Baba Mtakatifu Mstaafu: Historia: Maisha, Utume na Mchango Wake Kwa Kanisa la Afrika
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amefariki dunia Jumamosi saa 3: 34 Asubuhi tarehe 31 Desemba 2022 akiwa na umri wa miaka 95, katika makazi yake kwenye Hosteli ya Mater Ecclesiae iliyoko kwenye Bustani za Vatican tangu mwaka 2013 alipong’atuka kutoka madarakani kutokana na sababu za umri kuwa mkubwa. Alifanya maamuzi haya magumu, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine, aweze kulitumikia Kanisa la Kristo Yesu, kwa ari na moyo mkuu. Kwa uchungu na majonzi makuu, lakini tukiwa na tumaini la maisha ya uzima wa milele, tunawaalika kuungana na Mama Kanisa kwa ajili ya kumwombea maisha ya uzima wa milele Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Itakumbukwa kwamba, Joseph Aloisius Ratzinger, alizaliwa tarehe 16 Aprili 1927 huko Markti nchini Ujerumani. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 29 Juni 1951 wakati wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na miamba ya imani. Tangu wakati huo, vipaji vyake yalianza kung’ara na kuwa ni kati ya wanataalimungu mahiri waliojipambanua katika miaka 1950 ndani na nje ya Ujerumani. Akabahatika kupata nafasi ya kufundisha vyuo kadhaa vya taalimungu nchini Ujerumani. Tarehe 28 Mei 1977, Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising na tarehe 27 Juni 1977 akateuliwa kuwa Kardinali.
Hili ni tukio ambalo liliwashangaza watu wengi, kwani Askofu mkuu Joseph Ratzinger hakuwa na uzoefu sana katika shughuli za kichungaji kama Askofu. Akaliongoza Jimbo kuu la Munich na Freising kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1982. Tangu mwaka 1982 hadi mwaka 2005 alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa; Rais wa Tume ya Taalimungu Kimataifa pamoja na Tume ya Biblia Kimataifa pamoja na Dekano wa Baraza la Makardinali. Tarehe 19 Aprili 2005 akachaguliwa kuwa Papa wa 265, akiwa na umri wa miaka 78. Katika hotuba yake ya kwanza kabisa iliyosheheni unyenyekevu mkubwa alisema, baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II aliyekuwa maarufu sana, Makardinali wamemchagua yeye, mtu wa kawaida na mfanyakazi katika shamba la Bwana kuwa Papa, lakini Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anatambua jinsi ya kuendeleza kazi yake hata kwa kutumia vyombo dhaifu kama yeye. Baba Mtakatifu Benedikto XVI akajiweka chini ya sala na maombezi ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Tarehe 24 Aprili akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kusimikwa rasmi kuwa ni Kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki., Khalifa wa Mtakatifu Petro. Tarehe 7 Mei akasimikwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliwahi kusema, vishawishi vikuu vinavyowandama wanadamu katika ulimwengu mamboleo ni: Uchu wa fedha na mali; madaraka na elimu! Haya ni mambo ambayo yameendelea kusababisha kinzani na mipasuko mbali mbali katika maisha ya mwanadamu! Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, amekuwa ni kiongozi mwenye busara, hekima na nguvu ya ndani, aliyethubutu kuleta mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa! Lakini kama ilivyo kwa baadhi ya watu, walitaka kumnyong’onyeza kwa sababu zao binafsi! Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alianzisha mchakato wa mageuzi makubwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, lakini alikumbana na “vizingiti vikubwa” katika maisha na utume wake. Ni wakati wa uongozi wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI, viongozi kutoka Barani Afrika wakaanza kupata nafasi za uongozi wa juu kama wakuu wa Mabaraza ya Kipapa na wengine, kutumwa sehemu mbali mbali za dunia kama Mabalozi wa Vatican. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alikazia zaidi: Imani, Matumaini na Mapendo mambo msingi ambayo yangewawezesha waamini kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ameandika Nyaraka za Kitume zifuatazo: “Deus Caritas Est” yaani “Mungu ni upendo”, “Spe salvi” yaani “Matumaini yanayookoa”; Caritas in veritate yaani “Ukweli katika upendo” na Wosia wa kitume, ambao haukuumaliza kuuandika kama hitimisho la maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni “Lumen fidei” yaani “Mwanga wa Imani. Baada ya maadhimisho ya Sinodi mbali mbali, Baba Mtakatifu Mstaafu aliandika Wosia zifuatazo”: Verbum Domini” yaani “Neno la Mungu”; “Ecclesia in Medio Oriente yaani “Kanisa Mashariki ya Kati”; “Sacramentum Caritatis” yaani “Sakramenti ya