Vijana Wakatoliki Wanatumwa Kutangaza na Kushuhudia Upendo wa Mungu Kwa Mataifa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 15 Desemba 2022 amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa Chama cha Kitume cha Vijana Wakatoliki Italia, “L’Azione Cattolica Italiana, ACR” pamoja na viongozi na walezi wao wanaoshiriki kikamilifu katika mchakato wa makuzi yao: kiutu na kikristo. Mwaka 2022, Chama cha Kitume cha Vijana Wakatoliki Italia, “L’Azione Cattolica Italiana” kinaongozwa na kauli “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Mt 28:19. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amefafanua sehemu hii ya Injili inayowataka wafuasi wake kuwa ni wamisionari kwa watu wote wa Mataifa, ili kuwashirikisha upendo na furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kama Jumuiya ya waamini wanatumwa kuwa ni mashuhuda wa upendo wa Kristo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Vijana wasiogope kujitosa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, Mwana wa Mungu kwa kutumia kikamilifu karama na mapaji waliokirimiwa na Roho Mtakatifu katika maisha yao.
Baba Mtakatifu anakitaka Chama cha Kitume cha Vijana Wakatoliki Italia, kujikita katika mchakato wa umisionari, kwa kusimama na kutembea tayari kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa. Kamwe, wasibweteke na kudumaa kwa kula “Bata kwa mrija.” Vijana wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kukutana na kutazamana na jirani zao, ili kujenga urafiki wa kijamii, utakaowawezesha vijana kumfuasa Kristo Yesu, ili hatimaye, waweze kugundua upendo na kuonja furaha yake ya daima, huku wakijitahidi kuwa watu wema na wakarimu, chachu ya matumaini katika maisha yao, inayowawezesha kukua na kukomaa huku wakiwa huru na vijana wenye furaha. Vijana wanatumwa kama Jumuiya ya waamini, ili kuondokana na ubinafsi na choyo, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani zao. Vijana watambue kwamba, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alitoa upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; watu ambao wanaangaliwa na walimwengu “kwa jicho la kengeza.”
Baba Mtakatifu anawataka vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa amani kwa njia ya sala zao na kwamba, wanaweza kufanya mambo makubwa. Kamwe vijana wasiogope kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kwani Kristo Yesu yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali; wakati wa raha na starehe, au wakati wa shida na hali ya kukata tamaa. Sherehe za Noeli kwa sasa zinaanza kubisha hodi, Neno wa Mungu anazaliwa ulimwenguni ili kuwakirimia waja wake nguvu ya kusonga mbele, huku akiwashika mkono na kutembea pamoja nao, ili kuwasaidia kugundua maana ya kutembea kwa pamoja, kwa kuwakirimia nguvu wakati wa shida na magumu ya maisha; aweze kuwashika mkono na kuwanyanyua tena baada ya kuteleza na kuanguka; kuwalinda na kuwatunza nyakati za dhoruba na mawimbi mazito ya bahari, kwa sababu Mwenyezi Mungu anapenda kuwa ni rafiki mwaminifu kwa waja wake; rafiki ambaye vijana wanaweza kumtumainia. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuhakikisha kwamba, wanatumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Sherehe za Noeli ni muda muafaka wa kuwa ni mashuhuda wa udugu na wajenzi wa Injili ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo!