Tafuta

Papa:Bwana yuko nasi tusiogope sio hakimu mbaya ni wa huruma na upole

Mara nyingi tuna wazo potofu la Mungu.Sauti yake hailazimishi,lakini ni ya busara,heshima,unyenyekevu na ya upatanisho.Ni muhimu kusoma Neno la Mungu ambalo ni kama kupokea telegramu ndogo kutoka kwa Mungu.Ni uwepo hai unaotoa mwanga,nguvu,burudisho na kubadilisha maisha.

Na Angella Rwezaula; – Vatican.

Jumatano tarehe 21 Desemba 2022 zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Noeli, Baba Mtakatifu Francisko ametoa tafakari yake katika mwendelezo wa mada ya Utambuzi, kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican. Kwa maana hiyo Papa alibainisha kuwa katika mwendelezo huo utambuzi unaokaribia inakaribia kuisha, kwa yule  anayeendelea kufuatilia hadi sasa katekesi hizo anaweza labda kufikiria, kuwa mbona hili zoezi gumu ambalo ni utambuzi. Lakini kiukweli ni maisha ambayo yanakuwa magumu na ikiwa hatujifunzi kusoma, kuna hatari ya kuharibu, kuyapeleka mbele kwa manufaa yanayoishia kutudhalilisha. Katika katekesi ya kwanza tulikuwa tumeona kuwa daima, kila siku, utake usitake, tunatimiza matendo ya kufanya mang’amuzi, kwa kile tunachokula, tunacho soma, juu ya kazi na katika uhusiano. Maisha yanatuweka daima mbele ya chaguzi na ikiwa hatutimizi kwa namna ya utambuzi, mwishowe ni maisha yenyewe yanachagua kwa ajili yetu, kwa kutupelekea mahali ambamo hatukuwa tunakutaka.

Baba Mtakatifu amebainisha kwamba utambuzi lakini haufanyiki peke yakena hivyo amependa kufafanua zaidi baadhi ya msaada ambao unaweza kusaidia kufanya zoezi hilo muhimu la maisha ya kiroho, hata kama kwa namna moja au nyingine tulikwisha kutana nayo katika mchakato wa katekesi zilizotangulia. Msaada wa kwanza muhimu ni kukabiliana na Neno la Mungu na Mafundisho ya Kanisa. Haya yanatusaidia kusoma kile ambacho kinazungumza ndani ya moyo, kwa kujifunza kujua sauti za Mungu na kutofautisha na sauti nyingine, ambazo utafikiri zinapendelea umakini wetu, lakini ambazo zinatuacha mwishowe tumechanganyikiwa. Biblia inatuonya kwamba sauti ya Mungu inasikika katika utulivu, katika umakini na katika ukimya. Kwa kutoa mfano Baba Mtakatifu amesema “Tufikirie uzoefu wa nabii Elia: Bwana alizungumza si katika upepo unaopasua miamba, sio katika moto au katika tetemeko la ardhi, lakini katoka katika upepo mwanana (1Mfalme 19,11-12). Ni picha nzuri sana ambayo inatufanya kujua jinsi Mungu anavyozungumza. Kwa sababu sauti ya Mungu hailazimishi,  sauti ya Mungu ni nyeti, inaheshimu  na Papa ameongeza kusema kwamba sauti ya Mungu ni nyenyekevu na ndio kwa sababu hiyo inatoa amani. Ni katika amani tu, tunaweza kuingia kwa kina ndani mwetu binafsi na kujua shauku za dhati ambazo Bwana aliziweka katika moyo wetu.

“Na mara nyingi si rahisi kuingia katika amani hiyo ya moyo, kwa sababu sisi daima tuko bize na mambo mengi siku nzima ... Lakini tafadhali, tulia kidogo, ingia ndani yako mwenyewe. Dakika mbili, simama. Angalia moyo wako unavyohisi. Tufanye hivi ndugu, itatusaidia sana, maana katika wakati huo wa utulivu  ndipo tunasikia mara moja sauti ya Mungu inayotuambia: “Lakini angalieni, na hili, ni vyema mnalofanya... Turuhusu sauti ya Mungu ije mara moja katika utulivu. Hii ndiyo sababu anatungoja”, Papa ameongeza. Kwa mwaamini, Neno la Mungu sio kitu rahisi tu, kama  andiko la kusoma tu, lakini neno la Mungu ni uwepo wake ulio hai, ni kazi moja ya Roho Mtakatifu ambaye anatoa kitulizo, anafundisha, anatoa mwanga, nguvu, faraja na haki ya kuishi. “Kwa kusoma Biblia, kusoma kifungu kimoja au viwili vya Kibiblia ni kama telegram ndogo za Mungu ambaye anakufikia haraka moyoni. Neno la Mungu kidogo labda ninaweka chumvi ni Mbingu ya kweli iliyotangulia. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutoa mfano mwingine katika hili alikuwa ametambua vema Mtakatifu mkubwa na mchungaji, Askofu wa Milano Ambrosi ambaye alikuwa ameandika kuwa: “Ninaposoma Andiko Takatifu, Mungu anarudia kutembea  katika mbingu ya dunia” (barua 49,3). Kutokana na Biblia sisi tunafungua Mlango wa Mungu ambaye anatembea. Inavutia…”

