Hayati Papa Benedikto XVI: Shuhuda wa Ukweli wa Kiinjili & Udugu wa Kibinadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliyefariki dunia tarehe 31 Desemba 2022 na kuzikwa tarehe 5 Januari 2023 katika wosia wa maisha yake ya kiroho, aliouandika tarehe 29 Agosti 2006 anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake wa ajabu, ambao umemwongoza vyema katika maisha na utume wake. Anawashukuru wazazi wake kwa zawadi ya imani ambayo imemsindikiza katika safari ya majiundo yake ya kisayansi. Anawashukuru ndugu zake wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yake, hadi akafanikiwa kuona njia ya kweli. Anawakumbuka wale wote waliochangia katika hatua mbalimbali za maisha, wito na utume wake, ambao alibahatika kuwatangazia na kuwashuhudia uzuri wa imani na ana matumaini makubwa kwamba, imani hii itaendelea kubaki imara na thabiti. Anawashukuru kwa namna ya pekee kabisa watu wa Mungu mjini Roma na Italia katika ujumla wake, mahali ambako pamekuwa makazi yake kwa muda mrefu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika wosia wake wa maisha ya kiroho, anawataka watu wote aliokabidhiwa katika maisha na utume wake, waendelee kubaki imara na thabiti na kamwe wasipokwe imani kutokana na upembuzi yakinifu wa Maandiko Matakatifu.
Wawe imara na kamwe wasikengeuke kwa tafsiri za kifalsafa zinazoweza kutolewa mintarafu Maandiko Matakatifu. Anaomba msamaha kwa wale wote waliokwazika katika maisha na utume wake. Hayati Papa Benedikto XVI anawataka wajitahidi kuwa wanyenyekevu wanapofanya majadiliano katika medani mbalimbali za maisha kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima na Kanisa licha ya udhaifu wake ni Fumbo la Mwili wa Kristo. Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 11 Januari 2023 katika Mzunguko Mpya wa Katekesi kuhusu Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13; amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 5 Januari 2023 Mama Kanisa amemwimbia Mwenyezi Mungu wimbo wa sifa na shukrani kwa zawadi ya Hayati Papa Benedikto, mafundisho yake na ushuhuda wa maisha na utume wake. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwangalia kwa imani na matumaini, Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, ili kuonja yale mang’amuzi yaliyoibuliwa katika maisha na utume wa Mathayo mtoza ushuru ambaye alitubu, akaongoka na kuwa ni mtangazaji mwaminifu wa Injili na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.
Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI alijitahidi kuyasimika maisha yake katika Kweli za Kiinjili na Upendo wa Kidugu. Awe ni mfano bora katika mchakato wa kumwilisha: Kweli wa Kiinjili na Udugu wa Kibinadamu katika mazingira ya kifamilia, maeneo ya kazi na jamii katika ujumla wake. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kila siku ya maisha yao, wanatangaza na kushuhudia uzuri wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu ametambua uwepo na ushiriki wa wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali ambao wameanza mwaka wa masomo 2023-2024, bila kuwasahau mahujaji kutoka nchini Uganda. Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu unasimikwa katika ushuhuda na ushirika wa upendo kwa Mungu na jirani. Waamini wawe ni vyombo na wajenzi wa utulivu, amani na maridhiano katika jamii, kwa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene yanayosimikwa katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kuwakumbuka na kuwaombea watu wote wa Mungu wanaoathirika kutokana na Vita Kuu ya Tatu ya Dunia, inayoendelea kupiganwa vipande vipande, sehemu mbalimbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anapenda kuwaonesha uwepo na ukaribu wake katika kipindi hiki cha mahangaiko makubwa kwa sala na sadaka yake. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kimya mbele ya Sanamu ya Bikira Maria, Mama wa wote, inayoheshimiwa kwa namna ya pekee na watu wa Mungu nchini Belarus.