Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI: Ibada ya Misa Takatifu na Mazishi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika kipindi cha maombolezo na hatimaye, mazishi ya mwamini, wanapenda kukazia zaidi kuhusu: pumziko la milele katika amani ya Kristo Yesu, kama ambavyo Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anavyooneshwa akiwa amelala mbele ya Altare ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mama Kanisa anawahimiza waamini kutafakari juu ya umuhimu wa kushiriki katika Fumbo la Pasaka na hatimaye, waweze kuingia katika heri, maisha na uzima wa milele. Hii ni kwa sababu maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi!
Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Mama Kanisa anawaombea waamini marehemu ili watakaswe, ikiwa wanahitaji kutakaswa, kabla ya kupokelewa mbinguni, wakae na watakatifu, wakati miili yao inapobaki ardhini ikingojea kurudi kwa Kristo Yesu, Ufufuko wa wafu na uzima wa maisha ya milele. Ndiyo maana Mama Kanisa anatolea sadaka ya Misa Takatifu kwa ajili kuwakumbuka na kuwaombea marehemu, pia Mama Kanisa anasali na kuwaombea marehemu kusudi wapate msaada wa maisha ya kiroho, na waamini wanaokuwa bado hai wapate matumaini ya maisha na uzima ujao huko mbinguni.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 5 Januari 2023, kuanzia Saa 3:30 Asubuhi kwa Saa za Ulaya anaongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na baadaye Sala ya Mwisho na Ibada ya Buriani “Ultima Commendatio & Valedictio” na mazishi kufanyika kwenye Makaburi yaliyoko chini kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican “Grotte Vaticane.” Ibada hii ya Misa Takatifu inahudhuriwa rasmi na ujumbe kutoka Italia, Ujerumani na Makanisa ya Kikristo, bila kusahau umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia na wale wanaofuatilia tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Mwili wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI utatolewa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican saa 2:45 na kuwekwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, tayari kwa Ibada ya Misa Takatifu, wakati wote huo, waamini watakuwa wanasali Rozari Takatifu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake mwanana, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala, lakini zaidi kwa njia ya tafakari ya Rozari Takatifu. Baba Mtakatifu anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa ufunuo wa upendo na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapomsindikiza Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwenye usingizi wa amani.
Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa mahubiri, huku akiwa anaambatana na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali. Mara baada ya Misa Takatifu na Sala ya Mwisho na Ibada ya Buriani, Jeneza la mbao la mwili wa Baba Mtakatifu Mtakatifu Benedikto XVI, utakaokuwa umetumbukizwa kwenye sanduku la chuma likiwa limepigwa mihuri ya: Wahudumu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Chumba cha Kitume, Nyumba ya Kipapa na Ofisi ya Liturujia za Kipapa na kufungwa litapelekwa kwenye Makaburi yaliyoko chini ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro “Grotte Vaticane” kupitia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Maziko kama kawaida yatafanyika kwa faragha. Hayati Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI hatazikwa na Fimbo la Kiaskofu na badala yake ndani ya sanduku kutakuwemo sarafu za wakati wa uongozi wake, waraka unaosimulia kwa ufupi uongozi wake pamoja na Pallio Takatifu.
Itakumbukwa kwamba, Pallio takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachotengenezwa na manyoya ya kondoo wachanga; na kinavaliwa mabegani na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo makuu ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapatriaki. Kimsingi Pallio Takatifu ni kielelezo cha Kristo Mchungaji Mwema anayeyamimina maisha kwa ajili ya Kondoo wake; ni alama ya umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro; dhamana na utume wa Maaskofu wakuu na Mapatriaki kuwa ni wachungaji wema, tayari kujisadaka na kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni alama ya mshikamano wa kiimani na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Haya ni Mapokeo ambayo yamekuwepo ndani ya Kanisa tangu karne ya nne, Maaskofu wakuu walipokuwa wanafika mjini Roma, ili kukabidhiwa Pallio Takatifu. Mtakatifu Paulo wa sita, kwenye miaka 1970 alifanya mabadiliko makubwa kiasi kwamba, Pallio Takatifu wanapewa Maaskofu wakuu na Mapatriaki tu na wala sio tena alama ya heshima. Ikaamriwa kwamba, Maaskofu wakuu watakuwa wanapokea Pallio takatifu wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba ya imani, tarehe 29 Juni ya kila mwaka.
Maana ya Pallio Takatifu imeendelea kuboreka kutoka karne hadi karne kwani kwa mara ya kwanza, ilionesha yule Mwanakondoo aliyepotea na kwamba, Askofu mkuu, kielelezo cha mchungaji mwema, alikuwa anambeba mabegani mwake, upande wa kushoto. Pallio ambayo inavaliwa sasa na: Papa, Maaskofu wakuu na Mapatriaki imeongezewa misalaba mitano, alama ya madonda matano ya Yesu, Mkombozi wa Dunia. Alama ya misumari mitatu ni ile iliyotumika kumtundika Yesu Msalabani, mara mikono na miguu yake, ikafungwa kwa misumari. Itakumbukwa kwamba, kuanzia mwaka 2015 Maaskofu wakuu walioteuliwa, pale inapowezekana wanashiriki Ibada ya Misa Takatifu na Baba Mtakatifu, lakini, Pallio Takatifu watavishwa majimboni mwao na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi husika. Lengo ni kuwashirikisha watu wa Mungu wanaounda Jimbo kuu, wakiwa wameungana na Maaskofu mahalia, kushuhudia Askofu wao mkuu akivishwa Pallio Takatifu. Mkazo unawekwa kwenye umoja wa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu, Maaskofu mahalia pamoja na waamini wote katika ujumla wao.