Uchungu wa Papa kwa waathirika wa ajali ya Ndege Tanzania
Na Angella Rwezaula, – Vatican.
Tanzania nzima inaomboleza kwa sababu ya watu 19 kufariki dunia na abiria 26 kuokolewa na wananchi wa kawaida, kuanzia na wavuvi. Ni kutokana na Ndege ya Shirika la Ndege la Precision Air yenye namba za usajili 5HPWF ambayo ilikuwa inatoka Dar es Salaam kwenda Bukoba kupitia Mwanza, Dominika tarehe 6 Novemba 2022 ambapo ilishindwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Bukoba kutokana na hali mbaya ya hewa na kutumbukia katika Ziwa Victoria mita chache kabla ya kufika Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Kutokana na maombolezo na uchungu huo, Baba Mtakatifu Francisko anaungana nao kwa kutuma telegramu katika Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania, iliyotiwa saini na Kardinali Pietro Parolin Katibu wa Vatican, kwamba Papa anawatumia salamu za rambi rambi na kuwahakikishia ukaribu wake wa kiroho kwa watu wote waliokumbwa na mkasa huo.
Kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko amewaombea kwa Mwenyezi Mungu mapumziko ya milele marehemu wote na kuwatakia uponyaji kwa waliojeruhiwa na ili wapate nguvu wale ambao wanashiriki katika shughuli za uokoaji na kurejesha hali yao. Zaidi ya yote, Papa aliomba faraja na amani ya Mwenyezi Mungu kwa ndugu jamaa na marafiki wote waliokumbwa msiba huo mkubwa.
Ndege hiyo ya kampuni binafsi ya Precision Air, ilianguka ikiwa inakaribia kufika mji wa Bukoba, kaskazini-magharibi mwa nchi, baada ya kuondoka Dar es Salam, mji mkuu wa uchumi wa nchi ya Tanzania. Kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari vya ndani, ndege hiyo ilianguka majini umbali wa mita 100 kutoka uwanja wa ndege. Kwa maana hiyo watu 26 waliokolewa na 19 wakafariki wakiwemo marubani na wafanyakazi wawili kati ya watu 45.
Shuhuda nyingi za walionusurika zilienea kwenye mitandao ya kijamii tangu Jumapili hadi Jumatatu zikieleza jinsi ya kuanza safari yao na hadi tukio hilo. Na Taifa lilifanya tukio la kuaga miili kitaifa katika uwanja wa Mpira wa Kaitaba Bukoba, Jumatatu tarehe 7 Novemba 2022. Raha ya Milele Uwape ee Bwana na Mwanga wa Milele Uwaangazie na wapumzike kwa amani Amina.