Papa Francisko:Salamu kwa wote na upyaisho wa amani kwa Ukraine
Na Angella Rwezaula;- Vatican.
Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Jumatatu tarehe 26 Desemba ambapo Mama Kanisa anamkumbuka Mfiadini wa Kwanza mtakatifu Stefano, Papa Francisko akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican amesema, katika hali ya kiroho ya furaha na utulivu wa Noeli Takatifu, anawasalimu wote waliokuwapo na wale waliokuwa wakifuatilia kupitia vyombo vya mawasiliano ya kijamii.
Baba Mtakatifu Francisko kwahiyo amepyaisha salamu zake na wito wa amani: amani katika familia, amani katika jumuiya za parokia, na za kitawa, amani katika harakati na vyama vya kikanisa, amani kwa wale watu ambao wanasumbuliwa na vita, na amani kwa ajili ya nchi pendwa na inayotesekana Ukraine.
Baba Mtakakatifu Francisko ameona bendera nyingi za Ukraine zikipepea katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na kwamba zipo na hivyo tuombe amani kwa ajili ya watu hao wanaoteseka. Aidha ameeleza alivyopokea ujumbe mwingi kwa siku hizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa kuwa hawezi kujibu moja baada ya nyingine, amependa kueleza shukrani zake hasa kwa zawadi ya sala wanazomwombea. Hatimaye amewatakia Siku kuu njema ya Mtakatifu Stefano na kama kawaida amewambia wasisahau kusali kwa ajili yake.