Hija ya Kitume ya Papa Francisko Barani Afrika: DRC na Sudan ya Kusini: Uekumene, Haki na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 5 Februari 2023 anafanya Hija ya Kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini. Hizi ni nchi ambazo kwa miaka mingi wananchi wake wamejaribiwa na kutikiswa sana na vita pamoja na kunyonywa sana. Kutokana na vita watu wengi wamelazimika kuzikimbia nchi zao, ili kutafuta hifadhi na usalama pamoja na kutafuta maisha bora zaidi. Lengo la Hija hii ya Kitume ni kutangaza na kushuhudia amana na utajiri wa Neno la Mungu, Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; amani, maridhiano na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika nchi hizi mbili. Hija ya Baba Mtakatifu nchini DRC kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 3 Februari 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wapatanishwe katika Yesu Kristo.” Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma, maisha ya kiroho, damu na sala wanatembelea Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 3 Februari hadi tarehe 5 Februari 2023.
Hija hii inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho na ujenzi wa umoja wa Kitaifa, ili hatimaye, mamilioni ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum waweze kurejea tena katika maisha yao ya kawaida, huku wakishiriki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anasema hii ni hija ya uekumene wa amani kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Hizi ni jitihada za kutaka kurejesha amani na kuachana na kinzani, migogoro na mipasuko ya kikabila, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja, tofauti zao msingi ni amana na utajiri kwa wote. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mambo mengine, anapania kuwa ni hujaji wa amani, ili kusaidia kunogesha mchakato wa upatanisho, utakaosaidia kuleta faraja kwa Makanisa mahalia na watu wa Mungu katika ujumla wake; kwa kuwatia shime wananchi kujikita katika ustawi na maendeleo yao na hatimaye, kusaidia kuragibisha kuhusu hali ya watu wa Mungu Barani Afrika katika ujumla wake. Hili ni Bara kubwa linalo paswa kupewa uzito stahiki.
Baba Mtakatifu anawaalika na kuwahimiza waamini kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, kwani ndani ya Moyo wake safi usiokuwa na doa, watu wote wanapata utambulisho wao, kwa kupenda na kupendwa, hali inayoonesha uwepo wa Mungu kati ya waja wake. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Mlango wa Mbinguni ni “Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini.” Ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa wote wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma na upendo wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza yake ya kitume Barani Afrika, Jumatatu, tarehe 30 Januari 2023 amekwenda na kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ili kujikabidhi katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, akiombea mafanikio katika hija hii ya Kitume Barani Afrika.