Kwa hiyo Papa amesema uhusiano huo kiukweli na Biblia, na andiko na Injili inapelekea kuishi na uhusiano wa kweli na Bwana Yesu, kwa kutokuwa na woga kwa hilo. Moyo unazungumza katika moyo na huo ndio msaada muhimu na sio wa kudharau. Mara nyingi tunaweza kuwa na wazo potofu la Mungu, kwa kumfikiria kama hakimu mkorofi, hakimu mkali, tayari wa kutoa maagizo. Kinyume chake Yesu anatuonesha wazo la Mungu aliyejaa uhuruma na upole, tayari kujisadaka yeye mwenyewe ili kuweza kukutana nasi kama  fundisho la  Baba na  Mtoto mpotevu (Lk 15, 11-32). Papa ameongeza: “Wakati mmoja, mtu aliuliza, sijui kama ilikuwa kwa mama au bibi yangu, kwani walinisimulia: “Lakini nifanye nini, muda huu?”Jibu  “Msikilize Mungu, Yeye atakuambia la kufanya. Fungua moyo wako kwa Mungu”, ni ushauri mzuri. Na kwa kuongezea Papa amesema: Ninakumbuka mara moja, katika hija ya vijana, ambayo hufanyika mara moja kwa mwaka kwenye Madhabahu ya  Luján, kilomita 70 kutoka jiji la Buenos Aires: inachukua siku nzima kufika huko; Nilikuwa na tabia ya kuungamisha  wakati wa usiku. Alikaribia, kijana  mwenye umri wa miaka 22, akiwa na tattoos. Mungu wangu, nilifikiri hii itakuwa nini?”. Naye akaniambia: “Unajua, nimekuja kwa sababu nina tatizo kubwa na nilimweleza mama yangu kuhusu hilo na mama yangu akaniambia: ‘Nenda kwa Mama Yetu, fanya hija, na Mama Yetu atakuambia’. Na nimekuja. Nilikuwa na mawasiliano na Biblia hapo, nilisikiliza Neno la Mungu na likagusa moyo wangu na sina budi kufanya hivyo, hivyo..”. Papa Francsiko aliongeza “Neno la Mungu linagusa moyo wako na kubadilisha maisha yako. Na kwa hivyo niliona hiyo mara nyingi. Kwa sababu Mungu hataki kutuangamiza, Mungu anataka tuwe na nguvu zaidi, wema  kila siku”.

Anayebaki mbele ya Msulibiwa anahisi amani mpya, anajifunza kutokuwa na hofu ya Mungu, kwa sababu Yesu juu ya msalaba haogopeshi mtu, ni picha inayoonesha asiye na nguvu kabisa na pamoja na upendo uliojaa, mwenye uwezo wa kukabiliana kila jaribio kwa ajili yetu. Watakatifu daima walikuwa na upendeleo wa Yesu Msalaba. Simulizi ya Mateso ya Yesu ni njia kiongozi  kwa ajili ya kujikabili na ubaya bila kuhusika: ndani mwake hakuna hukumu na wala kujikabidhi, kwa sababu ni kwa njia ya mwanga mkubwa zaidi, mwanga wa Pasaka ambao unaruhusu kuona matendo yasiyosemekana, hatima kubwa zaidi ambayo hakuna kizuizi, kizingitia au kushindwa kunaweza kuthibitishwa. “Neno la Mungu sikuzote hukufanya utazame upande mwingine: yaani, kuna msalaba, hapa, ni mbaya, lakini kuna jambo lingine, tumaini, ufufuko. Neno la Mungu linakufungulia milango yote, kwa maana Yeye, Bwana, ndiye mlango. Hebu tuchukue Injili, na tuichukue Biblia mkononi: dakika tano kwa siku, si zaidi. Ibebe Injili  mfukoni pamoja nawe, kwenye mfuko wako, na unaposafiri, ichukue na uisome kidogo wakati wa mchana, ukiruhusu Neno la Mungu liwe karibu na moyo wako. Fanya hivyo utaona jinsi maisha yako yatakavyobadilika kwa ukaribu wa Neno la Mungu”. Kwa kuongezea “Ndiyo Padre lakini nimezoea kusoma Maisha ya Watakatifu”: ndiyo hiyo ni nzuri, lakini usiliache Neno la Mungu. Chukua Injili pamoja nawe, na uisome hata dakika moja tu kwa siku”, Papa ameshauri.

