Tafuta

Papa Francisko tarehe 12 Desemba 2022 amekutana na wajumbe wa  'Amiti' Judeo-Chretienne de France', kumbukizi ya Miaka 75 ya Majadiliano ya Kidini. Papa Francisko tarehe 12 Desemba 2022 amekutana na wajumbe wa 'Amiti' Judeo-Chretienne de France', kumbukizi ya Miaka 75 ya Majadiliano ya Kidini. 

Papa Francisko Majadiliano ya Kidini ni Kwa Ajili ya: Haki, Amani, Ustawi na Mafao ya Wengi

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Chama cha Urafiki Kati ya Wayahudi na Wakristo Nchini Ufaransa kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwao, mwaliko wa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini. Mwana historia Jules Isaac amechangia sana mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Imani, amani na matumaini ni fadhila ambazo zinapata chanzo na utimilifu wake mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini binadamu amedhaminishwa tunu hizi ili kuzifanyia kazi katika maisha yake hapa duniani; kwa kuchagua na kuambata mapenzi ya Mungu, ili hatimaye, aweze kusimama kidete kulinda na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa kujichotea: hekima, amana na utajiri wa Neno la Mungu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Wayahudi yataweza kuzaa matunda mengi ya ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Hija ya pamoja katika majadiliano ya kidini ni muhimu sana kwa ajili ya: Ustawi, maendeleo na mafao ya waamini wa dini hizi mbili, ili kufahamiana, kuheshimiana na kwa pamoja, kuweza kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu! Huu ni mchakato wa ujenzi wa fadhila ya upendo wa kidugu kati ya watu kwani Mungu ni asili na hitimisho la upendo. Tamko la Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano na waamini wa dini mbalimbali duniani, “Nostra aetate” ni msingi wa mahusiano mema ambayo yameendelea kujengeka na kuimarika kama ndugu wamoja kwa kutambua kwamba, hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Majadiliano ya kidini ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Urithi mkubwa ambao waamini wa dini mbalimbali wanaweza kuufanya katika maisha na utume wao ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya upendo kwa Mungu na jirani. Kizazi baada ya kizazi kinapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapaswa kupendwa kwa moyo wote, kwa roho yote na kwa nguvu zote. Upendo huu kimsingi, unapaswa pia kuelekezwa kwa jirani ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kumekuwepo na mafanikio makubwa yanayofumbata amana na utajiri wa maisha ya kiroho; uelewa na udugu wa kibinadamu unaopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya chuki na uhasama kwa Wayahudi; kwa kujikita katika mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya: haki, amani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Waamini wa dini mbalimbali wanao wajibu na dhamana ya kulinda uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kukuza na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini pamoja na kujikita katika mchakato wa kutunza mazingira nyumba ya wote! Ikumbukwe kwamba, Wayahudi na Wakristo wanao utajiri na amana ya maisha ya kiroho pamoja na mambo mengi mazuri wanayoweza kushirikiana kwa pamoja kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

Kumbukizi ya Miaka 75 ya Majadiliano ya Kidini nchini Ufaransa
Kumbukizi ya Miaka 75 ya Majadiliano ya Kidini nchini Ufaransa

Ni katika muktadha huu Chama cha “Amitié Judéo-Chrérienne de France” (AJCF) yaani “Chama cha Urafiki Kati ya Wayahudi na Wakristo Nchini Ufaransa” kinaadhimisha kumbukizi ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwake. Chimbuko la urafiki huu ni kutokana na maangamizi makubwa dhidi ya Wayahudi wa Ulaya: Holocaust, kwa lugha ya Kiebrania Shoah השואה) yalikuwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wayahudi milioni 5-6 kutoka Barani Ulaya wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kati ya miaka 1940 na 1945. Mauaji hayo yalipangwa na kutekelezwa na serikali ya Ujerumani chini ya Adolf Hitler kwa msaada wa serikali za nchi zilizofungamana na Ujerumani au zilizokuwa chini ya jeshi la Ujerumani. Mwaka 1946 Mwana historia Jules Isaac (1877-1963) akakamilisha utunzi wa Kitabu kuhusu Yesu na Israeli, na kufungua ukurasa mpya wa majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakristo. Chama cha Urafiki Kati ya Wayahudi na Wakristo Nchini Ufaransa tarehe 5 Agosti 1947 kikaadhimisha Mkutano mkuu wa Baraza la Kimataifa kati ya Wayahudi na Wakristo huko Seeliberg nchini Uswis. Mkazo ukawekwa kuhusu umuhimu wa mafundisho ya dini katika ngazi mbalimbali ili kuondokana na chuki, uhasama na dhuluma dhidi ya Wayahudi. Waamini wanapaswa kupatiwa tafsiri halali ya Vitabu Vitakatifu, ili kujenga upendo, mshikamano na maridhiano kati ya watu, badala ya watu wachache kutumia Vitabu Vitakatifu kwa ajili ya masilahi yao binafsi dhidi ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Majadiliano ya kidini yakoleze haki, amani na maendeleo ya wengi
Majadiliano ya kidini yakoleze haki, amani na maendeleo ya wengi

 

Wajumbe wakakazia muhimu wa kusoma historia ya Biblia na Historia ya Wayahudi. Kanuni 10 zilizochapishwa na Mkutano huu, zimekuwa ni rejea ya majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakristo kabla ya Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 12 Desemba 2022 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Chama cha “Amitié Judéo-Chrérienne de France” (AJCF) yaani “Chama cha Urafiki Kati ya Wayahudi na Wakristo Nchini Ufaransa” kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwao, changamoto na mwaliko kwa Wayahudi na Wakristo kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini. Mwana historia Jules Isaac amechangia sana mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wayahudi na Wakristo na kubahatika kukutana na kuzungumza na Papa Pio XII na Mtakatifu Yohane XXIII. Kitabu chake ni amana na utajiri kwa Wayahudi na Wakristo, kwani kinawahimiza waamini wa dini hizi mbili kutambuana, kushirikiana na kuheshimiana, huku wakiendelea kuchota amana na utajiri wa Kibiblia na Kitaalimungu ili kunogesha mchakato wa majadiliano ya kidini yatakayowawezesha waamini wa dini mbalimbali kujisikia wamoja licha ya tofauti zao msingi.

Upendo kwa Mungu na jirani usimikwe katika uhalisia wa maisha
Upendo kwa Mungu na jirani usimikwe katika uhalisia wa maisha

 

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, miaka 75 si haba, ni muda  wa kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha kupiga hatua hii kubwa, ingawa bado kuna mengi ya kutekelezwa. Kumbe, waamini wa dini zote wanapaswa kuwa na ujasiri na kuendelea kudumu katika njia ya majadiliano ya kidini, jambo linalohitaji moyo thabiti. Waamini wajenge utamaduni wa mshikamano hasa katika nyakati hizi ambamo ubinafsi na tabia ya watu kutaka kujifungia katika ubinafsi inazidi kupamba moto! Bado kuna chembe za chuki dhidi Wayahudi, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe ushirikiano wa waamini wa dini mbalimbali husaidie kuimarisha na kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu.

Majadiliano ya Kidini
13 December 2022, 15:12