Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni, alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mtandao wa Maduka ya Dawa Asilia Kimatifa “Rete di Farmacie Apoteca Natura.” Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni, alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mtandao wa Maduka ya Dawa Asilia Kimatifa “Rete di Farmacie Apoteca Natura.”   (Vatican Media)

Papa Francisko: Tiba Asilia Na Utunzaji Bora wa Mazingira

Ubunifu ni hitaji muhimu kwa wakati huu katika mchakato wa kulinda na kutunza ikolojia, kati ya binadamu na kazi ya uumbaji. Ubora huu unanogeshwa na sera na mikakati ya Mtandao wa Maduka ya Dawa Asilia Kimatifa unaopania pamoja na mambo mengine, kujenga mahusiano na mafungamano na watu asilia, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza ushauri mahalia

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtandao wa Maduka ya Dawa Asilia Kimatifa “Rete di Farmacie Apoteca Natura” unawajumuisha zaidi ya wafamasia maalum 5, 000 Kimataifa, wenye uwezo wa kuwasikiliza na kuwaongoza watu katika safari yao ufahamu wa afya, umuhimu wa dawa asilia katika mahitaji ya matibabu na kinga sanjari na ushirikishwaji katika mtandao wa uchaguzi na ugavi wa dawa asilia, kwa kuzingatia utu, heshima, haki msingi na mazingira anamoishi mgonjwa. Wafamasia hawa wanatumia uwezo wa dawa asilia kutoka sehemu mbalimbali za dunia kupitia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kisasa ili kuboresha afya ya watu na sayari dunia. Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni, alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mtandao wa Maduka ya Dawa Asilia Kimatifa “Rete di Farmacie Apoteca Natura.” Katika hotuba yake aliwashukuru na kuwapongeza kwa kutumia vyema kipaji chao cha ubunifu kwa ajili ya kutengeneza fursa za ajira; kwa kulinda na kuhifadhi mazingira bora nyumba ya wote; mambo yanayoweka uwiano mzuri kati ya binadamu na kazi ya uumbaji na kwamba, huo kamwe si uchawi wala mazingaombwe. Misitu ya asili ina utajiri mkubwa wa miti na mimea ambayo inaweza kutumika kwa ajili ya tiba asilia kwa watu wengi, kama ilivyo katika Ukanda wa Amazonia.

Tiba asilia na utunzaji bora wa mazingira ni chanda na pete
Tiba asilia na utunzaji bora wa mazingira ni chanda na pete

Ubunifu ni hitaji muhimu kwa wakati huu katika mchakato wa kulinda na kutunza ikolojia, kati ya binadamu na kazi ya uumbaji. Ubora huu unanogeshwa na sera na mikakati ya Mtandao wa Maduka ya Dawa Asilia Kimatifa unaopania pamoja na mambo mengine, kujenga mahusiano na mafungamano na watu asilia, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza ushauri kutoka kwa watu mahalia na hatimaye, kuufanyia kazi. Hii ndiyo namna bora ya kuwekeza katika huduma ya afya inayozingatia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Jambo la msingi ni kwamba, Mtandao huu unazingatia: utu, heshima na haki msingi za wazee na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa hakika tiba asilia haziwezi kukidhi mahitaji ya sera na mikakati ya tiba Kitaifa, lakini walau tiba asilia inachangia katika mchakato wa maboresho ya afya kwa watu maskini.

Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini
Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini

Kwa maneno machache anasema Baba Mtakatifu Francisko huu ni muhtasari wa amani ya ndani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Amani na utulivu wa ndani ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu. “Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini. Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa.” Rum 8:20.22. Ni katika muktadha huu, mwanadamu anaweza kugundua mpango na mwelekeo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu yaani: matumaini ya wokovu na ushirika kwa namna ya pekee, yanafumbatwa katika kazi ya uumbaji. Lakini kwa bahati mbaya katika ulimwengu wa utandawazi unaoonekana kana kwamba, umeungana na kuwa kama “Kijiji”, bado ule utamaduni wa ulaji wa kupita kiasi pamoja na ule wa kutupa bado unatawala kupita kiasi. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha utunzaji bora wa mazingira kwa kusikiliza na kujibu “Kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini” katika uhalisia wa maisha ya kila siku kila mtu kadiri ya hali na mazingira yake.

Msitu wa Amazonia ni amana na utajiri mkubwa kwa maendeleo ya wengi
Msitu wa Amazonia ni amana na utajiri mkubwa kwa maendeleo ya wengi

Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko katika “Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anawahimiza watu wote wa Mungu kujikita katika utamaduni wa utunzaji Bora wa mazingira nyumba ya wote, mwaliko wa kuingia katika tiba muafaka kwa ajili ya amani na utulivu; dhamana inayoweza kuendelezwa na kuragibisha katika uhalisia wa maisha ya watu wa kawaida. Huu ni mwaliko kwa wadau mbalimbali kuendelea kuonesha ubinifu kwa ajili ya kutengeneza mfumo wa uchumi mbadala unaosimikwa katika mahitaji ya mtu mzima, ustawi na maendeleo ya wengi.

Papa Tiba Asilia
22 November 2022, 14:19