Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya VI ya Maskini Duniani 13 Novemba 2022
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, ikiwa kama watu wa Mungu wanataka kushinda utamaduni wa kifo na kukombolewa kutoka katika udhalimu, wanapaswa kufuata ufukara wa Kristo Yesu, kwa kushiriki na kuambata maisha yanayosimikwa katika upendo, kwa kushirikiana na wengine katika kuumega mkate na kuishi kwa umoja kama ndugu wamoja, kwa kuanzia kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mchakato wa kuwaweka huru maskini wanateswa na baa la umaskini na matajiri wanaokosa furaha na utulivu wa ndani kwa sababu ya ubatili, ili wote kwa pamoja waweze kuwa na matumaini mapya. Mama Kanisa anawajibika kimaadili kuwasaidia na kuwahudumia maskini: kiroho na kimwili na ndiyo maana baada ya kufunga rasmi Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, ameanzisha Siku ya Maskini Duniani, ili Jumuiya za Kikristo sehemu mbali mbali za dunia, ziweze kuwa alama wazi ya upendo wa Kristo Yesu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Siku hii ni muhimu sana ili kuonesha na kushuhudia upendeleo wa Kristo Yesu kwa maskini, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasikiliza, kuwahudumia na kuwaonesha maskini upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii kwa kutambua kwamba, hata wao wameumbwa na wanapendwa na Baba wa mbinguni.
Siku ya Maskini Duniani ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano na tabia ya maamuzi mbele. Maadhimisho haya yanakamilishwa kwa namna ya pekee, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Huu ni ufalme wa kweli na wa uzima; ufalme wa utakatifu na wa neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Ufalme wa Kristo Yesu unafumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, ushuhuda wa utimilifu wa upendo wa Mungu na chemchem ya maisha mapya wakati wa Pasaka. Siku ya Maskini Duniani iwe ni nafasi ya kuwaonjesha huruma na upendo maskini na wahitaji; ni siku ya kuwakaribisha na kuwakirimia wageni; Siku inayowasaidia waamini kumwilisha imani yao katika matendo; watu wawe tayari kupokea msaada na kujitahidi kuishi kwa kuzingatia mambo msingi ya maisha, tayari kujiachilia kwa huruma ya Mungu. Iwe ni Siku ya kumwilisha Sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni, ambayo kimsingi ni Sala ya Maskini, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wanaohitaji mambo msingi katika maisha. Sala ya Baba Yetu inawawajibisha waamini kupokea na kugawana hata kile kidogo kilichopo, tayari kuvunjilia mbali tabia ya uchoyo na ubinafsi, kwa kutoa nafasi ya kuwashirikisha wengine furaha ya ukarimu.
Siku ya Maskini Duniani iwe ni fursa makini ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; nafasi ya kutambua kwamba, maskini wanawasaidia waamini wenzao kutambua ukweli na tunu msingi za Kiinjili. Ikumbukwe kwamba, Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu inayoadhimishwa Jumapili ya 33 ya Kila Mwaka wa Kanisa. Kwa mara ya kwanza Siku hii iliadhimishwa kunako mwaka 2017. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani tarehe 13 Novemba 2022 yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2Kor 8:9. Baba Mtakatifu anachambua jinsi UVIKO-19 ulivyo sababisha ongezeko la maskini duniani; vita inavyoendelea kuwatumbukiza watu katika baa la umaskini na kwamba, umaskini wa Kristo uwawajibishe waamini kushirikiana na kushikamana katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha tunu msingi zinazosimikwa katika mshikamano, kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo.
Umaskini ni matokeo ya ukosefu wa haki, unyonyaji, vita na ugawaji mbaya wa rasilimali za dunia. Umaskini wa Kristo Yesu, unawawezesha waamini kuwa ni matajiri wa huruma na mapendo, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Charles de Foucauld aliyetangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 15 Mei 2022. Baba Mtakatifu Francisko anasema, maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamepelekea mamilioni ya watu kukosa fursa za ajira, hali ya uchumi Kitaifa na Kimataifa kuyumba sana; mahusiano na mafungamano ya kijamii kuporomoka na kwamba, vita ya Mataifa yenye nguvu zaidi duniani, imepelekea Ukraine kuathirika sana na kwamba, kwa sasa kilio kikuu ni watu wa Mungu wanataka kuona amani ya kudumu inatawala, akili na nyoyo za watu. Mamilioni ya watu wamelazimika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ugenini. Maisha yao yako hatarini kutokana na ukosefu wa maji safi na salama, chakula, huduma bora za afya na upendo kutoka kwa ndugu zao. Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani: “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake” iwe ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kama ilivyokuwa kwa Mitume walipotembelea wanajumuiya ya Yerusalemu walivyoongezewa na neema, baraka, furaha na utajiri mwingi kwa kuwasaidia ndugu zao waliokuwa katika dhiki kubwa.
