Papa:Tuombee Caucasus&Maria aguse mioyo ili vita Ukraine viishe
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya tafakari na sala ya Malaika wa Bwana kwa waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Vatican, Dominika ya VI ya Majilio, tarehe 18 Desemba 2022, Baba Mtakatifu Francisko ameelezea juu ya wasi wasi wake kuhusu hali halisi iliyoundwa huko kwenye mkondo wa Lachin, katika Caucasus Kusini. Kwa namna ya pekee wasi wasi wa hali halisi ya kibinadamu kwa watu, ambao wanayo hatari mbaya sana wakati wa msimu huu wa baridi. Kwa maana hiyo:“Naomba kila mmoja anayehusika ajitolee kutafuta suluhisho za amani kwa manufaa ya wananchi”.
Kusali kwa ajili ya amani ili vurugu zikome nchini Peru
Baba Francisko aidha ameomba kusali kwa ajili ya amani ili vurugu katika nchi ya Peru ziishe na kuanza kuchukua njia ya majadiliano katika kushinda migogoro ya kisiasa na kijamii ambayo inatesa watu. Baba Mtakatifu amewasalimia wote ambao wamefika Roma kuanzia watu wa Italia na kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa namna ya pekee amewataja waamini kutika California, na wale wa Madrid; kama vile pia makundi ya Praia ya bahari, Catania, Caraglio na Parokia moja ya Roma ya Watakatifu Mashahidi wa Kwanza.
Maria aguse mioyo ya wale wanaoweza kusimamisha vita Ukraine
Baba Mtakatifu akiendelea amesema “kwa Bikira Maria ambaye Liturujia inatualika kutafakari katika Dominika ya Nne ya Majilio tumuombe aguse mioyo ya wale ambao wanaweza kusimamisha vita nchini Ukraine. Tusisahau mateso ya wale watu, kwa namna ya pekee watoto, wazee na watu wagonjwa. Tusali” amesisitiza Papa mara mbili. Hatimaye amewatakia wote Dominika njema na mchakato mwema wa safari ya hatua ya mwisho ya Majilio. Tafadhali wasisahau kusali kwa ajili yake. Amewatakia mlo mwema na kuwaaga wote.