Papa Francisko Kumbukizi Ya Miaka 53 ya Daraja Takatifu ya Upadre 13 Desemba 1969
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Kitaifa la Vipofu na Watu wenye Ulemavu wa Kuona Nchini Italia, “Consiglio Nazionale dell'Unione Italiana Ciechi e Ipovedenti” linampongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu kwa kufanya kumbukizi ya Miaka 53 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969 Mama Kanisa anapoadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Lucia, Bikira na Shahidi, Mlinzi na Mwombezi wa Vipofu na Watu wenye Ulemavu wa kuona. Baba Mtakatifu Francisko alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 huko Flores, Buenos Aires, nchini Argentina. Mwaka 2022 anatimiza miaka 86 tangu alipozaliwa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kitawa na Kikasisi, tarehe 13 Desemba 1969 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kunako mwaka 1992 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 27 Juni 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu tarehe 22 Februari 1998 na hatimaye kama Kardinali tarehe 21 Februari 2001. Tarehe 13 Machi 2013 akachaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuanza utume wake rasmi tarehe 19 Machi 2013. Hii ndiyo siri ya zawadi na fumbo la Daraja Takatifu ya Upadre linalomwezesha Baba Mtakatifu kuwa ni Kristo mwingine, “Alter Christus” kwa njia ya Daraja Takatifu ya Upadre.
Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kuwa ni mtetezi wa haki na amani; kwa kuendelea kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya: utu, heshima, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa mambo yanayokita mizizi yake katika ukweli na uwazi, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amewashukuru na kuwapongeza kwa kujitahidi kujenga na kudumisha jamii shirikishi, inayothamini utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kutembea na kuwasiliana katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, ili kujenga mazingira ambamo watu wote wanaweza kuishi kwa amani na utulivu. Baraza la Kitaifa la Vipofu na Watu wenye Ulemavu wa Kuona Nchini Italia ni nguvu imara katika mchakato wa ujenzi wa nchi ya Italia.
Mama Kanisa anatambua na kuheshimu udhaifu wa maisha ya mwanadamu na anapenda kuhakikisha kwamba, anatekeleza dhamana na wajibu wake unaosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu, amana na utajiri katika ujenzi wa jumuiya imara ya Kikanisa na jamii shirikishi, changamoto mamboleo. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, wanahitajiana na kukamilishana katika safari ya maisha yao haya duniani. Baraza la Kitaifa la Vipofu na Watu wenye Ulemavu wa Kuona Nchini Italia, “Consiglio Nazionale dell'Unione Italiana Ciechi e Ipovedenti” lilianzishwa rasmi tarehe 26 Oktoba 1920 huko mjini Genova, Kaskazini mwa Italia. Katika kipindi chote hiki, Baraza limekuwa mstari wa mbele kusimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za watu wenye ulemavu wa macho, ili kwa kushirikiana na kushikamana na wananchi wengine, waweze kujikita katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu wote. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka wajumbe wote chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Lucia, Bikira na Shahidi na hatimaye, kuwatakia heri na baraka katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli na Mwaka Mpya 2023.