Tafuta

Sikukuu ya Watoto Mashahidi wa Imani: Lindeni: Utu, heshima na haki msingi za watoto sehemu mbalimbali za dunia. Sikukuu ya Watoto Mashahidi wa Imani: Lindeni: Utu, heshima na haki msingi za watoto sehemu mbalimbali za dunia. 

Sikukuu ya Watoto Mashuhuda wa Imani: Lindeni: Utu, Heshima na Haki Msingi za Watoto

Papa Francisko kwa namna ya pekee kabisa, amewakumbuka na kuwaombea watoto wote wanaoteseka kutokana na kunyanyaswa utu na heshima yao; watoto ambao maisha yao yanasiginwa kwa baa la njaa la vita. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma apende kuwajalia waja wake nguvu, ari na mwamko wa kuwalinda na kuwategemeza. Haki, utu na heshima za watoto zilindwe.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 28 Desemba anaadhimisha Sikukuu ya Watoto Mashuhuda wa imani kwa kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi kusali kwa ajili ya kuwaombea watoto wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia: Kwa kutolewa mimba kabla hawajazaliwa kutokana na watu kumezwa na utamaduni wa kifo; kwa kuteseka kutokana na: Umaskini, baa la njaa na magonjwa na wale ambao wanabebeshwa silaha na kutumwa mstari wa mbele kama chambo kwenye mapigano. Sikukuu ya Watoto Mashahidi waliouwawa na Mfalme Herode kwa hofu ya kupoteza kiti chake za kifalme, baada ya kuambiwa kwamba, Kristo Yesu, Mfalme wa Mataifa amezaliwa mjini Bethlehemu ilianza kuadhimishwa tangu Karne ya tano. Hata katika ulimwengu mamboleo bado kuna sauti ya watoto wanaoteseka na kuuwawa kutokana na vita, ghasia, mipasuko ya kijamii; uchu wa mali, madaraka pamoja na tabia ya kutaka kujimwambafai. Tangu mwanzo, Mama Kanisa amewaangalia watoto hawa kama mashuhuda wa Fumbo la Umwilisho, watoto ambao hata kama hawakubahatika kumwona Kristo Yesu, lakini walikirimiwa Ubatizo wa Damu. Kumbe, wao ni mashuhuda wa Kristo Yesu kwa njia ya sadaka ya maisha yao. Mama Kanisa daima anafundisha kwamba, kifodini ni sadaka kubwa ambayo Mwenyezi Mungu hupenda kuwakirimia waja wake.

Watoto ni waathirika wakuu wa vita na mipasuko ya kijamii
Watoto ni waathirika wakuu wa vita na mipasuko ya kijamii

Sikukuu ya Watoto mashuhuda wa imani inafuatana na mashuhuda wa imani kama vile: Mtakatifu Stefano shahidi wa kwanza na Mwinjili Yohane ambao daima wamesimama kidete kutangaza na kushuhudia: Imani, Matumaini na Mapendo; daima wakitetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 28 Desemba 2022 kuhusu: Sherehe ya Noeli, amewakaribisha waamini kutafakari pamoja na Wasalesian wa Don Bosco, Mama Kanisa anapoanza kuadhimisha Jubilei ya Miaka 400 tangu Mtakatifu Francisko wa Sales, Askofu, Mwalimu wa Kanisa na Msimamizi wa Waandishi wa Habari alipofariki dunia tarehe 28 Desemba 1622. Papa Alexander VII akamtangaza kuwa Mwenyeheri 8 Januari 1662 na hatimaye Mtakatifu tarehe 19 Aprili 1665. Papa Leo wa XIII kunako mwaka 1887 akamtangaza kuwa ni Mwalimu wa Kanisa. Kwa namna ya pekee kabisa, amewakumbuka na kuwaombea watoto wote wanaoteseka kutokana na kunyanyaswa utu na heshima yao; watoto ambao maisha yao yanasiginwa kwa baa la njaa la vita. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, apende kuwajalia waja wake nguvu, ari na mwamko wa kuwalinda na kuwategemeza.

Watoto ni waathirika wa mabadiliko ya tabianchi
Watoto ni waathirika wa mabadiliko ya tabianchi

“Mungu Baba Mwenyezi, ambaye kwa mahubiri ya Watoto Mashuhuda wa imani wasio na hatia, leo wamekiri si kwa maneno, bali kwa kifodini; ili imani yetu tunayoitangaza kwa ndimi zetu, ishuhudiwe kwa maadili na utu wema.” “Deus, cuius hodierna die præcónium Innocéntes Mártyres non loquéndo, sed moriéndo conféssi sunt: ómnia in nobis vitiórum mala mortífica; ut fidem tuam, quam lingua nostra lóquitur, étiam móribus vita fateátur.” Baba Mtakatifu Francisko katika Salam na Baraka zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” wakati wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli tarehe 25 Desemba 2022 amegusia kuhusu: Kristo Yesu, Nuru ya Mataifa, “kwa Kiebrania: עִמָּנוּאֵל, Immanuel, yaani, "Mungu pamoja nasi.” Ni Noeli ya Amani, lakini kwa bahati mbaya walimwengu wanaendelea kuishi katika janga la ukosefu wa amani, watu wanapekenyuliwa na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kutokana na biashara haramu ya silaha duniani. Noeli ya Kristo Yesu iwe ni kielelezo cha upendo na mshikamano, ishara ya huruma, upendo na unyenyekevu wa Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Noeli ya kweli ni ile inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu mhusika mkuu na amani ya kweli kwa kumwangalia Mtoto Yesu aliyezaliwa mjini Bethlehemu, “Mtoto aliyezaliwa kwa ajili yetu.” Katika uchanga na udogo wake, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wawe na ujasiri wa kuwaona na kuwatambua watoto kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaoendelea kuteseka kutokana na ukatili wa binadamu. Wawaangalie na kuwatambua watoto wenye kiu ya haki na amani duniani.

