Papa Francisko Awaombea Wafungwa Msamaha Wakati wa Noeli 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Siku ya Kuombea Amani Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Paulo VI, tarehe Mosi, Januari 1968 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Theotokos inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe Mosi Januari ya kila mwaka. Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa tarehe 11 Aprili 1963, mwaka 2023, Kanisa linajiandaa kuadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu kuchapishwa kwake. Mtakatifu Yohane XXIII anasema, amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Kila mwanadamu ni nafsi yenye haki na wajibu. Hii ni haki ya kuishi na kuwa na maisha na haki za tunu za kimaadili na kiutamaduni. Kutokana na haki ya asili, watu wote wana haki ya kushiriki ukuaji wa ustaarabu; na kwa hiyo ni lazima kila mtu aweze kupata elimu nzuri ya msingi, na mafunzo ya ufundi na ya elimu ya juu yanayolingana na kiwango cha maendeleo ya elimu cha nchi yake. Ni lazima kila bidii na juhudi zifanywe ili kila mtu aweze kufikia viwango vya juu vya elimu, kadiri iwezekanavyo kulingana na karama zake, na kuchukua dhima na majukumu katika jamii zinazolingana na karama hizo za maumbile na ujuzi alioupata. Kuna haki ya kumwabudu Mungu kulingana na maongozi ya dhamiri nyofu. “Tumezaliwa kwa ajili ya kumpa Mungu aliyetuumba heshima inayompasa, iliyo ya haki, na kumtambua na kumfuata yeye peke yake. Nasi tumefungamana na kushikamana na Mungu kwa njia ya kifungo hicho cha utauwa, ambacho hata jina la dini yenyewe linatokana nacho” na hiki ni kielelezo cha ukweli.
Haki ya mtu kuchagua hali ya kuishi anayoipenda zaidi. Haki ya kuwatunza na kuwalea watoto kwanza kabisa ni juu ya wazazi wao. Haki zinazohusu uchumi lazima ziungane na haki ya kufanya kazi katika hali na mazingira visivyoathiri uzima wa mwili au maadili ya mtu, wala visivyodhuru mchakato wa kukua kwa vijana hadi wafikie ukomavu wa utu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani kwa kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ujumbe Baba Mtakatifu kwa ajili ya Siku ya Kuombea Amani Duniani hutumwa kwa wakuu wa nchi na Jumuiya ya Kimataifa na pia ujumbe huu huonesha dira na mwelekeo wa utendaji wa shughuli za kidiplomasia zitakazotekelezwa na Vatican. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya 56 ya Kuombea Amani Duniani tarehe 1 Januri 2023 unanogeshwa na kauli mbiu “Hakuna mtu anayeweza kujiokoa mwenyewe. Kupambana na UVIKO-19 na kwa pamoja kujielekeza kwenye njia za amani.” Katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli 25 Desemba 2022, Baba Mtakatifu amewaandikia wakuu wa serikali na nchi mbalimbali duniani ujumbe wa heri, baraka na matashi mema katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli, akiwasihi kuonesha huruma, upendo na msamaha kwa wafungwa magerezani, kwa kuboresha mchakato wa haki msingi za binadamu sanjari na hali ya magereza yenyewe, kwa kukazia haki na nyajibu za wafungwa magerezani.
Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee kabisa: Umuhimu wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafungwa magerezani, kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa Injili sanjari na Askari wanaopaswa kuwa na ujasiri wanapotekeleza dhamana na utume wao miongoni mwa wafungwa. Hii ni dhamana inayowataka siku kwa siku kuwa ni wajenzi wa haki na wajumbe wa amani kwa kuwakumbuka wafungwa hao waliofungwa kana kwamba wamefungwa pamoja nao na kama wanadhulumiwa, basi hata wao wahisi haya madhulumu mwilini wao. Gereza ni mahali pa mahangaiko ya binadamu. Askari magereza wanapaswa kutambua uzito wa kazi na wajibu wao kwa wafungwa pamoja na familia zao wenyewe. Kufurika kwa wafungwa magerezani ni kati ya changamoto changamani kwa wakati huu, hali ambayo inachangia pia kudhohofisha maisha ya Askari magereza, kiasi hata cha kukosa imani na matumaini. Kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, wafanyakazi na wafungwa wanaishi maisha yenye hadhi na utu wa kibinadamu, vinginevyo magereza yatageuka kuwa ni nyumba za chuki na uhasama badala ya kuwa ni mahali pa kurekebisha tabia na mwenendo wa wafungwa. Baba Mtakatifu anasema inawezekana kutoa msamaha kwa wafungwa, au kwa kuwapunguzia muda wa adhabu, ili kuwawezesha wafungwa kuyaangalia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini sanjari na kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema uhuru wao. Hii ni fursa ya kuchochea moyo wa toba na wongofu wa ndani.