Waamini wakawa wanakusanya sadaka kila wakati wa Dominika na huo ukawa ni mwanzo wa Sadaka ya Dominika ya Bwana, kielelezo cha furaha ya ndani, imani inayomwilishwa katika matendo na uwajibikaji katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kuhakikisha kwamba, jirani wanapata walau mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili. Dominika ni Siku ya Bwana, Neno la Mungu linasomwa na kutafakariwa, waamini wanashiriki katika chakula cha Bwana; Mashemasi wanawapelekea wagonjwa Ekaristi Takatifu majumbani mwao. Sadaka inatunzwa kwa ajili ya mahitaji ya maskini na wanyonge ndani ya jamii. Pole pole, ari na moyo huu ulianza kuzimika pole pole kama “Kibatari kisicho na mafuta.” Mtakatifu Paulo anawataka waamini kutekeleza na kutimiza wajibu wao. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kuwashukuru watu wa Mungu popote walipo kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Ukanda wa Mashariki ya Kati, Afrika ya Kati na Ukraine, licha ya changamoto wanazokumbana nazo wenyeji. Huu ni wakati wa kuendelea kujikita katika mchakato wa ukarimu kwa maskini na wahitaji zaidi kwa njia ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kamwe asiwepo maskini anayekufa kwa baa la njaa duniani.
Ukarimu usimikwe katika: amani na usalama wa raia na mali zao, kwa kuendelea kujikita katika: uhuru, uwajibikaji, udugu na mshikamano, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika fadhila ya: upendo, imani na matumaini kama msingi wa maisha na matendo yao. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni kielelezo cha huruma na upendo uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Kumbe, ujumbe wa Injili unapaswa kumwilishwa katika matendo na kwa njia hii watabarikiwa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujizatiti katika huduma ya upendo kwa maskini, kwani uchu wa fedha na mali ni kielelezo cha udhaifu wa imani, matumaini na upeo finyu wa maisha. Waamini wanahamasishwa kuwasaidia maskini kwa hali na mali pamoja na kusimama kidete katika msingi wa haki jamii na kuendelea kujikita katika toba, wongofu wa ndani, upendo kwa Mungu na jirani, kwani maskini na umaskini ni mambo msingi katika Injili, changamoto na mwaliko wa kupyaisha maisha mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Rej. Evangelii gaudium, 201. Kumbe, kuna haja ya kuwa na sera makini kwa ajili ya maskini pamoja na maskini wenyewe, ili kudumisha haki na usawa. Mwinjili Mathayo anawaalika waamini kujiwekea hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi. Rej. Mt 6: 19.
Waamini watambue kwamba, kuna mfumo wa umaskini unaosigina utu, heshima na haki msingi za binadanu na kuna ufukara unaowaweka watu huru, huu ni ufukara wa Kristo Yesu, chemchemi ya uhuru na amani ya kweli. Umaskini unaouwa ni matunda ya ukosefu wa haki, vita na ugavi tenge wa rasilimali za dunia na yote haya yanapata chimbuko lake katika utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kiasi hata cha kufisha maisha ya kiroho. Maskini wawasaidie waamini kutambua na kuambata mambo ya kweli na yale ya msingi katika maisha, kielelezo cha shukrani ya upendo; maskini ni shule ya fadhila za Kikristo. Ni mahali pa kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho na chemchemi ya ibada na chanzo cha neema. Ni shule inayowatakasa waamini dhambi zao, tayari kuambata utakatifu wa maisha, haki na amani. Ni katika muktadha wa ufukara wa Kristo Yesu, maisha ya waamini yana pyaishwa na kung’aa zaidi; kwa upendo unaowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi; upendo unaowalisha wenye njaa sanjari na kutetea utu na heshima yao, dhidi ya ukosefu wa haki. Kumbe, waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kugawana chakula na maskini, ili kujenga usawa na kuanza kujielekeza katika mchakato wa kuwakomboa maskini kutoka katika umaskini wao na matajiri kutoka ubatili na hali ya kujikatia tamaa.
Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alimtangaza Mwenyeheri Charles de Foucauld kuwa Mtakatifu tarehe 15 Mei 2022. Alikuwa ni mtu wa sala, ukimya, aliyependa kushirikisha wengine na hatimaye, akawa ni shuhuda na chombo cha ufukara wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko wa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwathamini maskini, kwani hawa ni watu waliopewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kristo Yesu hapa ulimwenguni; tangu kuzaliwa kwake hadi alipoitupa mkono dunia juu ya Mlima wa Kalvari. Waamini wajitahidi kuwa ni maskini wa kiroho; ndugu na wandani wa maskini; wamwige Kristo Yesu kwa maneno na matendo yao kama ilivyokua kwa Mtakatifu Charles de Foucauld aliyejisadaka kwa ajili ya maskini kwa matendo, kiasi hata akabahitika kushiriki katika mateso ya Kristo Yesu katika maisha yake ya kila siku. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu ana tumaini kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Sita ya Maskini Duniani tarehe 13 Novemba 2022 yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2Kor 8:9. Itakuwa ni Siku ya Neema na baraka, kama mwamini mmoja mmoja na waamini katika ujumla wao, watumie fursa hii kujiuliza ikiwa kama ufukara wa Kristo Yesu umekuwa ni mwandami wa safari ya maisha ya kila siku?