Tafuta

Matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) unaofanyika huko Sharm El-Sheikh, Misri: Mshikamano Matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) unaofanyika huko Sharm El-Sheikh, Misri: Mshikamano   (AFP or licensors)

PAPA FRANCISKO: Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP27

Papa Francisko: Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira haina budi kupewa kipaumbele cha pekee kama ilivyo pia kwa sekta ya afya na vita sehemu mbalimbali za dunia, wito kwa wote ni wongofu wa kiikolijia unaosimikwa katika wongofu wa kijumuiya ili kuleta mabadiliko ya endelevu na ya kudumu; mambo yanayopaswa pia kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa: Mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) unaofanyika huko Sharm El-Sheikh, Misri kuanzia tarehe 6-18 Novemba 2022, pamoja na Mkutano wa 15 wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai (COP-15) utakaofanyika kuanzia tarehe 7-19 Desemba 2022 huko Montreal, Canada, itasaidia kuunganisha familia ya binadamu katika mchakato wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika dimbwi la umaskini na magonjwa ya mlipuko. Ikolojia ya maisha ya kiroho iwahamasishe waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na shauku ya kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwa kufungamanisha maisha ya kiroho na utunzaji bora wa mazingira, kwa kutambua uwepo angavu wa Mungu katika kazi ya uumbaji, kwa kuonesha moyo wa ukarimu na kujali, kwa kutambua kwamba, ulimwengu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, huu ni mwaliko wa kujitoa sadaka kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu.  

Changamoto za mabadiliko ya tabianchi zishughulikiwe Kimataifa
Changamoto za mabadiliko ya tabianchi zishughulikiwe Kimataifa

Kuna kilio kikubwa cha Mama Dunia na maskini, kutokana na ulaji wa kupindukia unaosababisha majanga makubwa katika maisha ya mwanadamu. Wajibu kwa ajili ya dunia ya Mwenyezi Mungu maana yake ni kwamba, wanadamu kwa kujaliwa akili, wanapaswa kuheshimu sheria za maumbile na uwiano uliopo kati ya viumbe vya dunia hii. Kazi ya uumbaji na kilio cha maskini ni mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee, bila kuwasahau watu mahalia ambao kimsingi wamekuwa wahanga wa athari za mabadililo ya tabianchi kama vile: ukame wa kutisha, mafuriko, vimbunga pamoja na ongezeko kubwa la kiwango cha joto duniani. Lakini, ikumbukwe kwamba, kilio cha maskini kina nguvu kwani kinapanda hadi mbinguni. Uchoyo na ubinafsi ni sababu kubwa ya kilio cha Mama Dunia na maskini na kwamba vijana wanawataka watu wazima, kusimama kidete kulinda ikolojia ya ulimwengu huu, kwa kuheshimu kazi ya uumbaji; kwa toba na wongofu wa ndani, kwa kujenga na kudumisha urafiki mpya na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani.

Maskini ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi
Maskini ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi

Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira haina budi kupewa kipaumbele cha pekee kama ilivyo pia kwa sekta ya afya na vita sehemu mbalimbali za dunia, wito kwa wote ni wongofu wa kiikolijia unaosimikwa katika wongofu wa kijumuiya ili kuleta mabadiliko endelevu na ya kudumu; mambo yanayopaswa pia kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa. Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) uliofunguliwa tarehe 6 Mwezi Novemba hadi 18 Novemba 2022 ni sehemu ya mchakato kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa vitendo Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 13 Novemba 2022 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameyaelekeza mawazo yake kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) unaoendelea huko Sharm El-Sheikh, Misri. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itajizatiti na hatimaye, kufanya maamuzi magumu yanyosimikwa katika ujasiri na hali ya kujiamini katika utekelezaji kwa vitendo Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21.

Athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ya Kimataifa.
Athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ya Kimataifa.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) alionesha jinsi ambavyo Vatican katika sera na mikakati yake ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote inavyoendelea kutoa ushirikiano kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuridhia Makubaliano ya COP27 hadi kufikia mwaka 2050. Kuendelea kujikita katika mchakato wa kuragibisha elimu ya ikilojia na maendeleo fungamani ya binadamu. Amesema, changamoto na matatizo yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji toba na wongofu wa ndani pamoja na maamuzi thabiti yanayopaswa kufanywa na kutekelezwa kwa ujasiri. Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Vita ya Tatu ya Dunia inayoendelea kupiganwa sehemu mbalimbali za dunia ni matukio yenye athari kubwa kisiasa, kiuchumi na kijamii kiasi cha kutishia ulinzi na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa; Usalama na uhakika wa chakula duniani. COP27 ni fursa muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mambo makuu manne: Kudhibiti, kukabiliana, fedha, hasara na uharibifu (Mitigation, adaptation, finance, loss and damage).

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.

Kwa hakika kizazi cha Karne ya 21 kitakumbukwa kwa kubeba dhamana na wajibu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kiwango cha wastani wa nyuzi joto 1.5C ndicho kinachotakiwa vinginevyo, Jumuiya ya Kimataifa itakuwa inakabiliana na janga kubwa la uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Kumbe, changamoto ya kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 45% ifikapo mwaka 2030 ni muhimu sana. Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, kuna haja ya kutekeleza kwa vitendo upunguzaji wa nyuzi joto 1.5C kama ilivyobainishwa kwenye Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi. Kila nchi itaamua kiwango cha mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kiwango hicho kitategemea uchumi wa nchi husika na pia kiasi cha uzalishaji wa gesijoto. Kuongeza uwekezaji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa angalau asilimia 50% ya fedha za jumla za ufadhili wa umma wa mabadiliko ya tabianchi. Yote haya yanahitaji wongofu wa kiikolijia, unaojikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; maendeleo fungamani ya binadamu, mshikamano wa udugu wa kibinadamu sanjari na upendo. Wongofu wa kiikolojia unahitaji haki jamii hasa kwa watu maskini ambao wanaathirika vibaya kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Mkutano wa 15 wa Umoja wa Mataifa wa Bioanuwai (COP-15) utafanyika kuanzia tarehe 7 – 19 Desemba 2022 huko Montreal, Canada. “UN Biodiversity Conference (COP 15) 7 - 19 December 2022 Montreal, Canada.” Huku zaidi ya spishi milioni moja za wanyama na mimea zikitishiwa kutoweka na robo tatu ya mfumo wa ikolojia wa Dunia kubadilishwa na shughuli za binadamu, COP-15 lazima ianzishe mfumo mpya wa kimataifa ili kukomesha mmomonyoko wa bayoanuwai ifikapo mwaka 2030.

Papa COP27
14 November 2022, 15:20