upendo”; Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika.” Katekisimu ya Kanisa Katoliki: muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na maisha ya Sala na hatimaye, maadhimisho ya Mwaka wa imani, ilikuwa ni fursa ya kufanya rejea tena katika mafundisho makuu ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican, ili kuendelea kuyapyaisha na kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa. Familia ya Mungu Barani Afrika inamkumbuka kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa kuridhia maamuzi ya Mtakatifu Yohane Paulo II ya kuadhimisha Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Barani Afrika, iliyofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4-25 Oktoba 2009. Mtakatifu Yohane Paulo II alikwisha tangaza nia hii hapo tarehe 13 Novemba 2004, lakini akafariki dunia kabla ya kutekeleza ndoto hii ambayo imekuwa na mafao makubwa kwa Kanisa la Mungu Barani Afrika.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI wakati wa hija yake ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 17-23 Machi 2009 alizindua rasmi hati ya kutendea kazi yaani “Instrumentum Laboris” huko Cameroon na Angola. Tarehe 9 Novemba 2011 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akawasilisha Wosia wa Kitume “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” huko Benin kwa heshima ya Kardinali Bernardin Gantin aliyeishi na kufanya naye kazi kwa miaka mingi mjini Roma. Alionesha ujasiri wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kanisa la Mungu Barani Afrika. Sekretarieti kuu ya Sinodi ya Maaskofu ikasema, Kanisa ni Jumuiya ya waamini wanaopaswa kujipatanisha na Mungu na jirani zao, ili kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya haki, amani na upatanisho. Bara la Afrika limekuwa likikabiliwa na vita, migogoro na kinzani za aina mbali mbali; unyonyaji sanjari na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya huruma na mapendo, kumbe, jitihada zote za haki, amani na upatanisho zinapaswa kupata chimbuko na hatima yake kwenye Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa muhtasari tu, Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” unaongozwa na kauli mbiu “Ninyi ni chumvi ya dunia ... Ninyi ni nuru ya ulimwengu” Mt. 513:14.
Kanisa Barani Afrika kama chombo cha haki, amani na maridhiano.” Wosia huu umegawanyika katika sehemu kuu mbili: Sehemu ya kwanza: Tazama, nayafanya yote kuwa mapya: Kanisa katika huduma ya upatanisho, haki na amani. Familia ya Mungu Barani Afrika inahimizwa kuwa ni shuhuda katika huduma ya upatanisho, haki na amani kama chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kristo katika moyo wa maisha ya Kiafrika ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu kupatanishwa kwanza na Mwenyezi Mungu na hatimaye, kuanza mchakato wa kujipatanisha na jirani zao kwani upatanisho hushinda matatizo, hurudisha heshima ya watu binafsi na hufungua njia ya maendeleo na amani ya kudumu kati ya watu na katika ngazi mbali mbali. Hii ni changamoto ya kujikita katika haki na kuhakikisha kwamba, jamii inajenga na kudumisha mifumo inayosimamia na kutekeleza haki. Mwaliko kwa waamini ni kuishi kadiri ya haki ya Kristo inayofumbatwa katika toba, wongofu wa ndani na upendo wa dhati kabisa! Baba Mtakatifu Mstaafu anasema, upendo katika ukweli ni chemchemi ya amani inayokita mizizi yake katika huduma halisi ya kidugu na kwamba, Kanisa ni chombo cha haki, amani na upatanisho.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume, “Dhamana ya Afrika”, anabainisha mahali pa kufanyia kazi kwa ajili ya upatanisho, haki na amani: toba, wongofu wa ndani, kwa kujali utu na heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto kwa waamini kukimbilia katika kiti cha huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili kukuza na kudumisha umoja na mshikamano katika maisha ya kiroho. Mchakato huu hauna budi kwenda sanjari na utamadunisho wa Injili na uinjilishaji wa tamaduni mbali mbali Barani Afrika, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na Neno la Mungu yakipewa msukumo wa pekee katika maisha ya waamini. Haki, amani na upatanisho vipate chimbuko lake ndani ya familia, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kuwajali na kuwathamini wazee; kwa wanaume na wanawake kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na nyajibu zao katika familia na jamii kwa ujumla. Kanisa linapaswa kuwajali na kuwathamini vijana wa kizazi kipya, kwa kuwashirikisha katika maisha na utume wa Kanisa.
