Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani Desemba 3, 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba na kwa mwaka huu 2022 kauli mbiu inayonogesha maadhimisho haya: "Suluhisho la Mabadiliko kwa Maendeleo Jumuishi: Nafasi ya Ubunifu katika Kuchagiza Dunia fikivu yenye Usawa. Siku hii ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1992 na azimio la 47/3. Lengo kuu ni kukuza uelewa wa masuala ya ulemavu na kuhamasisha uungwaji mkono kwa ajili ya utu, heshima, haki, ustawi, mafao na maendeleo wa watu wenye ulemavu. Pia inalenga kuongeza ufahamu wa mafanikio yatakayopatikana kutokana na ushirikiano wa watu wenye ulemavu katika kila nyanja ya maisha ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Siku hii mjini Vatican imeadhimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, iliyoongozwa na Askofu mkuu Giuseppe Baturi, wa Jimbo kuu la Cagliari, ambaye pia ni Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI.
Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho haya ametoa ujumbe maalum na baadaye amekutana na kuzungumza na watu wenye ulemavu. Katika hotuba yake amekazia zaidi: Utu, heshima na mchakato wa ujenzi wa jumuiya shirikishi na kwamba, Jumuiya za Kikristo ziwe ni mahali ambapo watu wenye ulemavu watajisikia nyumbani kwa kupendwa, kukaribishwa na kuthaminiwa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ameendelea kuwa mstari wa mbele kwa kusimama kidete kulinda, kuendeleza na kudumisha, utu na heshima ya binadamu na kwamba, huu ni wajibu fungamani wa Kanisa na hasa katika kipindi hiki cha Majilio. Walemavu katika shida na mahangaiko yao, haki zao msingi zinapaswa kulindwa. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa na Uso wa huruma kwa wale wote waliokuwa wametengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.
Jumuiya za Kikristo zinapaswa kujipambanua katika ujenzi wa ujirani mwema, kwa kuzingatia mahitaji msingi kwa watu wenye ulemavu, haki zao msingi pamoja na kuwahakikishia kwamba wanapata pia huduma za maisha ya kiroho, ili hata wao katika ulemavu wao, waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Ni wajibu wa watu wa Mungu kujenga jumuiya shirikishi kwa kuondokana na mifumo yote ya ubaguzi, kama kielelezo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu na ushirika unaosimikwa katika toba na wongofu wa ndani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya za Kikristo zitajipambanua katika mchakato wa ujenzi wa jamii shirikishi, hawa ndio wale ambao Kristo Yesu anawapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake. Walemavu waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu; wawe ni ishara ya matumaini katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika utu na udugu wa kibinadamu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa siku hii amesema ulimwengu unakabiliwa na msururu wa majanga ambayo yanaathiri watu wenye ulemavu hivyo kunahitajika kupatikane suluhu za mageuzi ili kuwezesha kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, SDGs na kutomwacha mtu yeyote nyuma. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema suala la mageuzi linahitaji mafungamano na ushirikiano mkubwa wa sekta ya umma na binafsi ili kuandaa sera na mikakati ya pamoja kwa kushirikiana na watu wenye ulemavu. “Msingi wa ushirikiano huu lazima uwe na ushirikishwaji kamili wa watu wenye ulemavu ili uweze kujumisha utofauti wao katika michakato yote ya kufanya maamuzi. Ubunifu na teknolojia zinaweza kuwa zana zenye nguvu za kuwajumuisha” amesema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Bwana Antonio Guterres ameeleza kwamba, watu wenye ulemavu wakijumuishwa wanaweza kuongeza ufikiaji wa mawasiliano, elimu, na hivyo kupata fursa ya kujifunza mambo msingi katika maisha. Na wanaweza kufungua maeneo mengine mapya kwa watu wenye ulemavu kushiriki katika nguvu kazi na jamii kwa ujumla na kwa usawa. “Lakini ili tuweze kufikia hili la kutumia vyema teknolojia, ni lazima kwanza tuondoe mgawanyiko wa kidijitali na kulinda haki za binadamu katika anga ya kidijitali. Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Kujumuisha Watu wenye Ulemavu unatoa ramani halisi ya kuendeleza ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu na kuwafikia katika kazi zote za Shirika hili. Amesema Guterres na kuongeza kwamba, “Tunafanya haya kuanzia makao makuu hadi mashinani, tunafanya kazi kutathmini, kushughulikia na kukuza ufikiwaji wa kidijitali na tunaongoza kuwa mfano wa ujumuishaji wa watu wenye walemavu.” Guterres amehitimisha ujumbe wake kwa kusema katika siku hii na kila siku, iwe ni fursa ya kushirikiana na kushikamana katika kutafuta suluhisho bunifu ili kujenga ulimwengu unaofikiwa na wenye usawa kwa wote bila ubaguzi.