Salam za Rambirambi kwa Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk kwa Kifo cha Baba Yake Mzazi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambirambi kwa Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Mkuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki la Kyiv-Halyč, nchini Ukraine kufuatia kifo cha baba yake mpendwa, Bwana Yuriy Shevchuk aliyefariki dunia tarehe 5 Desemba 2022 akiwa na umri wa miaka 79 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Baba Mtakatifu anasema, amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Mzee Yuriy Shevchuk.
Baba Mtakatifu Francisko anapenda kumhakikishia uwepo wake wa karibu katika kipindi hiki cha maombolezo kwa kuondokewa na baba yake mpendwa pamoja na wale wote wanaoomboleza msiba huu mzito. Baba Mtakatifu anapenda kuiweka roho ya Marehemu Mzee Yuriy Shevchuk mikononi mwa huruma na upendo wa Mungu. Huku akiwa ana Sali anapenda pia kuwapatia baraka zake za kitume, kwa wale wote wanaoshiriki katika msiba huu mzito!