Baba Mtakatifu amebainisha kwamba ni vizuri kufikiria maisha na Bwana kama uhusiano mmoja wa urafiki ambao unakua siku baada ya siku. “Je mlisha fikiria hilo? Ni njia! Tufikirie Mungu anayetupenda, anayetutaka kama marafiki. Urafiki na Mungu una uwezo wa kubadilisha moyo ni moja ya zawadi kubwa za Mungu. Tunaye baba mpole, Baba mpendelevu, Baba ambaye anatupenda, ambaye alitupenda daima: tunapofanya uzoefu, moyo unafunguka na kuanguka mashaka, hofu, na hisia za kutostahili. Hakuna kinachoweza kupinga upendo huo wa kukutana na Bwana. Baba Mtakatifu amesema, hiyo inatukumbusha msaada mwingine mkubwa, wa zawadi ya Roho Mtakatifu ambaye yupo ndani mwetu na ambaye anajenga, anauhisha Neno la Mungu tunalolisoma, anatushauri maana mpya, anafungua milango ambayo utafikiri ilikuwa imefungwa, anaelekeza njia za maisha mahali ambapo utafikiri ilikuwa ni giza tu na mkanganyiko.

Baba Mtakatifu Francisko ameuliza swali ikiwa wanasali kwa Roho Mtakatifu. “Lakini je ni nani huyo hasiyejulikana. Ndiyo sisi tunasali kwa Baba, sala ya Baba Yetu, Tunasali kwa Yesu, lakini tunamsahau Roho! Kwa kutoa mfano amesema siku moja akiwa anafanya katekesi kwa watoto, aliuliza swali “ Je kwa upande wetu Roho Mtakatifu ni nai?. Na mtoto mmoja akasema ndio mimi ninajua!” Na Papa akauliza ni nani? Mtoto akajibu ni (“Il paralitico”),yaani (aliye pooza). Kwani yeye alikuwa anasikia ‘Paraclito’ yaani Mfariji kwa kufikiria ni aliyepooza. Kwa kuongeza, papa amesema: “Na mara nyingi, hii ilinifanya nifikiri,  Roho Mtakatifu yuko kwa ajili yetu, kana kwamba yeye ni mtu ambaye hazingatiwi. Roho Mtakatifu ndiye anayetoa uzima nafsi yako! Hivyo Mruhusu aingie. Ongea na Roho unapozungumza na Baba, unapozungumza na Mwana: zungumza na Roho Mtakatifu, ambaye hana chochote kilichopooza! Ndani yake mna nguvu ya Kanisa, yeye ndiye anayekupeleka mbele. Roho Mtakatifu ni mang’amuzi katika matendo, kwa uwepo wa Mungu ndani mwetu ni zawadi kubwa sana ambayo Baba anahakikishia wale ambao wanamuomba (Lk 11,13). “Je Yesu anaitaje? Zawadi “ Mbakini hapa Yerusalemu kwa kusubiri zawadi ya Mungu ambayo ni Roho Mtakatifu. Inavutia kupeleka maisha katika urafiki na Roho Mtakatifu, kwa sababu yeye anakubadilisha, Yeye anakufanya ukue, ”Papa ameongeza.

Liturujia ya masifu inaanza kwa vipindi vya sala ya siku kwa maombi haya: Ee Mungu njoo uniokoe, Bwana njoo haraka uwe msaada wangu”. Bwana unisaidie! Kwa sababu peke yangu siwezi kwenda mbele, siwezi kupenda na siwezi kuishi… Maombi haya ya wokovu ndiyo maombi yasiyoisha ambayo yanabubujika kutoka katika kina cha uwepo wetu. Mang’amuzi yana lengo hilo la kujua wokovu unaotendwa na Bwana katika maisha yangu, unanikumbusha kuwa kamwe mimi siko peke yangu na ikiwa ninapambana, ni kwa sababu jambo hilo ni muhimu.  “Roho Mtakatifu yuko pamoja nasi daima. Papa kwa kutoa mfano amesema: “ mwingine anaweza kusema alifanya jambo baya, je lazima aende kuungama, kwani hawezi kufanya lolote…”. Lakini, je ulifanya jambo baya?  Basi Ongea na Roho aliye pamoja nawe na umwambie: “Nisaidie, nimefanya jambo hili baya sana”. Lakini usighairi mazungumzo na Roho Mtakatifu.  Mwambie “Padre ,  mimi niko katika dhambi ya mauti”: haijalishi, zungumza naye ili aweze kukusaidia kupokea msamaha. Usiache kamwe mazungumzo haya na Roho Mtakatifu”, Papa ametoa ushauri. Kwa misaada hiyo, ambayo Bwana anatupatia na hatupaswi kuogopa. Hivi endeleni mbele na kuwa na ujasiri na kwa furaha! Amehitimisha Papa.

Katekesi ya Papa 21 Desemba 2022
21 December 2022, 16:12