Kitendo cha Baba Mtakatifu Francisko kuwapigia magoti viongozi wa Sudan ya Kusini ni kielelezo cha kilio cha ndani kutoka kwa Baba Mtakatifu anayeguswa na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini kutokana na vita, njaa na magonjwa! Ni kitendo kinachovuka protokali za kidiplomasia, lakini kinaeleweka kwa watu wanaotambua mateso ya wananchi wa Sudan ya Kusini ambao wana kiu ya haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa! Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Sudan ya Kusini kushinda kishawishi cha utengano, kinzani, mipasuko na vita na kuanza kukumbatia na kuambata mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Katika kipindi hiki cha mpito, matatizo na changamoto kamwe haziwezi kukosekana, lakini jambo la muhimu ni kutambua kwamba, wao ni wananchi na waasisi wa Sudan ya Kusini, wanaotegemewa kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Baba Mtakatifu anasema, Injili ya amani inasimikwa katika kukuza na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watambue kwamba kama viongozi wanawajibika mbele ya Mungu na mbele ya raia wao wanaotamani kuona haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa vikitawala tena Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amani inawezekana Sudan ya Kusini, kinachotakiwa kwa sasa ni utashi wa kisiasa unaofumbatwa katika toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa kitaifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Sudan ya Kusini. Kardinali Parolin anakaza kusema, kinachohitajika ni kuwa na utashi wa kisiasa tayari kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kwa vitendo.

Ushuhuda wa kiekumene na watu wa Mungu Sudan ya Kusini
Ushuhuda wa kiekumene na watu wa Mungu Sudan ya Kusini

Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian la Scotland, wanatembelea kwa pamoja Sudan ya Kusini, kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Hizi ni sauti za viongozi watatu wa Makanisa, wanaotaka kupaaza sauti zao kwa ajili ya ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano nchini Sudan ya Kusini. Hija hii ya Kitume, inapania kumwezesha Baba Mtakatifu Francisko kujionea mwenyewe matumaini na umaskini wa watu wa Mungu, unaopaswa kusimikwa katika msingi wa haki na amani, kama jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu. Mama Kanisa nchini Sudan ya Kusini anataka kuendeleza mchakato wa huduma ya upendo kwa watu wa Mungu hususan katika huduma ya upendo inayomwilishwa katika sekta ya elimu na afya. Kardinali Pietro Parolin anasema, anayo furaha kubwa kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya Kitume Barani Afrika ambako anatembelea DRC na Sudan ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, mwezi Julai 2022, Kardinali Parolin alitembelea nchini DRC na Sudan ya Kusini kuonesha mshikamano wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye kutokana na changamoto za kiafya alilazimika kufuta hija hiyo Barani Afrika. Sasa watu wa Mungu wako tayari kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu kuwatembelea.

Watu wa Mungu wanasubiri kwa hamu ujio wa Papa Francisko DRC na S.Kusini
Watu wa Mungu wanasubiri kwa hamu ujio wa Papa Francisko DRC na S.Kusini

Baba Mtakatifu akiwa ameungana na viongozi wengine wa kidini, wanaweza kusaidia kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu wa Mungu nchini DRC na Sudan ya Kusini. Haya ndiyo matamanio ya wengi, changamoto na mwaliko kwa watu wote wa Mungu kupyaisha tena dhamana na wajibu wao, ili kujielekeza zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa sasa na kwa siku za usoni! Viongozi watambue kwamba, wananchi wa Sudan ya Kusini, wamechoka na vita ambavyo vimewasababishia majanga na maafa makubwa katika maisha yao na sasa wanatamani kuona leo na kesho iliyo bora zaidi, inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na upatanisho! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikana pamoja na viongozi wengine wa Makanisa wataweza kutembelea Sudan ya Kusini, kama kielelezo cha mshikamano wa uekumene wa sala na huduma ya upendo, ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini nchini Sudan ya Kusini, watakuwa kweli mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, maridhiano na umoja wa kitaifa. Ushuhuda huu unapaswa kufumbatwa katika sala, maongozi ya maisha ya kiroho na huduma makini, kielelezo cha imani inayofumbatwa katika matendo!

Papa Hija Afrika

 

28 January 2023, 17:12