Tafuta

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 11 Februari 2013 alifanya maamuzi mazito yaliyosimikwa katika hekima na busara; imani, matumaini na mapendo: Fadhila za Kimungu Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 11 Februari 2013 alifanya maamuzi mazito yaliyosimikwa katika hekima na busara; imani, matumaini na mapendo: Fadhila za Kimungu 

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI: Imani, Matumaini na Mapendo: Yesu Nakupenda!

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake, amehubiri katika kipindi cha miaka 71, ameandika vitabu 66; Nyaraka za Kitume 3 na Wosia wa Kitume 4. Machapisho yote haya, ameyatolea muhtasari dakika chache kabla ya kufikwa na mauti kwa kusema, “Yesu Nakupenda.” Hizi ni fadhila za Kimungu ili kupyaisha imani tayari kuitangaza na kuishuhudia kikamilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika wosia wake wa maisha ya kiroho, aliouandika tarehe 29 Agosti 2006 anawataka watu wote aliokabidhiwa katika maisha na utume wake, waendelee kubaki imara na thabiti na kamwe wasipokwe imani kutokana na upembuzi yakinifu wa Maandiko Matakatifu. Wawe imara na kamwe wasikengeuke kwa tafsiri za kifalsafa zinazoweza kutolewa mintarafu Maandiko Matakatifu. Anaomba msamaha kwa wale wote waliokwazika katika maisha na utume wake. Anawataka wajitahidi kuwa wanyenyekevu wanapofanya majadiliano katika medani mbalimbali za maisha kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima na Kanisa licha ya udhaifu wake ni Fumbo la Mwili wa Kristo. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 11 Februari 2013 alifanya maamuzi mazito yaliyosimikwa katika hekima na busara; imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Januari 2023 anaandika historia mpya ya Kanisa Katoliki kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mtangulizi wake Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliyefariki dunia tarehe 31 Desemba 2022. Kuna watu ambao wameacha alama ya kudumu katika taalimungu, kwa kuchangia mawazo na nia, sanjari na kufanya tafakari ya kina kuhusu Fumbo la maisha ya mwanadamu mintarafu Fumbo la Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ameweza kuunganisha mawazo katika masomo ya Sayansi na katika huduma yake ya kichungaji kama Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa Benedikto XVI: Imani, Matumaini na Mapendo
Papa Benedikto XVI: Imani, Matumaini na Mapendo

Tafakari zake zimekuwa ni chombo ambacho kiko tayari kusaidia mchakato wa kuifahamu, imani, tayari kuitangaza na kuishuhudia, kwa kuwaongoza wenye matumaini katika kuufikia ukweli mfunuliwa. Kwa ufupi kabisa, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake, amehubiri katika kipindi cha miaka 71, ameandika vitabu 66; Nyaraka za Kitume 3 na Wosia wa Kitume 4. Machapisho yote haya, ameyatolea muhtasari dakika chache kabla ya kufikwa na mauti kwa kusema, “Yesu Nakupenda.” Fadhila za Kimungu zinapania kuwasaidia waamini kupambana na changamoto mamboleo, kwa kukazia zaidi mambo msingi katika maisha ya Kikristo na hivyo kuendelea kuyaboresha siku kwa siku. Fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Mapendo ni tunu ambazo Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali walizichukua vibindoni mwao ili kumpelekea Mtoto Yesu, yaani: Dhahabu, Uvumba na Manemane. Mababa wa Kanisa wanasema, dhahabu ni alama ya ufalme wa Kristo. Huu ni ufalme wa milele na wa ulimwengu wote; ni ufalme wa kweli na uzima, utakatifu, haki, upendo na amani! Uvumba ni alama ya Umungu wa Kristo, yaani Nafsi ya Pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Manemane ni kielelezo cha ubinadamu wake, Kristo Yesu aliyezaliwa kwake Bikira Maria, akateswa, akafa na kufufuka. Waamini kama Mamajusi wa nyakati zile, wanabeba ndani mwao Fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Mapendo, huku bondeni kwenye machozi.

Papa Benedikto XVI: Chemchemi ya mageuzi Sekretarieti kuu ya Vatican
Papa Benedikto XVI: Chemchemi ya mageuzi Sekretarieti kuu ya Vatican

Fadhila ni maelekeo ya mazoea ya kutenda mema. Kuna fadhila kuu tatu za Kimungu: Imani, Matumaini na Mapendo. Rej. 1Kor 13:13. Hizi zinaunda fadhila adili na kuzipatia uzima. Imani ni fadhila ya Kimungu inayomwezesha mwamini kumsadiki Mwenyezi Mungu, kila kitu alichokisema na alichowafunulia na ambacho Kanisa Takatifu lawataka wakisadiki kwa sababu Mungu ndiye ukweli wenyewe. Kwa imani mwanadamu hujitoa nafsi yake yote kwa Mwenyezi Mungu, hutafuta kujua na kufanya mapenzi ya Mungu. Mwenye haki ataishi kwa imani na kwamba, imani hai hutenda kazi kwa upendo; na imani bila matendo hiyo imekufa. Imani inapaswa kusimikwa katika matumaini na mapendo ili kuweza kuunganika vyema na Kristo Yesu. Imani inapaswa kuungamwa, kutangazwa na kushuhudiwa. Rej. KKK 1814-1816. Matumaini ni fadhila ya Kimungu inayowawezesha waamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele kwa kutumainia ahadi za Kristo Yesu na kutegemea, siyo nguvu zao wenyewe, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu, kwa sababu Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika utekelezaji wa ahadi zake. Kwa njia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, waamini wanaweza kuhesabiwa haki kwa neema yake ili wapate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama tumaini lao.

Fadhila za Kimungu: Imani, Matumaini na Mapendo
Fadhila za Kimungu: Imani, Matumaini na Mapendo

Fadhila ya matumaini inajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Matumaini hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na mapendo. Matumaini ya Kikristo yanakita mizizi yake katika Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Matumaini ni “nanga ya roho”, hakika na thabiti; ni silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu. Matumaini ni fadhila ya Kikristo inayojikita katika unyenyekevu na nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari ya maisha, licha ya vikwazo na magumu yaliyopo. Matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayawezi kumdanganya mwamini kwani Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika kutekeleza ahadi zake. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya furaha na amani mioyoni mwa waja wake. Rej. KKK 1817-1821.

Papa Mstaafu Benedikto XVI alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti
Papa Mstaafu Benedikto XVI alikuwa ni mtu mwenye imani thabiti

Mapendo ni fadhila ya Kimungu inayomwezesha mwamini kumpenda Mwenyezi Mungu kuliko vitu vyote, kwa ajili yake Mwenyewe; jirani kama wanavyojipenda wenyewe, kwa ajili ya mapendo ya Mungu. Yesu aliyafanya mapendo kuwa ni Amri mpya. Upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake umejionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Pasaka. Mtume Paulo katika utenzi wake kuhusu upendo anasema: “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.” 1Kor13:4-8. Matunda ya upendo ni furaha, amani, huruma; upendo unadai ukarimu na kuonyana kidugu; upendo ni wema; hukuza hali ya kupokeana; hubaki huru bila ya kujitafutia faida; ni urafiki na umoja. Utimilifu wa kazi zote ni upendo. Hapo ndipo lilipo lengo. Mwaliko kwa waamini kulimbilia, ili wapate kitulizo cha ndani. Rej. KKK 1822-1829.

BXVI Fadhila za Kimungu
03 Januari 2023, 16:48