Papa Francisko: Katika shida na mahangaiko yao, watu wa Mungu wamkimbilie Kristo Yesu ambaye ameteswa na kufa Msalabani, ameshinda dhambi, ubaya wa moyo na mauti! Papa Francisko: Katika shida na mahangaiko yao, watu wa Mungu wamkimbilie Kristo Yesu ambaye ameteswa na kufa Msalabani, ameshinda dhambi, ubaya wa moyo na mauti! 

Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu: Uhuru wa Kuabudu

Dominika ya 34 ya Mwaka, ni Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Huu ni wito na mwaliko kwa watu wa Mungu kuendelea kujiaminisha mbele ya Kristo Yesu, Bwana wa historia na nyakati zote ni zake. Katika shida na mahangaiko yao, watu wa Mungu wamkimbilie Kristo Yesu ambaye ameteswa na kufa Msalabani, ameshinda dhambi, ubaya wa moyo na mauti! Huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Papa Pio wa XI katika Waraka wake wa Kitume wa “Quas primas” yaani “Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu, tarehe 11 Desemba 1925 alianzisha rasmi Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu iliyokuwa inaadhimishwa hapo awali, mwishoni mwa Mwezi Oktoba ya mwaka, kabla ya Sherehe ya Watakatifu wote, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi Novemba kwa kutambua utakatifu wa Kanisa unaosimikwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Rej. Lumen gentium 39. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican waliihamishia Sherehe hii katika Dominika ya 34 inayofunga rasmi mwaka wa Kanisa. Ufalme wa Kristo unakita mizizi yake katika akili, utashi na nyoyo za watu wenye mapenzi mema, kama kielelezo cha upendo. Huu ni Ufalme ambao unapata chimbuko lake kutoka katika Maandiko Matakatifu na kwa namna ya pekee kushuhudiwa kwenye Agano Jipya pale Pilato alipomuuliza ikiwa kama Kristo Yesu alikuwa ni Mfalme. Rej. Yn 18: 37. Kristo Yesu ni Mfalme na Mkombozi wa Ulimwengu na kwamba, watu wamewekeza imani, mapendo na matumaini yao kwake. Huu ni Ufalme wa maisha ya kiroho; Ufalme wa Ulimwengu wote unaomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao yake.

Hekima ya Mungu Imetundikwa Msalabani: Uhuru wa kweli.
Hekima ya Mungu Imetundikwa Msalabani: Uhuru wa kweli.

Huu ni Ufalme wa milele na wa Ulimwengu wote; Ufalme wa kweli na uzima; Ufalme wa utakatifu na wa neema; Ufalme wa haki, mapendo na amani. Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu, Mama Kanisa anapenda kukazia zaidi kuhusu: Uhuru wa kidini, uhuru wa kuabudu na uhuru wa dhamiri nyofu, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kadiri ya Maandiko Mtakatifu. Mama Kanisa anapenda kuendeleza dhamana na utume wake wa kutangaza, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa ulimwenguni. Lengo kuu la Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu ni kuendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha: Utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na kukoleza maisha adili  na matakatifu, ili mwisho wa siku, waamini waweze kuunganika kwa pamoja na Kristo Yesu katika Ufalme wake wa mbinguni; Ufalme ambao hauna mwisho. Hii ni changamoto kwa waamini kuwa makini ili wasijikute wanaelemewa na hatimaye, kutumbukizwa na kumezwa na malimwengu. Kristo Yesu awe ni mtawala wa maisha yako na Serikali inayokuongoza. Kristo Yesu ni mtawala wa mbingu na dunia, changamoto na mwaliko kwa waamini kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuingia na hatimaye kushiriki katika Ufalme wa Kristo Yesu milele yote.

Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu tangu mwaka 1925
Sherehe ya Kristo Mfalme wa Ulimwengu tangu mwaka 1925

Uhuru wa Kanisa unapata chimbuko lake katika uhuru wa Kristo Yesu, Mfalme wa Ulimwengu. Watunga sera na sheria mbalimbali watekeleze dhamana na wajibu huu kwa kuzingatia Amri za Mungu; haki na amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi dhidi ya vita, chuki na uhasama kati ya watu wa Mataifa na matokeo yake ni mateso na mahangaiko yasioyokuwa na kifani kwa watu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Utambuzi, Jumatano tarehe 16 Novemba 2022, amewakumbusha waamini kwamba, Dominika ya 34 ya Mwaka, ni Sherehe ya Kristo Yesu Mfalme wa Ulimwengu. Huu ni wito na mwaliko kwa watu wa Mungu kuendelea kujiaminisha mbele ya Kristo Yesu, Bwana wa historia na nyakati zote ni zake. Katika shida na mahangaiko yao, watu wa Mungu wamkimbilie Kristo Yesu ambaye ameteswa na kufa Msalabani, ameshinda dhambi, ubaya wa moyo na mauti!

Sherehe Kristo Mfalme
16 November 2022, 17:37