Kuna watoto wengi ambao wameathirika kwa utapiamlo wa kutisha
Kuna watoto wengi ambao wameathirika kwa utapiamlo wa kutisha

Ulinzi wa utu, heshima na haki msingi za mtoto ni dhamana na wajibu wa kisiasa na kijamii na Kanisa linatambua haki hizi msingi katika maisha na utume wake; kama ilivyo kwa “Tamko la Haki za Mtoto la Mwaka 1959” na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za Mtoto wa Mwaka 1989 na kama haki hizi zinavyofafanuliwa kwa kina katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuwawezesha watoto kukua na kukomaa katika mazingira bora, rafiki na salama katika maisha na utu wao. Hawa ni watoto walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, walipewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Unyenyekevu wa watoto ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wanaotaka kuingia kwenye Ufalme wa Mungu. Lakini, Kristo Yesu anaonya kwamba, ole wake atakayemkwaza mtoto mdogo, itabidi afungiwe jiwe la kusagia shingoni na kuzamishwa baharini! Changamoto pevu kwa wakati huu ni ulinzi wa utu, heshima na haki msingi za watoto na vijana; ukuaji wao makini na salama; furaha na matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kulinda na kudumisha haki msingi za watoto, hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, watoto wanapata elimu bora na huduma msingi ya afya hasa kwa wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Watoto hawa wamejikuta wakitumbukia na kutumbukizwa katika wimbi la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbalimbali za dunia.

Mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu ni muhimu
Mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu ni muhimu

Matokeo yake ni kwamba, baadhi yao wana nyanyaswa, wanadhulumiwa na kutumbukizwa katika biashara ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo! Kuna watoto wanaofariki dunia kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; magonjwa yanayoweza kuzuilika na kutibika pamoja na ujinga! Watoto hawa ni mboni ya jicho la Kristo Yesu! Kanisa litaendelea kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, haki za watoto zinalindwa na kuheshimiwa na kwamba, watoto wanapewa haki ya kufurahia utoto wao katika mazingira: salama, ya amani na utulivu na kwamba, watoto hawa wasipokwe furaha na matumaini yao kwa sasa na kwa siku za usoni! Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za Jumla kwa Mwezi Novemba 2022, katika ujumbe wake kwa njia ya video, inayosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea watoto wanaoteseka kwa sababu mbalimbali; watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wahanga wa vita na wale wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo; wote hawa wapewe fursa ya kupata elimu na kuonja upendo kutoka katika familia zao. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, katika ulimwengu mamboleo kuna watoto wanaoteseka na kuishi katika mazingira magumu na hatarishi mithili ya watumwa. Hawa ni watoto wenye majina, sura na utambulisho ambao wamepewa na Mwenyezi Mungu na wala si namba au idadi yao inayowafanya watu kuwavutia hisia.

Watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya nyanyaso za aina zote
Watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya nyanyaso za aina zote

Watu wanasahau dhamana na wajibu wao kwa watoto hawa na matokeo yake, wanawanyanyasa, wanawanyonya na kuwadhulumu, kiasi cha kupokwa haki yao ya kucheza, kusoma na kuwa na ndoto ya maisha bora zaidi. Hawa ni watoto ambao kamwe hawafurahii hata kidogo fukuto na maisha na upendo wa kifamilia. Kwa mtoto yoyote anayedhulumiwa, anayetelekezwa, bila kupelekwa shule au kupatiwa matibabu muafaka ni kilio kinachopaa mbinguni kwa Baba wa milele na hii ni aibu kwa miundo mbinu ambayo imejengwa na watu wazima na kwamba, kutelekezwa kwa watoto katika mazingira magumu na hatarishi ni makosa ya familia na jamii katika ujumla wake. Kimsingi watoto wanayo haki ya kupata elimu, kupendwa na watambue kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu kamwe hajawasahau. Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali na kuwaombea watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, yatima na wahanga wa vita. Wawe na uhakika wa kupata elimu na fursa ya kufurahia maisha na upendo wa kifamilia. NB: Radio Vatican inamtakia heri na baraka tele Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S. anayeadhimisha kumbukizi ya miaka 59 tangu kuzaliwa kwake. Anabainisha kwamba chimbuko la wito wake wa Kipadre ni upendo katika huduma inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, Mama wa fadhila zote, umoja na mshikamano wa kidugu!

Watoto Mashuhuda
28 December 2022, 17:37