Ikumbukwe kwamba, watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, walindwe, waheshimiwe na kuthaminiwa; ukweli na unyenyekevu ni msaada mkubwa kutoka kwa watoto. Familia ya Mungu Barani Afrika, haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuheshimu na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kanisa Barani Afrika lisaidie juhudi za utawala bora; kwa kuheshimu utawala wa sheria, demokrasia shirikishi; uhuru na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuonesha mshikamano wa hali na mali kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Utu, heshima na haki zao msingi ni mambo ya kuzingatiwa na wote. Kanisa Barani Afrika linahamasishwa kujenga na kudumisha utandawazi wa upendo na mshikamano. Juhudi hizi zikite mizizi yake katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kujenga umoja na udugu wa familia ya Mungu inayowajibika. Ni katika kutekeleza yote haya, Kanisa Barani Afrika litaweza kuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Baba Mtakatifu Mstaafu katika Wosia wake wa Kitume, "Africae munus" yaani “Dhamana ya Afrika”: Sehemu ya Pili anakazia umuhimu wa kushirikishana karama. Maaskofu wanahimizwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano na familia ya Mungu, ili kuendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.
Maaskofu wawe ni wachungaji wema na watakatifu; waaminifu na wakweli katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mapadre wahakikishe kwamba, wanaendelea kujipyaisha katika maisha na utume wa Kanisa hasa katika Maandiko Matakatifu na Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kukabiliana na changamoto mamboleo. Mapadre wanapaswa kujikana na kubeba vyema Misalaba yao, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Ni wakati wa kuendelea kuiga mifano bora ya wamisionari na watakatifu kutoka Barani Afrika. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anathamini sana mchango wa watawa na makatekista Barani Afrika pamoja na kuwahimiza waamini walei kujifunga kibwebwe ili kuweza kuyatakatifuza malimwengu, kwa njia ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kanisa Barani Afrika liendelee kuwekeza katika sekta ya elimu, huduma ya afya na katika teknolojia na ulimwengu wa mawasiliano ya jamii. Kanisa liendelee kuwafundisha waamini umuhimu wa Neno la Mungu na ushiriki makini katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa hususan: Ekaristi Takatifu chanzo na utimilifu wa maisha na utume wa Kanisa. Sakramenti ya Upatanisho ni muhimu katika maondoleo ya dhambi, ili hatimaye, kuishi: kwa upendo, huruma, umoja na udugu wa kibinadamu. Juhudi zote hizi ziende sanjari na uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni mwanga wa ulimwengu. Huu ni wakati hata kwa watoto wa Mungu Barani Afrika kushiriki kikamilifu kwa ari na mwamko mpya wa shughuli za kimisionari ndani na nje ya Bara la Afrika. Uinjilishaji mpya Barani Afrika unafumbatwa katika huduma ya upatanisho, haki na amani. Mwishoni mwa wosia wake, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anawataka watu wa Mungu Barani Afrika kujipa moyo, kuinuka na kuanza safari ya haki, amani na upatanisho, kwani wao ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu.
Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013, Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, (1858) sanjari na Kumbu kumbu ya Mkataba wa Lateran (1929), Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alipoamua kwa hiyari yake mwenyewe, kung’atuka kutoka madarakani kutokana na uzee pamoja na kuanza kuzorota kwa afya yake, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine, kuendeleza dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni wajibu unaofumbatwa katika utekelezaji wa majukumu haya kwa njia ya maadhimisho mbali mbali ya Mafumbo ya Kanisa, mikutano pamoja na hija za kitaifa na kimataifa. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI baada ya kutafakari kwa kina, akaona alikuwa anaishiwa nguvu za kuweza kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi mkuu. Hili ni tukio ambalo limeweka historia kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni kiongozi ambaye amewashangaza sana walimwengu, kwani walidhani kwamba, ni mtu aliyekuwa na uchu wa madaraka! Lakini, ukweli wa mambo utaendelea kushamiri katika historia ya maisha na utume wa Kanisa. Utashi wa kutaka kuleta mageuzi ndani ya Kanisa ni nguvu aliyoionesha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Kunahitajika ujasiri, hekima na busara, ikisukumwa na nguvu ya ndani, kuweza kuamua kukaa pembeni na kuendelea kusali kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa! Bravo, Papa Mstaafu Benedikto XVI! Papa Mstaafu Benedikto XVI aliliongoza Kanisa kwa hekima na busara, akalitaka Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuambata zaidi imani, matumaini na mapendo, mambo makuu yanayojionesha katika Nyaraka zake za Kitume. Aliwataka kwa namna ya pekee kabisa, viongozi kulisafisha Kanisa kutokana na kashfa mbalimbali, sakata ambalo limevaliwa njuga sasa na Baba Mtakatifu Francisko, yaani: nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo!